Tamasha la Bibi Titi Mohamed lavunja rekodi Rufiji, wafunguka mazito

NA GODFREY NNKO

IMEELEZWA kuwa, Hayati Bibi Titi Mohamed alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa enzi zake ambaye licha ya kutokuwa mtu wa kelele, alikuwa jasiri, hodari, imara na aliyekirimiwa talanta ya kipekee katika uongozi kwa manufaa ya wengine.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 15, 2022 kwenye Kongamano la Tamasha la Bibi Titi Mohamed lililofanyika Ikwiriri katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani huku akitajwa kuwa mpigania Uhuru na aliyemuunga mkono Rais wa Kwanza wa Tanzania,Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kongamano hilo la aina yake ambalo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda pia liliwakutanisha pamoja viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali.
Miongoni mwao ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, wabunge, wanasiasa na wananchi kutoka ndani na nje ya Rufiji.

Halima Mzee

Katika kongamano hilo, mtoto pekee wa Bibi Titi Mohamed, Halima Mzee amesema kuwa, mama yake alikuwa mtu wa tofauti ambaye hofu ya Mungu ilimjaa ndani yake hivyo kumuwezesha kila analolifanya kutanguliza mbele maslahi ya watu.
"Kwanza napenda kuwashukuru waandaaji wa tamasha hili, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji (Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo) na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, naweza kuzungumza machache, wengi hawamjui Bibi Titi alikuwa wa namna gani.

"Kweli Bibi Titi alikuwa na hofu ya Mungu kwa yale aliyokuwa anafanya, alitanguliza mbele maslahi na maendeleo ya watu katika maisha yake.
"Aliwapenda sana watu, alikuwa na huruma nadhani kama angekuwepo leo angefurahia sana, Hata Rais wetu (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan) anafuata nyayo zake. Basi sisi kama wanafamilia hatuna budi kuwashukuru na kuwapongeza sana kwa kuendelea kumuenzi Bibi Titi na kumpa heshima yake," amesema Mtoto wa pekee wa Bibi Titi Mohamed, Halima Mzee.

Prof.Shani

Katika hatua nyingine,Prof. Shani Omari Mchepange kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ameiomba Serikali kuanzisha Makumbusho ya Bibi Titi ili yatumike kwa ajili ya kurithisha mchango na maono yake ya harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika (Tanzania) kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Prof.Shani amesema, Bibi Titi Mohamed ana historia kubwa inayopaswa kutuzwa kwani, licha ya kujitoa kwa ajili ya Taifa aliudhirishia ulimwengu kuwa, mwanamke si mtu wa chini.

"Bibi Titi Mohamed ninamuongelea kama mtumia fursa baada ya kuona tu akatumia fursa. Kama mnakumbuka kipindi kile mwanamke alikuwa duni sana, lakini yeye kwa uanamke wake akaona hii ni fursa kwake ya kuionesha jamii, Watanzania na Dunia nzima kwamba mwanamke sio mtu wa chini.
"Nadhani tukitoka hapa kwa wale ambao ni wanawake tuna wajibu wa kutumia fursa kwa kuendeleza siasa. Kwa Bibi Titi ametupa funzo muhimu sana,"amesema Prof.Shani.

Ameendelea kufafanua kuwa, "Fikiria kwa kipindi kile ukoloni ambao ulikuwepo usingeweza kutoka bila kufanya harakati za kuuondoa madarakani, sasa haki kama hiyo aliichukulia kama fursa ya kujipambanua na kujibainisha miongoni na wanawake na wanaume waliokuwepo. Aliweza pia kujiunga kuwa katika kitengo cha TANU yaani ndani ya chama ambacho kilileta uhuru.
"Mama huyu (Bibi Titi Mohamed) ametoa mfano mzuri sana na bora katika harakati za ukombozi wa nchi yetu. Lakini pia alikuwa na ushawishi mkubwa,"amefafanua Prof.Shani.

