Waahidi kuweka maslahi ya Tanzania mbele Bunge la EALA

NA DIRAMAKINI

WAWAKILISHI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameapa kuweka mbele maslahi ya Taifa mbele.
Wabunge hao wapya wa Bunge la Tano la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania wameapishwa katika kikao cha kwanza cha Bunge hilo kilichofanyika Desemba 19,2022 jijini Arusha.

Kikao hicho kwa ajili ya uapisho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi saba wananachama ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudani Kusini.
Wabunge hao walioapishwa licha ya kuapa kuwa watiifu kwa jumuiya hiyo na kuulinda mkataba huo, waliahidi kutanguliza maslahi ya Tanzania pindi watakapoanza majukumu yao mapya ambayo huchukua muda usiozidi miaka 10.

James Ole Milya, ambaye anaingia kwenye bunge hilo baada ya kuwa nje ya duru za kisiasa kwa muda, alisema yuko tayari kulinda maslahi na vipaumbele vya nchi bungeni humo.
Mbunge huyo wa zamani wa Simanjiro alibainisha kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki imejaliwa rasilimali nyingi, akisema kuwa kama mbunge mpya atajipa jukumu la kuhakikisha kuwa Watanzania wanazitumia vyema fursa hizo.
"Nimekuwa na uzoefu wa kutosha wa kuhudumu kama mbunge, lengo langu pekee litakuwa kutanguliza na kutetea maslahi ya Tanzania katika Bunge la EALA,"amesema.

Naye Dkt.Shogo Mlozi amesema,ni shauku yake kuona anapigania na kutetea maslahi ya Taifa katika Bunge la Afrika Mashariki.
Amesema,nchi zote washirika zina hisa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kwamba jukumu lao kama wabunge ni kuhakikisha wanalinda na kutetea Mkataba wa EAC ikiwemo maslahi ya Taifa.

Wengine walioapishwa ni pamoja na Machano Ali Machano, Mashaka Ngole, Ansar Kachwamba, Dkt.Ng’waru Maghembe, Dkt.Abdullah Makame na Angela Kizigha.

Wote wawili, Dkt.Maghembe na Makame wanakamilisha muhula wa miaka mitano uliosalia huku Bi. Kizigha akirejea baada ya kuhudumu katika Mkutano wa Tatu wa EALA kati ya 2012 na 2017.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Dkt.Stergomena Tax pia alikula kiapo kama mjumbe wa baraza hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Tax akijibu maswali ya waandishi wa habari,aliwapa changamoto wabunge wa Tanzania kuendeleza ajenda ya mtangamano wa EAC.

"Nchi inatamani kufanya biashara zaidi na majirani zake, natarajia hii pia ni miongoni mwa ajenda yenu kuu mnapoanza majukumu yenu leo,"alisema.
Waziri pia alitoa changamoto kwa wanachama wa EALA kuweka kipaumbele pia katika kufikiwa kwa Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki, ambao ni nguzo ya tatu ya muungano wa wanachama wa jumuiya hiyo.

Uapisho huo umekuja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwachagua wabunge tisa ambao wataiwakilisha nchi katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EELA).
Ni kupitia uchaguzi uliofanyika Septemba 22, 2022 bungeni jijini Dodoma ambapo kati ya wabunge hao tisa, mmoja ni wa upinzani kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambaye ni Mashaka Ngole.

Spika wa Bunge, Dkt.Tulia Ackson siku hiyo aliwatangaza Angela Kizigha, Dkt. Shogo Mlozi, Nadra Mohammed, Dkt. Abdullah Makame, Machano Machano, Ansari Kachwamba, James Millya na Dkt.Ng'waru Maghembe ambao wote ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Miongoni mwa wagombea walioangukia pua kwenye kinyang’anyiro hicho ni Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo akizidiwa kura na Mashaka wote kutoka vyama vichache vyenye uwakilishi bungeni.

Pia, waliohudhuria wakati wa kuapishwa kwa wajumbe wa EALA ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa aliyemwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news