TUNGEMSHITAKI KWA KADINALI RUGAMBWA:Hoja ikawa inakuwaje Padri mwenye nadhiri ya useja aishi na mama wa Kichaga mtaani?

NA ADELADIUS MAKWEGA

JAMANI eee ! tunapokaa na watoto wa watu tunapaswa kukaa nao vizuri sana iwe shuleni, kwenye siasa na hata katika masuala ya imani.

Kwa hakika hawa watoto wetu wana changamoto nyingi na madhaifu mengi kadhaa wa kadhaa ambapo wakubwa wanapaswa kuhakikisha pale hawa watoto wanapokosea wanalo jukumu kubwa la kuwarudisha katika njia iliyo sahihi ili kesho waje kuwa watu wema kwa jamii yao.

Jambo la muhimu zaidi hawa wanaonekana leo ni watoto au vijana hapo baadaye wanaweza kuwa mashahidi wa wema au ubaya wa wale wakubwa waliowalea katika utoto.

Mwanakwetu unaweza kujiuliza kwa nini ninayasema haya leo hii? Mwaka 1987 tulikuwa vijana wadogo sana na wakati wa likizo tulipenda sana kucheza mechi za mtoano za mchezo wa soka kwa kutumia mipira ya makaratasi kulingana na maeneo tuliyokuwa tunatokea.

Nakumbuka kuna siku tulicheza mechi hiyo ya mtoano pale Mbagala Msalabani (Misheni) tulipokuwa tunakutana watoto wengi tuliokuwa tukisoma mafundisho ya dini.

Watoto tuliokuwapo ni wale wanaotokea Mtoni Kijichi, Mbagala Kizuiani, Mbagala Kizinga na Mtoni Mtongani.

Hapa Mbagala Msalabani palikwa na Kanisa dogo na makazi ya Padri mmoja wa Kiitaliano ambaye alikuwa Padri mwema sana, nakumbuka watoto waliokuwa na vidonda au wale walioumia katika michezo hapo kanisani Padri huyu aliwafunga vidonda bure bila malipo yoyote yale utadhani alikuwa muuguzi.

Mazingira haya yalikuwa na miti mingi ya matunda kama vile mapera, miembe. mikorosho, minazi, mapapai na hata migomba, kwa hiyo watoto wote tuliangua matunda hayo na huku tukicheza kwa pamoja bila ya kujali dini zetu.

Mazingira haya ya eneo la kanisa hili yalivutia mno na ndiyo maana watoto wengi tulitamani kucheza hapo ikiwa kama bustani ya Edeni, hakukuwa na ukuta wala geti kuzunguka eneo hilo ambapo watoto walipotaka kucheza waliingia tu na kucheza bila kukatazwa na ndiyo maana wale tuliosoma mafundisho na watoto wa jirani na kanisa hilo walicheza pamoja.

Kwa miaka mingi sijajaliwa kuyaona mazingira yenye mandhari zuri kama yale labda kidogo pale Ndanda Misheni.

Siku hiyo mechi ilichezwa na ya kwanza ilikuwa baina ya Mtoni Mtongani na Mtoni Kijichi, wenyeji walikuwa ni Mtoni Kijichi mechi ilichezwa vizuri na Mtoni Mtongani walifungwa mabao 7-2 na mechi ya pili ilikuwa ya Mbagala Kizinga na Mbagala Kizuiani mechi ilikuwa kali mno maana Mbagala Kizinga ilikusanya watoto wa Mangaya, Sabasaba, Mpili na Machinjioni.

Nao Mbagala Kizuiani ilikusanya watoto wa Shimo la Mchanga, Moringe na Kibonde Maji kwa hiyo lilikuwa kundi la watoto wengi. Katika mechi hiyo ya pili Mbagala Kizinga ilishinda kwa mabao 3-2.