Katika hatua nyingine amebainisha kuwa,Bibi Titi Mohamed wakati huo alipita Nyumba kwa Nyumba kuhamasisha wanawake kwa wanaume. "Hii yote ilikuwa fursa kubwa sana kwake, ambalo kwetu tunapata somo maana kwa alionesha njia.
"Kipindi hicho pia cha ukoloni hawakuruhusu siasa na kazi na yeye hakuwa mfanyakazi, lakini alifanya kazi ya siasa kwa ushupavu na hakuwa na elimu kubwa, alikuwa na elimu ndogo, lakini aliweza kufanya kazi na kuhakikisha kwamba analeta mageuzi chanya kwa ajili ya jamii yake nchini na Afrika nzima."

Inaelezwa kuwa, Tanganyika ilipopata uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye aliyesifiwa na kupewa jina la Baba wa Taifa. Lakini bila ya Bibi Titi Mohamed, asingekuwa na ushawishi wa kutosha wa kufanikiwa kuikomboa Tanganyika katika mikono ya wakoloni.
Bibi Titi Mohamed ambaye alizaliwa 1926 kwenye familia ya Kiislam. Kama wenzake wengi wa wakati huo, hakupata elimu rasmi, lakini alijifunza mengi kutoka kwa wazazi wake na familia yake kwa ujumla.

Kila wakati kabla ya hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa akiimba ili kuwahamasisha watu wasikilize, ndiyo maana tunaweza kusema kwamba, nyuma ya mafanikio ya Mwalimu Nyerere alikuwa Bibi Titi.
Katika miaka ya 1950, alikuwa ni miongoni mwa wale waliopigania uhuru wa Tanganyika kutoka ukoloni wa Uingereza akiwa pamoja na Mwalimu Julius Nyerere chini ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU).

Aidha,Bibi Titi alikuwa ni mwanamke wa kwanza kujiunga na harakati mbalimbali za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mwanzoni mwa harakati zake za kisiasa, alifanikiwa kulishawishi kundi kubwa la wanawake kujiunga pamoja naye.
Kama kiongozi wa tawi la wanawake la chama cha TANU, alikuwa na jukumu la kuwashawishi wanawake kuunga mkono maoni na sera za TANU.

Pia baada ya uhuru wa Tanganyika na katika miaka ya mwanzo ya kuundwa kwa Tanzania, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bibi Titi alipewa uwaziri chini ya uongozi wa Rais Julius Nyerere.
"Tunaona aliachwa hadi na mume wake, lakini hakurudi nyuma alisimama kidete, hadi anakuwa mwanasiasa mkubwa ndani ya Taifa na mzalendo. Hadi anavuka mipaka ya nchi na kwenda nje tunashuhudia kabisa mama huyu alitoa fundisho kubwa ambalo lazima tumuenzi."

Kenya

Sauti yake na ujasiri wake ulipendwa na wengi, Tom Mboya na Jaramogi Oginga Odinga ambao walikuwa viongozi mashuhuri wa kupigania uhuru nchini Kenya, na miongoni mwa viongozi waanzilishi wa Muungano wa Kitaifa wa Kenya (KANU).

Waliomba ushiriki wa Bibi Titi katika makusanyiko ya kisiasa ya uhuru nchini Kenya. Alishiriki katika mikutano ya kisiasa Mombasa, Kisumu, Machakos na Nairobi.
Ujumbe wake ulielekezwa kwa wakoloni (Uingereza) kumwachilia huru Mzee Jomo Kenyatta; ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza wa KANU na baadaye akawa rais wa Kenya, lakini alifungwa jela kwa uhaini.

Sauti yake nchini Kenya ilikuwa na athari chanya na ilisababisha wanaume na wanawake kuungana tena katika kupigania uhuru wao.

Jomo Kenyatta alipoachiliwa miaka ya baadaye, alikuja Tanzania kuzungumza mbele ya Watanzania pale Jangwani, Dar es Salaam.

Alimshukuru Bibi Titi na Watanzania kwa msaada wao. Ilikuwa wakati wa mkutano huo Julius Nyerere aliposema kwamba yuko tayari kuchelewesha uhuru wa Tanzania ili angoje Kenya ipate wa kwao kwa matumaini kwamba ndipo nchi hizo mbili zingeungana.

