Wafichua ukatili kwa wanafunzi maeneo ya uvuvi

NA FRESHA KINASA

BAADHI ya wanawake wanaofanya kazi za kiuchumi na biashara ndogondogo katika maeneo ya mialo ya samaki katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara wamesema vitendo vya wanafunzi kuacha shule na kujiingiza katika shughuli za uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki ni ukatili kwa watoto.
Ambapo wameiomba jamii kushiriki kikamilifu kudhibiti hali hiyo ili kuhakikisha watoto wanapata elimu kwa manufaa yao na Taifa kwa siku za usoni.

Hayo yamesemwa Desemba 2, 2022 na wanawake wanaojishughulisha na shughuli za uvuvu na biashara za mazao ya samaki wa Wilaya ya Musoma kutoka kata za Bukumi, Bukima, Bwasi na Kiriba walipotembelea Mwalo wa Makoko ili kujifunza na kubadilishana uzoefu wa biashara na fursa za masoko.
Wanawake hao wamewezeshwa na Shirika la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) kupitia Mradi wa Funguka kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia uliozoeleka maeneo ya uvuvi unaotekelezwa kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society katika halmashauri za Wilaya ya Musoma na Bunda.

Lucia Juma ni mwanamke kutoka Kata ya Kiriba amesema, wazazi kutowapeleka watoto shule ni ukatili na ukiukwaji wa haki za watoto, hivyo lazima wahakikishe haki hiyo inazingatiwa kikamilifu kwani ni haki yao ya msingi.
"Kutompeleka mtoto shule, na kumwacha anajishugulisha na shughuli za uvuvi mdogomdogo ziwani ni ukatili dhidi ya mtoto, wazazi wawajibike kwa kutimiza wajibu wao,"amesema Lucia wakati akichangia katika majadiliano yaliyofanyika katika ofsi za BMU mwalo wa Makoko Manispaa ya Musoma.

Naye Benta Daniel mfanyabiasha wa kuuza dagaa katika mwalo wa Makoko amesema,wanawake wanayo nafasi kubwa katika malezi ya watoto, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kujenga watoto ili wakue kwa kuzingatia maadili ya jamii na tabia njema.

Benta amekemea baadhi ya vitendo vya watoto wa kike katika maeneo ya mialo yakiwemo mavazi na matumizi ya maneno yasiyo na staha kwani kufanya hivyo ni kuwarithisha watoto tabia zisizo njema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa BMU Mwalo wa Makoko, Elisha Onyango amesema Mwalo huo ndiyo mwalo pekee katika ukanda huo ambao hauna watoto wengi wanaofanya kazi za uvuvi na uchakataji wa samaki kutokana na mkazo unaofanywa kwa kushirikiana na wananchi kwa kuwazuia wanafunzi na watoto wadogo kujishughulisha na uvuvi na ajira katika eneo hilo ukilinganisha na mialo mingine.

Onyango amewaeleza washiriki hao kuwa BMU Makoko imekuwa ikiwafikisha katika ofisi za Serikali za mitaa watoto wanaoacha shule na kujiingiza katika shughuli za uvuvi ambapo wazazi pia wanashirikishwa katika kufikia maamuzi ya kuwasaidia watoto kuendelea na masomo.

Kwa upande wa Shirika la VIFAFIO kupitia mratibu wa maradi huo, Robinson Wangaso amesema pamoja na wanawake hao kujadili vitendo vya ukatili wa kijinsia uliozoeleka maeneo ya mialo, lakini pia ziara hiyo imelenga kuwaunganisha na wanzao wa mwalo huo wa Makoko ili waweze kujifunza mbinu mbalimbalia za kibiasha pamoja na fursa za Masoko.
Wangaso amesema kwamba, changamoto za dhana ya ukatili wa kijinsia maeneo ya uvuvi ni nyingi, hivyo wadau wengine wajitokeze kufanya kazi na kundi hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limeachwa pembezoni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news