Kumbuka mechi hizo ni za mtoano tukapumzika watoto wakavamia mapera ya kanisani wengine wakanywa maji ya bomba kando na kanisa dogo na mechi zikaendelea.

Sasa ilichezwa mechi baina ya Mtoni Mtongani na Mbagala Kizuiani kutafuta mshindi wa tatu na Mtoni Mtongani ilishinda kwa mabao 4-0 na ukawadia wakati wa kucheza fainali kati ya Mbagala Kizinga na Mtoni Kijichi.

Timu hii ya watoto wa Mtoni Kijichi ilikusanya watoto wa Mbagala Misheni, Mwanamtoti, Mikwemeni na Mbagala Kubwa (Kuu).

Mechi ilicheza vizuri sana na watoto wa Mtoni Kijichi yenye Mbagala Misheni waliwafunga bao la kwanza watoto wa Mbagala Kizinga.

Tambua kuwa hawa watoto wa Mtoni Kijichi mechi hii ilikuwa inachezwa kwao kwani ndipo lilipokuwa kanisa hilo.

Mbagala Kizinga wakafungwa bao la pili na mchezaji maarufu wa Mtoni Kijichi aliyefunga pia bao la kwanza aliyefahamika kama Mteule. Shamshamra hizo ziliwatoa majumbani watoto wengi waliokuwa likizo na kufika jirani na uwanja huu kutazama mechi hiyo.

Katika mechi hiyo mwanakwetu nipo, lakini sikuwa mchezaji maana mpira wa miguu nilikuwa siuwezi kwa madai kuwa mwanakwetu nikicheza ninapiga madochi, wale wote wanaopiga madochi hawakupata namba kama mimi.

Ndugu zangu wa Mbagala Kizinga uzalendo ukawashinda wakaanzisha vurugu uwanjani, wakampiga Mteule. Kwa kuwa Mteule alikuwa anaishi jirani na kanisa hilo ndugu zake hawakukubali ikatokea vurugu uwanjani.

Kwa kuwa vurugu hiyo inatokea katika mazingira ya kanisa Padri akatoka katika makazi yake akatuambia tuliokuwapo hapo, “Vatoto msifanye vurugu shambani mwa bwana.” Padri Muitaliano, Padri Mkarimu alisema hayo.

Watoto wakamjibu vibaya huyu Padri wa Kiitaliano ambaye alikuwa akipenda sana maendeleo ya watu wa Mbagala.

Maneno yale yaliyosemwa dhidi ya Padri hayakusikika kwake, lakini uwanjani yalisikika na kila mmoja wetu. Tuliyokuwa tunafahamika majina yetu Padri akaagiza tusicheze tena na turudi nyumbani.

Mechi ya fainali ya mtoano ikaishia hapo lakini watoto wana hasira wengine kwanini Padri wetu aambiwe vile? Wengine wakasema labda linalosemewa ni la kweli.

Wengine wana hasira kuwa mechi ingendelea waliofungwa wangerudisha mabao yale mawili.

Watoto wanaotokea Mbagala Kizinga wanasoma mafundisho Kanisani wamekasirika mara mbili kufungwa mabao mawili na Mteule huyo huyo aliyetufunga katamka maneno mabaya.

Mwenye siri ni Mteule ambaye alifunga mabao hayo mawili ya fainali ya mtoano na ndiye aliyetamka, lakini hakuwa muumini wa kanisani hapo. Hapo sasa kila mmoja anarudi nyumbani kwake wengine wamevimba nyuso zao na wengine macho yao yamevilia damu kwa sababu ugomvi.

Mtoto mmoja Msomali Mkristo ambaye jicho lake lilivilia damu alipofika kwao alibanwa akasimulia kilichotokea na akiyataja majina ya watoto kadhaa akiwamo Mteule na maneno aliyoyasema katika ugomvi huo.