"Bibi Titi alihamasishwa kuachwa huru kwa Jomo Kenyatta na baadaye kweli aliachiwa.Tunajivunia sana kwa màma huyu ambaye alikuwa msuluhishi kimataifa kwa kazi nzuri alizofanya." amesema Prof.Shani.

Chatanda

Naye Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda amesema kuna umuhimu kwa kuanzisha taasisi ambayo itajihusika na Bibi Titi Mohamed kama ilivyo Kigoda cha Mwalimu Nyerere kwa upande wa wanaume.
Pia ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwa na siku maalum kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Bibi Titi huku akisisitiza kuandikwa kwa kitabu kinachomwelezea kiongozi huyo shupavu, mwanaharakati na mpigania uhuru wa Tanzania.

Mbali na kumpongeza Mheshimiwa Mchengerwa na Halmashauri ya Rufiji kwa kuandaa tamasha hilo, Chatanda amefafanua kwamba, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imefanya kazi kubwa nchini ya kudumisha utamaduni na kuendesha matamasha mbalimbali.
Amesema, kwa kufanya hivyo wizara hiyo inachangia katika historia ya kuwaenzi wapigania Uhuru na kuendeleza masuala ya maendeleo hasa ya wanawake.

"Ndiyo maana naipongeza wizara kwa kuandaa tamasha kutukumbusha utamaduni wetu," Chatanda huku akitoa tuzo maalum kwa Mheshimiwa Mchengerwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi nzuri.
Tuzo ya wizara ilipokewa na viongozi wakuu wa wizara hiyo akiwemo. Waziri Mohammed Mchengerwa, Naibu Waziri Pauline Gekul na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi.

Pia, Chatanda amesema, Rais Dkt. Samia ndiyo Bibi Titi Mohamed wa sasa kwa vile, anaishi maono yake, hivyo wataendelea kumuunga mkono kwa hali na mali.
Wakati huo huo, Chatanda amesisitiza kuwa UWT pia inaamini katika kauli mbiu ya tamasha inayosema "Mwanamke ni jeshi imara katika kuleta mabadiliko, tumuenzi".

Mwananchi

Miongoni mwa wananchi na mkazi wa Ikwiriri Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Said Khamis amesema kuwa, ni jambo la heri kuona Bibi Titi Mohamed anaenziwa katika ardhi ya Rufiji.

Ikumbukwe, baada ya Uhuru, Bibi Titi alikua Mbunge anayewakilisha Rufiji na Naibu Waziri katika Wizara ya Tamaduni na Maendeleo.

Pia alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Umoja wa Wanawake Tanzania, miongoni mwa viongozi wa kwanza wa Jumuiya ya Ustawi wa Waislamu wa Afrika Mashariki na mjumbe wa kamati iliyokuwa ikitayarisha Siku ya Maulid kila mwaka.
"Awali ya yote nimpongeze kijana wetu ndugu, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Mbunge na Waziri ambaye kwa kushirikiana na Halmashauri yetu ya Rufiji wamefanikisha jambo hili muhimu. Huku Rufiji kuna historia kubwa juu ya Taifa letu, ninaamini hatua hii ni njema katika kuendea hatua nyingine ya kuwaenzi viongozi wetu wengi ambao walilisaidia na hata kufanya mambo makubwa ndani na nje,"amefafanua Khamis.

Kate

Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Bi.Kate Kamba amesema kuwa, Bibi Titi Mohamed ataendelea kukumbukwa na kuenziwa kutokana na namna ambavyo alikuwa hodari na shupavu katika kulipigania Taifa enzi za ukoloni.
"...Wazungu wakoloni hawakutaka kabisa, kwa hiyo walitubana na kuna mikoa kabisa hawakutaka kuwa na elimu kama Kigoma ili wao tuwafanyishe kazi.Wao hawakuthamini elimu na elimu waliyokuwa wanatupa ilikuwa haitusaidii sisi kubadilika katika maisha yetu.

