WAMEREKEBISHA SAA: Ni muda rasmi wa masomo, saa za kazi Rwanda

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI ya Jamhuri ya Rwanda imefanya mabadiliko katika muda rasmi wa masomo na saa za kazi kama hatua ya kutoa nafasi kwa pande zote kuwajibika kwa ufanisi ili kuleta matokeo bora.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkutano wa Baraza la Mawaziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, maazimio hayo yanalenga kukuza elimu bora na pia kuboresha tija mahali pa kazi na ustawi wa familia.
Hayo ni moja ya maazimio yaliyotolewa na kikao cha Baraza la Mawaziri ambacho kiliongozwa na Rais Paul Kagame mnamo Ijumaa, Novemba 11, 2022 nchini humo.

Saa za shule zitakuwa kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi 11 jioni, kulingana na mabadiliko mapya ambapo utekelezaji wake unaanza rasmi Januari Mosi, 2023.

Maazimio hayo yanafikiwa ikiwa madarasa kwa shule nyingi za umma nchini Rwanda yamekuwa yakianza saa 7 asubuhi na kumalizika saa 16:45 jioni kutoka Jumatatu hadi Ijumaa ya wiki.

Aidha,idadi ya saa za kazi pia imebadilishwa kutoka saa tisa hadi nane kwa siku.Saa rasmi za kazi zitakuwa saa nane kutoka saa tatu asubuhi hadi saa 11 jioni.

Kabla ya mabadiliko hayo mapya, muda wa juu zaidi wa saa za kazi nchini Rwanda umekuwa saa 45 kwa wiki, kwa mujibu wa Sheria ya Kazi ya mwaka 2018 nchini Rwanda. Mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa kuanzia Januari Mosi,mwakani, na wizara husika zinatarajiwa kutoa maelezo zaidi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, uamuzi huo wa Rwanda ni mwema hasa ukizingatia changamoto ambazo kundi la wanafunzi na wafanyakazi wanakabiliana nazo wanapoelekea katika maeneo yao kuwajibika, endelea;


1. Wamerekebisha saa,
Nyumbani waweze kaa,
Usingizi ulojaa,
Ili uweze ishia.

2. Ni muda wa kwenda shule,
Kwa watoto wetu wale,
Wapate muda walale,
Usingizi malizia.

3. Ni ndugu zetu wa Rwanda,
Jinsi watoto wapenda,
Wasome bila kukonda,
Afya wakizingatia.

4. Hili Lao lavutia,
Kwetu nikiangalia,
Muda vema kutumia,
Watoto kufundishia.

5. Upite barabarani,
Asubuhi kama nini,
Watoto wako njiani,
Mabasi wasubiria.

6. Jinsi wanajiwahia,
Hapo ungetarajja,
Giza singewakutia,
Bado wangali kwa njia.

7. Panda nao mwendokasi,
Hali zao wengi hasi,
Wanasinzia kwa kasi,
Huku wajisimamia.

8. Wengi sa kumi na moja,
Ongezea saa moja,
Eti elimu ni hoja,
Jinsi wanajiwahia.

9. Rwanda hilo wameona,
Jinsi lilivyowakuna,
Wamefikiria sana,
Muda kujipunguzia.

10. Sababu nyingine nzuri,
Ambayo wamefikiri,
Hawakutaka subiri,
Muda jibadilishia.

11. Wazazi nao watoto,
Kuuongeza mvuto,
Itengwe chai ya moto,
Pamoja weze tumia.

12. Hii inasaidia,
Muda wa kukutania,
Mambo kufuatilia,
Jambo la kufurahia.

13. Muda ni mbilli na nusu,
Watoto wawaruhusu,
Madarasa kuwahusu,
Kwa amani kitulia.

14. Wenye kazi saa tatu,
Huo muda ni wa utu,
Muda na watoto wetu,
Kwao huo wasalia.

15 .Na sisi tuangalie,
Waroro tuangalie,
Kuteswka sisalie,
Athari zaitaishia.

16. Kuamka asubuhi,
Kabla staftahi,
Kweli mno wanawahi,
Twapaswa wahurumia.

17. Shule zilivyojazia,
Kote ukiangalia,
Bora tukaangalia,
Kero kuwapunguzia.

18. Muda wao kusinzia,
Na vitanda kutumia,
Vizuri watabakia,
Na afya zitabakia.

19. Lingine kuangalia,
Jipya nimefikiria,
Watoro kiangalia,
Vitu wanavyotumia.

20. Mizigo madaftari,
Kwa kweli huo hatari,
Huko mbele ya safari,
Madhara yatasalia.

21. Hili kulazimishia,
Kaunta jinunulia,
Kubwakubwa nakwambia,
Migongo wanaumia.

22. Ukimbeba mtoto,
Na begi ule uzito,
Hatari kama kokoto,
Ila wanavumilia.

23. Kuwe na utaratibu,
Hili tatizo kutibu,
Haraka lete majibu,
Shida kuwapunguzia.

24. Tusaidie watoto,
Shule ziwe na mvuto,
Waachane na msoto,
Shule watafurahia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

1 Comments