Katika vurugu hiyo pia kijana mmoja wa Kigoa nayeye aliumia, mwanakwetu alitajwa jina lake kwani ndiye aliyeuchukua mpira huo baada ya Padri kusema watoto waache vurugu hizo na warudi nyumbani.

Wazazi walikaa pamoja na kujiuliza lililotokea na kumshirikisha Katekista Kidiwa (alikuwa na tabia ya kuyasaga meno huku akitembea). Mazungumzo yalipofanywa wazazi na Katekista kukubaliana kuwa huo ni ugomvi wa watoto, lakini mbona maneno yaliyotamkwa dhidi ya Padri yalikuwa maneno ya kikubwa?.

Huo ulikuwa sehemu ya ugomvi wa watoto, lakini kwa nini wamseme vibaya Padri wetu? Je maneno haya yana ukweli? Kama yana ukweli kwa nini Padri huyu asishatakiwe kwa Kadinali Laurean Rugambwa.

Katekista akasema maneno ni mabaya na hata kama mnataka kumfuata Kadinali, tafuteni ukweli kwa siri. Mzee mmoja mshika dini sana, mzee wa Kichaga ambaye alikuwa Inspekta wa UDA akasema kazi hiyo nipeni mimi na hao vijana. Katekista akasema haya, “Jambo hili liwe siri kwa kuwa kumchunguza mtu msafi kwa ubaya inakatisha tamaa.”

Watoto wote waliotajwa majina tukaitwa na wazazi wetu na kiongozi wa kikao hicho alikuwa huyu mzee wa Kichaga wa Mabasi ya UDA.

Uchunguzi ulipofanywa wa mwenendo wa Padri kuwa Mteule huwa anamuona kwa mama mmoja wa Kichaga-Mbagala Misheni. Hoja ikawa inakuwaje Padri mwenye nadhiri ya useja aishi na mama wa Kichaga mtaani?

Baada ya miezi miwili tukaitwa tena wakaambiwa wazazi kuwa jambo hilo halina ukweli wowote kwani Mteule mwenyewe na rafiki yake kijana wa ng'ombe wa mama Kichaga walithibitisha kuwa mwanzoni walihisi hivyo, lakini baadaye waligundua hakukuwa na mahusiano mabaya.

Padri huyu ambaye aliizoea familia hiyo na hadi mtoto mmoja wa familia ya mama huyu akawa mtawa na mazoea hayo ndiyo yaliyoibua maneno haya.

Mwishoni baada ya mazungumzo haya Baba wa Mteule aliomba msamaha kwa viongozi hao kwa maneno hayo ya mwanawe.

Mzee wa Kichaga Inspekta wa UDA akasema tungebaini ukweli kwa hakika tungemshitaki Padri kwa Kadinali. Wakati tunatoka na baba nikamuuliza wanaweza kumshitaki Padri ? Baba akanijibu kuwa Kadinali ndiyo mkubwa waamini na watawa wote.

Mwanakwetu, wazazi, walezi na kila mmoja wetu anawajibu wakuhakikisha watoto wanaendelea kufundishwa tabia njema kwa Jamii wanamoishi kulingana na maadili ya Imani zao na kuthamini Imani ya dini nyingine pamoja na maadili Jamii.

Hatua hii itawasaidia kuwa waumini na wananchi wema ambao wanapenda kumtumikia Mungu na Taifa lao ili nao waje kuwarithisha hayo mema watoto wao na kufanya Tanzania kuendelea kujipambanua kuwa kisiwa cha amani Duniani.

Baada ya tukio hilo tukawa tunamtania Mteule kuwa aje kusali ili awe Mkatukumeni, haikupita muda mrefu ukazungushwa ukuta eneo lote na watoto tukawa tunaingia kusali tu na siyo kucheza tena na mafundisho dini wakaanza kutufundisha masista-makekista Sista Theresia na Sista Getruda kutoka Shirika la Dada Wadogo nao Katekista Mbunda na Kidiwa wakapangiwa majukumu mengine.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news