UPIMAJI WA LOLOTE KWA HAKI

NA ADELADIUS MAKWEGA

KUNA wakati Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ilisisitiza mno ujenzi wa vituo vya afya katika kata mbalimbali nchini Tanzania, huku baadhi ya wilaya zilipata bahati ya kupatiwa mamilioni ya fedha za ujenzi wa vituo vya afya kati 3-5 na vituo hivyo kupunguza umbali wa kufuata huduma za afya ikiwamo kuhifadhi maiti katika hospitali za wilaya.

Miongoni mwa wilaya zilizonufaika sana na hilo ni Mbozi katika Mkoa wa Songwe mpaka mwaka 2019 walikuwa na vituo vya afya vitano, vitatu vipya kwa pesa ya serikali na vituo vya afya viwili vilijengwa na taasisi za dini kimoja kukabidhiwa kwa serikali (Kituo cha Afya Nanyara) na kimoja kikimilikiwa na taasisi ya dini (Mbozi Misheni).

Katika ujenzi wa vituo hivyo vya afya vitatu kila kimoja kikipata shilingi milioni 400 na huo ujenzi ulisimamiwa kwa karibu na watumishi wa umma na wananchi katika maeneo mbalimbali.

Wakati huo Mbozi Mganga Mkuu wa Wilaya alifahamika kama Dkt.Abdul Mshana. Kila kituo kilichokuwa kinajengwa kilikuwa na kamati mbalimbali za wananchi wa maeneo hayo. Mwanakwetu alipotembelea maeneo hayo alisimuliwa mengi sana na wanavijiji hao juu ya watumishi waliokuwa wanafanya kazi na wanakijiji hao nyakati zote tangu kuanza ujenzi hadi kukamilika.

Ujenzi huo uliongeza ujirani baina ya wananchi na viongozi wao, huku wakubwa wengi walifika kukagua shughuli za mradi huo unavyoendelea.

Siku moja mwanakwetu alitembelea Kituo cha Afya cha Isansa hapa alioneshwa kitu cha zaidi na wananchi wa eneo hilo ambao walikuwa wakulima wa mahindi, maharage na kahawa kwa kiwango cha juu mno.

“Hii ni nyumba ya mtumishi iliharibika kwa athari za moto, lakini hapa kando ndiyo tunapikia chakula chetu kila siku tunapokuwa na kazi ya usimamizi wa ujenzi wetu kulingana na kamati zetu na kila mwanakamati akichangia kiasi cha fedha hizo kwa chakula.”

Mwanakwetu alivutiwa sana na kamati hii ya Isansa na yeye kuchangia unga na ukapikwa ugali siku hiyo na kula nao. Wakati anakula ugali na kamati hiyo ya Isansa walimuuliza Dkt.Abdul Mshana Mganga, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi yupo wapi? Dkt Mshana amepata barua ya kupangiwa majukumu mengine huko Kilimanjaro.

“Mbona tunasikia kuwa ameshushwa cheo na kwenda kuwa daktari wa kawaida ? Kwani huyu kijana wa Kipare amefanya nini?” Mwanakwetu hakufahamu kilichotokea, lakini akitoa ahadi kulifuatilia hilo na kuliuliza kwa kina.

“Yule kijana hana maneno mengi, tulishirikiana naye sana, alikuwa analala katika chumba cha madaktari hapa hapa katika kituo cha afya, akija mama mjamzito anamsaidia hadi anajifungua salama, jambo hilo lilitutia moyo kuweza kushiriki kwa karibu ujenzi huu, sasa nyinyi mmemuondoa Mungu anawaoneni.”

Mwanakwetu alijibu kuwa atakuja Mganga mwingine wa Wilaya, mjumbe mmoja akajibu akisema, “Sawa kuja atakuja mganga mwingine, lakini kuweza kutuhudumia kama Dkt.Abdul Mshana, kulala hapa hapa! Kula nasi! Hilo ni ndoto.”

Kwa kuwa ujenzi huo ulikuwa unafanyika kwa muda maalumu, Dkt.Abdul Mshana na wenzake kadhaa akiwamo Togolai Gembe (Afisa Afya) walijitahidi mno kuifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa na hata mara nyingi kuviacha vitanda vyao Vwawa na Mlowo-Mbozi na kuhamishia makazi yao kwenye kuhakikisha mradi huu unakamilika.

Mwanakwetu alikula ugali huo wa mapishi ya Kinyia, lakini matonge ya ugali huo hayakupita vizuri kooni mwake kwa maana wenye nchi walilalamikia kuondolewa Mganga wao wa Wilaya Dkt.Abdul Mshana.