"Na mpaka sasa hivi elimu tuliyonayo ni tofauti na Wajerumani, Wachina walitupa sisi ya kufanyia kazi za ukarani hawakutaka...tulipopata Uhuru cha kwanza tukikuwa na matatizo makubwa matatu. Ujinga, maradhi na umaskini na akichokifanya Baba wa Taifa baada ya Uhuru shule zote zikataifishwa za misheni ili kila mtu asome.

"Kwa sasa hivi tunaona Mama Samia jinsia anavyosisitiza elimu, ameweza kutumia mbinu na ujanja wake wote hadi zile fedha za COVID-19 ambazo si rahisi World Bank kukupa hela na utumie unavyotaka yeye ametumia mbinu na kufanikiwa kuzipeleka kwenye elimu.
"Amethubutu na amefanikiwa, kwa hiyo sasa hivi watoto wetu wote watasoma haya ni mambo ambayo yanatija kwa Taifa letu. Hii inatuonesha jinsi ambavyo wanawake wanaweza kwa dhati, haikuwa rahisi angalia huko tulikotoka hapakuwa na katibu mwanamke ndani ya chama, kwa hiyo Rais wetu anatuonesha uwezo wa wanawake ni mkubwa."

"Rais anaangalia mengi fikiria alivyoweza kufufua utalii,hakika mama Huyu Bibi Titi angefufuka leo akaona jinsi wanawake wanavyoongoza ndege wanavyochapa kazi, meli, madaktari angeona raha kabisa wanawake kuweza mambo mengi mazuri kwa nchi yetu,"amesema Bi.Kamba.

Prof.Mutembei

Kwa upande wake, Prof.Aldin Kai Mutembei kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema kuwa, "Nilipomsoma kwa dhati Bibi Titi nikajua anatufundisha jambo moja kubwa, sana sio lazima uwe msomi mkubwa sana uweze kutenda jambo.
"Elimu ni zana pana, huyu (Bibi Titi) alikuwa na elimu zaidi hata zaidi ya maprofesa kwa sababu mambo aliyoyatenda yalikuwa makubwa sana, alikuwa mwanaharakati, mwanasiasa na pia msanii.

"Wimbo ambao ulikuwa ukiimbwa mara kwa mara kuna tafsiri mbalimbali sana nilikuwa najiukiza kwa nini alizaliwa sehemu ya juu hapa Rufiji.
"Nataka nisisitize kwa wanafunzi lazima tujifunze kuwa na lugha fasaha, Bibi Titi alikuwa na mchango mkubwa sana katika kukuza lugha ya Kiswahili, moja kati ya sifa aliyokuwa nayo ni kuongea lugha fasaha.

"Mwalimu Nyerere amesifiwa sana katika hotuba yake, lakini ukweli ni kwamba alijifunza unubi kutoka kwa Bibi Titi Mohamed na ndio maana Mwalimu Nyerere akakubalika miongoni mwa Waislamu miongoni mwa Waswahili kwa sababu aliweza kutumia mbinu za Kiswahili na unubi wa Kiswahili.

"Alijifunza kutoka kwa Bibi Titi Mohamed, alikuwa na ushawishi mkubwa sana, si tu alikuwa jasiri nakumbumbuka miaka ya 60 watu walikuwa wanaenzi sana lugha ya Kiingereza ikawa hata vigumu kuzungumza Kiswahili bungeni kwa ujasiri wa Mwalimu Nyerere alizungumza Kiswahili bungeni kwa mara ya kwanza kutoka kwa Bibi Titi Mohamed.

