ULIMWENGU MWALIMU MZURI...Lakini simu yake ataipata siku akihitimu shule

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWAKA 2005 Afisa Elimu Msaidizi Daraja la III, Lilian Mwamanda, mwalimu wa masomo ya Historia na Jiografia alikuwa akifundisha somo la Jiografia kidato nne, akiwa mbele ya wanafunzi wake hapo hapo alibaini kuwa mwanafunzi mmoja wa kike alikuwa na simu ya mkononi akiaandika ujumbe wa mapenzi kwa mtu mwingine.
Mwalimu huyo Mnyakyusa-Mhaya aliichukua simu hiyo na kuendelea kufundisha somo lake hadi mwisho, alipomaliza kufundisha somo hilo mwalimu huyu alimtaka binti huyu kuandika maelezo kwa nini anafanya mawasiliano ya simu akiwa darasani?.

Barua hiyo iliandikwa kisha mwalimu huyo kumueleza mwalimu mwenzake wa zamu siku hiyo ambaye alikuwa ni mwanakwetu juu ya tukio hilo.

Kwa bahati nzuri mwanakwetu alikuwa mwalimu wa zamu siku hiyo pamoja na mwalimu Mwamanda wakawasiliana na mwalimu wa nidhamu, Leonadi Gange na yeye kukubaliana nao kuwa simu hiyo ikahifadhiwe kwa Mkuu wa Shule na binti huyo atakabidhiwa siku atakapomaliza shule Novemba 2005. 

Walimu kadhaa walikiri kuona simu hiyo kwa binti huyo siku za nyuma kwa hiyo maamuzi ya kuhifadhiwa yalionekana kuwa ni sahihi kwa walimu wote.

Saa nane wanafunzi walirudi majumbani mwao, baada ya muda mama wa binti huyo ambaye alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Isimani alifika shuleni hapo kuuliza kwa nini bintiye amepokonywa simu yake?.

Kwa bahati nzuri Mkuu wa Shule hii alieleza kilichotokea katika tukio hilo na maamuzi ya simu hiyo atapatiwa mara baada ya kuhitimu shule hiyo. 

Mama wa binti huyo alikuwa mkali mno kwa kuwa bintiye huyu alimpenda sana huku wengine wakisema kuwa alikuwa mtoto pekee wa mwalimu huyu, yeye alikuwa kifungua na kitinda mimba wake.

Mwanakwetu, Mwalimu Mwamanda na mwalimu wa Nidhamu Gange waliitwa kwa Mkuu wa Shule kumsikiliza mzazi huyo, walizungumza mengi huku mwalimu Mwamanda akasema maneno haya, “Mama mimi ni binti kama mwanao, binti unapokuwa na simu unapatikana kwa urahisi mno kwa mambo yoyote yale yawe mazuri au yawe mabaya. 

"Hivyo ukiwa na simu lazima uwe na uwezo wa kuvishinda vishawishi vibaya kwa kuwa ukitafutwa unapatikana, bintiyo bado mdogo kukabiliana na hilo.”

Mama huyu alisema mengi kuwa walimu hao walikuwa wakimuonea gere bintiye kumiliki simu ambapo wakati huo eneo hilo la Isimani mkoani Iringa palikuwa na mti mmoja mkubwa barabarani ambapo mtandao ulikuwa ukipatikana tu na maeneo machache machache kwenye vichuguu kwa kuutafuta mno.

“…Kama nataka simu si bora ninunue dukani, ogopa pasua kichwa, ogopa za mitaani. Yaani hatua tatu, netiweki haisomi, hata ukiwa nyuma, aliyeuza haumuoni…”

Hali hiyo ilifanana fika na aliyokuwa akisema Solo Thang na wenzake Joy Moe na Sogg Dogy katika wimbo wa Simu Yangu ambapo ulikuwa ukitamba mno wakati huo.

Kumbuka wapo ofisini kwa Mkuu wa Shule, mwalimu wa nidhamu alimueleza mzazi huyo kuwa bintiye ana mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi mwezake ambaye ndiye aliyemsaidia kununua simu hiyo. 

