Waathirika dawa za kulevya 114 wahitimu mafunzo ya ujuzi kwa njia ya mtandao Kibaha

NA MWANDISHI WETU

ELIMU ni Ujuzi kwa njia ya Mtandao imeibua vijana 114 ambao ni waathirika wa dawa za kulevya baada ya kupata mafunzo katika fani mbalimbali na kuhitimu katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha mkoani Pwani.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha akitoa vyeti kwa wanafunzi waliomaliza masomo ya miezi mitatu kwa njia ya mtandao.

Katika sherehe za mahafali ya 50 ya chuo hicho yaliyofanyika Kibaha, jumla ya wanufaika 6,157 wamehitimu katika fani mbalimbali za kuendeleza ujuzi ambapo mafunzo hayo yalitolewa kwa muda wa miezi mitatu kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia (WB).
Akiongea wakati wa kuwatunuku vyeti mgeni rasmi Prof. Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI amesema, mafunzo ya ujuzi yamewarudisha ndugu zetu 114 waliotengwa na jamii kutokana na kuathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya.

"Nimefarijika sana kusikia kwamba kati ya wanufaika 6,157 waliosoma kwa njia ya mtandao, 114 ni ndugu zetu kutoka kundi la waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya na leo hii niko hapa kuwapa vyeti vyao ili wakaanze kufanya shughuli za kuwaingizia kipato".
Baadhi ya wanufaika ambao ni wahitimu wa mafunzo ya ujuzi kwa njia ya mtandao wakiwa katika sherehe ya mahafali ya 50 katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.

Prof. Shemdoe ameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kutoa ufadhili wa mafunzo ya Ujuzi kwa njia ya Mtandao ambapo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kilipata kiasi cha Shilingi Milioni 131.2 na kimetoa mafunzo hayo kwa miezi mitatu.
Aidha, Prof. Shemdoe amewaasa wahitimu wote wa mafunzo ya ujuzi kwa njia ya mtandao kutumia ujuzi walioupa kuzifikia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa kujiunga katika vikundi na kuomba mikopo kutoka Mifuko ya Halmashauri na Mfuko wa Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi kwani ipo kwa ajili yao na Serikali imetenga fedha za kutosha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania, Bw. Waziri Salum amesema, Serikali inatambua mchango wa vijana hasa kama nguvu kazi ya Taifa na ndiyo maana inatenga bajeti kwa ajili ya miradi ya kuendeleza ujuzi ili waweze kujiajiri ama kuajiriwa.

Amesisitiza kwamba, ni wakati muafaka sasa kwa vijana kuchangamkia fursa za mafunzo ya kuendeleza ujuzi bila kujali kama wana elimu ya juu (Degree) ili waweze kuzifikia fursa zinazolewa kupitia elimu hiyo kwa haraka zaidi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe (Mgeni Rasmi) akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa mwanafunzi wa fani ya Ufugaji wakati wa mahafali ya 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.

"Nimekutana na vijana wengi sana ambao ni wahitimu wa elimu ya juu lakini hawajapata ajira na wameamua kujiingiza kwenye elimu ya ujuzi na leo wanazalisha bidhaa mbalimbali ziko sokoni na pia wametengeneza ajira kwa wenzao"
Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bw. Waziri Salum akiangalia aina mbalimbali za kuku wanaozalishwa na wanafunzi wa fani ya ufugaji kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha alipohudhuria mahafali ya 50 chuoni hapo.

Mkurugenzi Waziri ameupongeza uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha na kusema kimekuwa chuo cha mfano kwa kudahili jumla ya wanafunzi 6,157 ukilingalisha na lengo walilowekewa na kudahili wanafunzi 300 hadi 400.
Jackline Munuo ni mmoja kati ya wanufaika wa mafunzo ya ujuzi kwa njia ya mtandao ambaye ametokea mkoani Singida akiwa ni muhitimu kutoka Chuo Kikuu Dodoma na alimaliza mwaka 2013. Kupitia mafunzo ya kuendeleza ujuzi amejifunza fani ya ushonaji nguo na hadi sasa ana uwezo wa kushona nguo za familia yake na za wateja pia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news