"Na ukisoma katika kumbukumbu za Bunge utaona yeye (Bibi Titi) hakusita sita akiwa na mawazo yake aliongea Kiswahili na akasisitiza lazima tuendelee kuongea Kiswahili bungeni,"amefafanua Prof.Mutembei katika kongamano hilo ka kumbukumbu ya Bibi Titi Mohamed wilayani Rufiji.
Wakati huo huo, Prof.Mutembei amefafanua kuwa, "Lakini pia Mwalimu Nyerere kila alipokwenda kuhutubia ukitazama kwenye magazeti mwalimu alipokuwa Bibi Titi nyuma yake kabla Mwalimu hajaongea Bibi Titi njoo anaimba wimbo mmoja wa kuwavutia watu, kama mtu anayesafisha njia katika vitabu vya misaafu alikuwa ni Yohana Mbatizaji.

"Akizungumza Mwalimu anakuja kuhutubia, kwa vijana tunajifunza nini kutoka kwa Bibi Titi hapa tunajifunza alikuwa jasiri sisi tutakuwa jasiri kwa namna gani ili tumuenzi? Pia alikuwa na matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.

"Naomba tuendelee kumuenzi Bibi Titi Mohamed kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha kaka, dada na watu wote. Jambo la tatu alikuwa na uhuru wa fikra. Jambo la nne alisimamia kile alichokiamini, alijisimamia mwenyewe na pia kile alichokisimamia katika jamii.

"Na mwisho, alitetea umma wa wanyonge ambao sauti yao haisikiki miongoni mwa wanajamii na ndio maana Mwalimu Nyerere alimuweka katika nafasi mbalimbali ikiwemo Waziri wa Mambo ya Jinsia na mambo mengi alifanya kwa ajili ya Watanzania.

"Ukiangalia kwa umakini mkubwa Bibi Titi Mohamed alitumia lugha ya mficho kuwaficha wengi. Kumbuka hizi nyimbo za miaka mingi ziliimbwa, lakini zilifumbwa kwa ajili ya werevu kufumbua, alifumba Waingereza na aliziimba kwa misemo, methali nahau ambayo inaficha mambo.Bibi Titi alitumia sanaa yake kujenga na kuhakikisha nyimbo zake zinachangia Uhuru wetu,"amefafanua Prof.Mutembei.

Shibuda

Naye mwanasiasa mkongwe nchini, John Magale Shibuda amebainisha kuwa, "Chama Cha Mapinduzi mnadeni kubwa sana, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo Bibi Titi Mohamed alikuwa hodari katika kusimamia mambo mazuri ambayo yalikuwa na faida.
"Alikuwa ni Mama ambaye alitimiza wajibu wake kikamilifu na pia ingefaa kwa vyama vyote vya siasa kumpongeza na kumuenzi mama huyu, kwani alisaidia kwa kiwango kikubwa kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika.

"Mimi,niwaambie jambo moja wanasema kuishi kwingi kuona mengi, Waislamu huwa wanakaa na Wakristo huwa wanakaa hivi, mfumo wa vyama vingi tunakutana lini kwa ajili ya kumuenzi Bibi Titi?.
"Hii ni kwa faida ya uzao wa sasa na kizazi cha kesho. Nakuombeni CCM, mnadeni kubwa sana la kumuenzi mwasisi huyu. Naombeni kuwaambieni jambo moja wana CCM, wenzangu tunahitaji kumuenzi na kumpa heshima yote mama huyu.

"Kwa Nini nayasema haya? Kizazi hiki kisipoambiwa haya hakitaweza kuyajua na kuyatambua leo tunaye hapa Bibi Kate Kamba hajaandika kitabu, Mzee Malecela tunapoteza kumbukumbu na pia niwaombe wajumbe wa kamati kuu tunasikitika kuona watu wanachoma kumbukumbu na nyaraka za zamani kuwa zimechakaa.

"Naombeni kuwe na kitengo cha kuweza kuhifadhi na kutunza hizo kumbukumbu za zamani na nyaraka muhimu Mheshimiwa Mchengerwa nakupongeza kwa hatua hii muhimu na kuziishi siasa za ukombozi za waasisi wa taifa hili kwa moyo wa dhati,Wana Rufiji nawaomba msije mkaizamisha meli hii, mtoto huyu (Mohamed Mchengerwa) ni hazina ni fahari ya Bibi Titi hatupendi kusifia mema ya watu, lakini mbona ya akikosea watu husema?.