Kuuliza huko kulikuwa kama utani, lakini mishale ya ukweli ilimuingia moyoni mwake. Je kipi kilitokea kwa Daktari huyu? Alipouliza kwa wenzake wote Halimashauri hakuna aliyefahamu hilo,

“Ukimuona mwezako wamethubutu kumpigwa ngumi usoni, tambua kuwa mpigaji anaweza kukutwanga ngumi na wewe kwa namna ile ile, kwa hiyo ni vizuri kwanza kujua sababu na pili ukweli wa sababu hiyo.” Kumbuka hii ni kanuni ya maisha.

Mwanakwetu kwa kuwa alipokea nakala ya barua ya maamuzi ya Dkt.Mshana aliamua kufunga safari kwa aliyeiandika barua hiyo, Dkt.Zainab Chaula ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayesimamia Afya wakati huo na kwa kuwa haya ni maamuzi ya mambo ya watu (umma) mwanakwetu aliamini kuwa, Dkt.Chaula atakuwa na majibu tu.

Mwanakwetu alifika Dodoma kuonana na Naibu Katibu TAMISEMI pale Mkapa House, hapo alijulishwa kuwa ofisi yake ipo katika ghorofa moja mbele, kwa hiyo alifunga safari hadi huko ambapo vongozi kadhaa wa TAMISEMI wanaosimamia afya walikuwapo.

Hapa alipanda ngazi za ghorofa hilo na kufika ofisini na kwa bahati ndani ya chumba hicho alikuwapo mtu mmoja akizungumza naye.

Alipotoka mtu huyu, mwanakawetu alibaini sura ya aliyekuwa anaongea na Dkt.Zainab Chaula alikuwa anamfahamu. Ndugu anaitwa Godfrey Richardi ambaye alisoma na mwanakwetu Shahada ya Sanaa ya Habari Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa mwaka 2005 miaka 14 nyuma wakati huo.

Godfrey umetoka kufanya nini kwa Naibu Katibu Mkuu wetu? Mwanakwetu alimuuliza, ndugu huyu alicheka sana akasema na wewe mwanakwetu unakwenda kufanya nini kwa Dkt.Zainab Chaula?. Mwanakwetu akamwambia ndugu huyu kuwa anakwenda kwa Dkt.Zainab Chaula kwa kuwa ni bosi wake. Godfrey Richard mtu mwema sana, mkarimu na mcheshi akasema,

“Na mimi natoka kwa bosi wetu, Watanzania mwenzetu, Daktari wetu na aliyeopo ofisini mwetu.” Mwanakwetu akaagana na ndugu Richard na kuingia kwa Dkt Zainab Chaula.

Hapa mwanakwetu alijitambulisha kwa kiongozi huyu na kumuueleza juu ya kuhamishiwa na kupangiwa majukumu mengine kwa Dkt.Mshana,“Nia tufahamu hili siku nyingine kama tumekosea, tusikosee tena, je shida ni nini?.

Mwanakwetu alipouliza swali hilo, Dkt.Zainab Chaula alikuwa na majibu mzuri sana wakati huo huo na mwanakwetu kujua pa kuanzia na kufahamu aliyefanya hivyo na hoja zake ni nini? Mjadala ulikuwa mzuri na wamaelewano makubwa huku mwanakawetu akijifunza pia tabia za Dkt.Zainab Chaula. Baada ya mazungumzo hayo alitoka na kuagana na kiongozi huyo na kurudi alipotoka.


Mwanakwetu alipofika Mbozi na kumfuata aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo na kumuuliza juu ya Dkt.Abdul Mshana suala lake lilikuwaje? Ndugu huyu alijibu kuwa alifika katika kituo kimoja cha afya alipokuwa akiuliza maswali alibaini kuwa Dkt. Mshana hakuweza kumjibu vizuri maswali yake. Mwanakwetu aliuliza kama kuna lingine dhidi ya tabibu huyu ndugu huyu akasema hakuna.

“Si jambo la hekima kutazama kipengele kimoja tu tunapofanya maamuzi juu ya mtu yoyote yule maana hapo unafanya upimaji na tujitahidi kupima kwa haki kwa vipengele vingi maana hata shuleni mwanafunzi kutokufanya vizuri katika Majira ya Nukta siyo kigezo cha kusema hafahamu Hisabati, anaweza akafanya vizuri katika Matrix, Algebra na hata Logarithm, kila mada tunachukua alama kidogo kidogo alafu ndipo utaweza kupima kwa haki katika hisabati hivyo ndivyo ilivyo hata katika mambo mengine.”

Mwanakwetu alitoka hapo na kurudi zake kwake.Siku ya leo mwanakwetu anajipa upofu juu ya alipo Dkt.Zainab Chaula, lakini pia hafahamu kabisa alipo Dkt.Abdul Mshana. Mwanakwetu anatambua kuwa hawa wote ni bado na ni madaktari wa binadamu wanaweza kumtibu binadamu yoyote yule ambao ni mimi wewe, tukumbuke kufanya upimaji wowote kwa kwa haki.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news