Kwa uchunguzi wa mwalimu wa nidhamu mvulana huyu alikiri kununua simu hiyo. Mzazi wa binti huyo hakusadiki maneno haya japokuwa alioneshwa barua za maelezo zilizoandikwa na bintiye na mvulana huyo waliokuwa wanasoma kidato cha nne pamoja. 

Mwalimu Mwamanda alisema kwa huzuni mno, huku machozi yakimtoka dhidi ya maneno hayo ya mzazi huyo,

“Mwalimu mwenzetu kama sisi tunamuonea gere binti yako kuwa na simu, sisi tunamshitakia Mungu jambo hilo, lakini simu yake ataipata siku akihitimu shule.”

Kikao hicho kilimalizika na mama huyu hakukabidhiwa simu, walimu hawa wa zamu wakachukua kitabu kinachofahamika kama Log Book ambapo kila jioni walimu wa zamu wanaandika taarifa ya shule ya siku hiyo, kwa hiyo hata hii kesi ya simu ikawa miongoni mwa matukio makubwa ya siku yaliyonukuliwa nakuweka sahihi zao.

Maisha yaliendelea na binti huyu alifanya mtihani kwa kidato cha nne na alipomaliza alitakiwa kujaza fomu ya kukabidhi mali za shule, alipomaliza alipewa simu yake na kuondoka zake kwa amani. 

Kwa bahati nzuri binti huyu na yule mvulana walifaulu kidato cha tano shule tafauti na kuhitimu kidato cha sita mwaka mmoja, mvulana alijiunga na Chuo Kikuu na binti huyu kujiunga na Chuo cha Ualimu kwa mafunzo ya stashahada ya ualimu.

Maisha yanaendelea, Januari 2016 mwanakwetu alikwenda Kariakoo katika benki mojawapo hapo alikutana na dada mmoja mwanasheria aliyesoma naye Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Nanza Mmbuji, yeye alikuwa akifanya kazi na benki hiyo ya Kitanzania. 

Nanza Mmbuji dada mmoja mkarimu sana, mpole sana, mwema sana, mnyenyekevu sana kwa wateja wake alipomuona mwanakwetu na mkewe alizungumza nao na kuwasaidia kupata huduma kwa dakika chache mno ambapo hadi leo hii mwanakwetu hajawahi kuhudumiwa kwa haraka mno kama siku hiyo, rekodi ya Nanza haijawahi kuvunjwa tena. 

Mwanakwetu alipokuwa akitoka katika benki hiyo nje alikutana na binti yule mwanafunzi wake wa Isimani wakati huo na yeye akitoka katika benki hiyo kuhudumiwa. Mwalimu shikamoo ! Mwanakawetu alihitikia marahaba, za siku?.

“Za siku ni nzuri tu, siku hizi mimi ni mwalimu wa Halimashauri ya Lushoto.” Walibadilishana namba mwalimu na mwanafunzi wake na kila mmoja kuondoka zake. Miezi saba baadaye mwanakwetu alikuwa mwajiri wa binti huyu katika Halimashauri hiyo, lakini wakati huo binti huyu alikuwa akihama kutoka Halimashauri hiyo na kwenda halimashauri nyingine.

Binti huyu alizungumza na mwanakwetu mengi hapo Lushoto akisema kuwa yule kijana aliyekuwa rafiki yake shuleni alizaa nae mtoto mmoja na alipomaliza Chuo Kikuu kijana huyu alioa binti mwingine na yeye kuachana naye kabisa.

Huku akikumbuka tukio lile na mwalimu Lilian Mwamanda la kumkamata na simu darasani akiwa kidato cha nne. 

Akiyakumbuka mengi akisema bayana kuwa hata sasa yeye ni mwalimu anayaona kwa macho yake na anayasema hayo hayo kwa wanafunzi wake, lakini kumuelewa inakuwa ngumu sana kwao, anawaambia kuwa ulimwengu ndiye mwalimu mzuri.

0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news