"Historia ya Bibi Titi Mohamed naomba ipelekwe na Mkoa wa Mwanza na mikoa mingine kwa upana wake, watu wazidi kumtambua kuthamini mchango wa mama huyu shupavu na shujaa, UWT naombeni mzidi kulibeba jambo hili muhimu.
"Bibi Titi alikuwa si mtu wa kelele, alikuwa ni mhimili wa siasa safi. Alikuwa akija usukumani na kuwatania wasukuma kwamba amkeni tusonge mbele.

"Alihamasisha umoja na kujenga morali kwa kuwatia moyo wananchi pale ambapo walitetereka yeye kama Mama hakurudi nyuma kutia hamasa na kutia moyo.

"Ni talanta ambayo alijaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya faida kwa wengine na ndio maana leo hii tunamuenzi na kumkumbuka mchango wake,"amefafanua Shibuda.
 
Tamasha hilo ni la siku mbili kwa maana ya Desemba 14 hadi 15, 2022 lilianza kwa dua maalum ya kumuombea Bibi Titi Mohamed ambapo leo asubuhi limeendelea kwa kongamano maalum na baadaye burudani iliyowakutanisha maelfu ya wananchi.

Aidha, limeratibiwa na Ofisi ya Mbungewa Rufiji chini ya Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ambaye pia ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Mheshimiwa Mchengerwa

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amesema,utamaduni wa kuendelea kuwaenzi waasisi wa Taifa ni miongoni mwa siri ya kipekee inayosaidia kuharakisha maendeleo katika nyanya mbalimbali.
Pia Mheshimiwa Mchengerwa amesema kuwa, huko awali kulikuwa na tatizo kidogo la kutokumbuka kazi kubwa na kazi nzuri ambazo zilifanywa na waasisi wa Taifa letu.

"Wapo watu wengi walifanya kazi kubwa na kazi nzuri, ambao kwa bahati mbaya hatukuwa na desturi nzuri ya kuandika historia zao,hata kuwakumbuka na ikumbukwe kuwa hakuna Taifa lolote ambalo linaweza kupiga hatua kama litasahau kazi kubwa na nzuri zilizofanywa na wale waliotutangulia.

"Na hili linatukumbusha kwamba ili uweze kupiga hatua nzuri hata kimaendeleo lazima ujifunze yale yaliyofanywa na waasisi wa Taifa hili pale ambapo walitoa elimu na maelekezo ni kuangalia uweze kujirekebisha, kujifunza na uweze kupiga hatua kwenda mbele.

"Leo ni siku muhimu tunamkumbuka Bibi Titi Mohamed na ikumbukwe tu kwamba harakati za kumkumbuka Bibi Titi Mohamed zilianza na Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshmiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, yeye ndiye aliona umuhimu na mchango mkubwa uliofanywa na Bibi Titi Mohamed na sisi wananchi wa Mkoa wa Pwani hatukuwa na ajizi, tukasema kwamba tumkumbuke Bibi Titi Mohamed,"amefafanua Mheshimiwa Mchengerwa.
Amefafanua kuwa, mwaka jana walifanya sherehe kubwa katika Mkoa wa Pwani katika Wilaya ya Rufiji ambapo ndipo uzazi wa Bibi Titi Mohamed ulipo.

"Ni hapa Rufji. Yeye (Bibi Titi) alikuwa Mbunge wetu wa kwanza katika Mkoa wa Pwani, lakini mbunge wa kwanza katika wilaya hii ya Rufiji.

"Leo tuna mengi ya kujifunza ukiisoma historia ya Bibi Titi Mohamed, ukiadithiwa historia ya Bibi Titi Mohamed utajua alikuwa mtu wa aina gani, alikuwa mtu mzalendo kila Mtanzania analo jambo la kujifunza sio wanawake tu hata sisi vijana wa kiume, alikuwa shupavu, jasiri, mtu aliyetamani kuona kila mtu yuko huru.

"Inawezekana kabisa mafanikio ya nchi yetu leo yanatokana na kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa taifa letu akiwemo Bibi Titi Mohamed ambaye alikuwa mstari wa mbele bega kwa bega na Mwalimu Nyerere.
"Alikuwa kiongozi wa kwanza mwanamke hapa Tanzania, lakini kule nchini Kenya wakati wa kudai Uhuru kule alikuweko akihamasisha wanawake amekwenda mpaka Zanzibar akihamasisha akiwataka viongozi kwamba hawawezi kufanikiwa iwapo wanawake watabaki nyuma.

"Akasema wanawake watoke majumbani waende wakafanye siasa kwa sababu ya ushawishi walionao, ukweli wao na nguvu walionayo katika jamii.
"Sisi vijana tunajivunia sana, sisi ambao tulipata bahati ya kumuona Bibi Titi Mohamed, sisi ambao tumeweza kusoma na kujionea historia namna ambavyo harakati za ukombozi, namna ambavyo alikuwa mzalendo, mkweli akiamini analoliamini akimhamasisha kila mmoja wetu kudai Uhuru akimtaka kila Mtanzania kipindi kile Tanzania Bara ajiunge na TANU ili kwenda kudai Uhuru.

"Kwa hiyo yapo mambo mengi ya kujitoa mhanga kwa ajili ya taifa lake na mengine mengi kwa ajili ya maendeleo Bibi Titi aliyahamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili wakati ule wa miaka ya 60, kipindi kile Bibi Titi bungeni akiwa anadai wakazi wa eneo fulani waweze kupatiwa taa za barabarani lipo neno alilolisema ambalo Mwalimu Nyerere akiwa Waziri Mkuu alihakikisha anahamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili.

"Lipo neno alilitumia ambalo lilihamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani ya Bunge haya yote na mengine mengi tukisema tuyaeleze tutakesha,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Mchengerwa.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mchengerwa amefafanua kuwa, "Haya yote yalifanywa na Bibi Titi Mohamed na sisi tunatamani kwamba mchango wa waasisi hao mchango wa mwanamke ulikuwa mkubwa ukimuacha Bibi Titi Mohamed wapo wanawake wengine wengi katika orodha tutawasikia kesho hawa mchango wao hautambuliwi, wanatambuliwa tu baadhi ya wanaume, hawa wanawake walifanya kazi kubwa sana.

"Wako wengi hawatambuliwi, na wengine historia zao hazijaandikwa tunayo kazi kubwa sana kila mmoja wao historia zao ziandikwe ziweze kutunzwa vizazi na vizazi miaka 200, miaka 300, miaka 500 tusipoyafanya haya leo vizazi vyetu havitajua kwamba tulipokwenda kupigania uhuru mambo gani yalifanyika, ushawishi gani tuliufanya nani alikiwa mstari wa mbele.
"Wako wengi ambao walifanya makubwa, lakini pasipo kuandikwa historia zao zitapotea kuna umuhimu mkubwa sana kuandika historia yao kuwa na siku yao kuwakumbuka na sisi tumeshaamua tutakuwa na siku maalum kumkumbuka Bibi Titi Mohamed na tumekubaliana na wenzetu ndani ya chama...

"Tunakumbuka uzalendo na ujasiri kutoka kwake kutokana na msingi thabiti yeye na viongozi wengine walituachia, Bibi Titi alikuwa Mbunge wa kwanza hapa kwa hiyo ametufunza mengi ule ujasiri wake wa kujenga hoja, kutenda haki na kuharakisha maendeleo leo tuna barabara ya Kilwa Road, barabara hii ilijengwa kwa kumuenzi Bibi Titi Mohamed.
"Leo ina lami, Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Mwinyi alijenga hii kumuenzi, leo pia Kuna mitaa mingi Dar es salaam na sisi tumekubaliana kwamba pamoja na kuwa na siku maalum tunakwenda kuandika haya yote ambayo tumeyazungumza kwa maneno, lakini hayajaandikwa yako mengi sana,"amebainisha Waziri Mchengerwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news