Waziri Mchengerwa awamegea Watanzania yasiyofahamika kumhusu Bibi Titi Mohamed

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Utamaduni,Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amesema,utamaduni wa kuendelea kuwaenzi waasisi wa Taifa ni miongoni mwa siri ya kipekee inayosaidia kuharakisha maendeleo katika nyanya mbalimbali.
Ameyasema hayo leo Desemba 14, 2022 ikiwa ni siku ya kwanza ya Tamasha la Bibi Titi Mohamed Memorial Art Festival ambalo limewakutanisha mamia ya wakazi na wananchi wa Wilaya ya Rufiji wakiwemo wageni kutoka nje ya wilaya hiyo na Mkoa wa Pwani.

Tamasha hilo limeandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Rufiji chini ya Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ambapo kesho litaendelea katika Uwanja wa Ujamaa Rufiji.

Pia Mheshimiwa Mchengerwa amesema kuwa, huko awali kulikuwa na tatizo kidogo la kutokumbuka kazi kubwa na kazi nzuri ambazo zilifanywa na waasisi wa Taifa letu.
"Wapo watu wengi walifanya kazi kubwa na kazi nzuri, ambao kwa bahati mbaya hatukuwa na desturi nzuri ya kuandika historia zao,hata kuwakumbuka na ikumbukwe kuwa hakuna Taifa lolote ambalo linaweza kupiga hatua kama litasahau kazi kubwa na nzuri zilizofanywa na wale waliotutangulia.

"Na hili linatukumbusha kwamba ili uweze kupiga hatua nzuri hata kimaendeleo lazima ujifunze yale yaliyofanywa na waasisi wa Taifa hili pale ambapo walitoa elimu na maelekezo ni kuangalia uweze kujirekebisha, kujifunza na uweze kupiga hatua kwenda mbele.

"Leo ni siku muhimu tunamkumbuka Bibi Titi Mohamed na ikumbukwe tu kwamba harakati za kumkumbuka Bibi Titi Mohamed zilianza na Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshmiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, yeye ndiye aliona umuhimu na mchango mkubwa uliofanywa na Bibi Titi Mohamed na sisi wananchi wa Mkoa wa Pwani hatukuwa na ajizi, tukasema kwamba tumkumbuke Bibi Titi Mohamed,"amefafanua Mheshimiwa Mchengerwa.
Amefafanua kuwa, mwaka jana walifanya sherehe kubwa katika Mkoa wa Pwani katika Wilaya ya Rufiji ambapo ndipo uzazi wa Bibi Titi Mohamed ulipo.

"Ni hapa Rufji. Yeye (Bibi Titi) alikuwa Mbunge wetu wa kwanza katika Mkoa wa Pwani, lakini mbunge wa kwanza katika wilaya hii ya Rufiji.

"Leo tuna mengi ya kujifunza ukiisoma historia ya Bibi Titi Mohamed, ukiadithiwa historia ya Bibi Titi Mohamed utajua alikuwa mtu wa aina gani, alikuwa mtu mzalendo kila Mtanzania analo jambo la kujifunza sio wanawake tu hata sisi vijana wa kiume, alikuwa shupavu, jasiri, mtu aliyetamani kuona kila mtu yuko huru.
"Inawezekana kabisa mafanikio ya nchi yetu leo yanatokana na kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa taifa letu akiwemo Bibi Titi Mohamed ambaye alikuwa mstari wa mbele bega kwa bega na Mwalimu Nyerere.

"Alikuwa kiongozi wa kwanza mwanamke hapa Tanzania, lakini kule nchini Kenya wakati wa kudai Uhuru kule alikuweko akihamasisha wanawake amekwenda mpaka Zanzibar akihamasisha akiwataka viongozi kwamba hawawezi kufanikiwa iwapo wanawake watabaki nyuma.

"Akasema wanawake watoke majumbani waende wakafanye siasa kwa sababu ya ushawishi walionao, ukweli wao na nguvu walionayo katika jamii.

"Sisi vijana tunajivunia sana, sisi ambao tulipata bahati ya kumuona Bibi Titi Mohamed, sisi ambao tumeweza kusoma na kujionea historia namna ambavyo harakati za ukombozi, namna ambavyo alikuwa mzalendo, mkweli akiamini analoliamini akimhamasisha kila mmoja wetu kudai Uhuru akimtaka kila Mtanzania kipindi kile Tanzania Bara ajiunge na TANU ili kwenda kudai Uhuru.
"Kwa hiyo yapo mambo mengi ya kujitoa mhanga kwa ajili ya taifa lake na mengine mengi kwa ajili ya maendeleo Bibi Titi aliyahamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili wakati ule wa miaka ya 60, kipindi kile Bibi Titi bungeni akiwa anadai wakazi wa eneo fulani waweze kupatiwa taa za barabarani lipo neno alilolisema ambalo Mwalimu Nyerere akiwa Waziri Mkuu alihakikisha anahamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili.

"Lipo neno alilitumia ambalo lilihamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani ya Bunge haya yote na mengine mengi tukisema tuyaeleze tutakesha,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Mchengerwa.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Mchengerwa amefafanua kuwa, "Haya yote yalifanywa na Bibi Titi Mohamed na sisi tunatamani kwamba mchango wa waasisi hao mchango wa mwanamke ulikuwa mkubwa ukimuacha Bibi Titi Mohamed wapo wanawake wengine wengi katika orodha tutawasikia kesho hawa mchango wao hautambuliwi, wanatambuliwa tu baadhi ya wanaume, hawa wanawake walifanya kazi kubwa sana.
"Wako wengi hawatambuliwi, na wengine historia zao hazijaandikwa tunayo kazi kubwa sana kila mmoja wao historia zao ziandikwe ziweze kutunzwa vizazi na vizazi miaka 200, miaka 300, miaka 500 tusipoyafanya haya leo vizazi vyetu havitajua kwamba tulipokwenda kupigania uhuru mambo gani yalifanyika, ushawishi gani tuliufanya nani alikiwa mstari wa mbele.

"Wako wengi ambao walifanya makubwa, lakini pasipo kuandikwa historia zao zitapotea kuna umuhimu mkubwa sana kuandika historia yao kuwa na siku yao kuwakumbuka na sisi tumeshaamua tutakuwa na siku maalum kumkumbuka Bibi Titi Mohamed na tumekubaliana na wenzetu ndani ya chama...

"UWT wakiridhia kutakuwepo siku maalum kama sasa ni mwaka wa pili tunamuenzi Bibi Titi Mohamed na tutaendelea na utaratibu huu iwe leo, kesho na kufanya matamasha na dua kwa sababu Bibi Titi Mohamed hakuwa tu kiongozi wa siasa bali alikuwa mwanasanaa na pia aliwahi kuwa Naibu Waziri katika sekta hii ya Sanaa na mambo mengine mengi yenye mchango mkubwa."
"Tunakumbuka uzalendo na ujasiri kutoka kwake kutokana na msingi thabiti yeye na viongozi wengine walituachia, Bibi Titi alikuwa Mbunge wa kwanza hapa kwa hiyo ametufunza mengi ule ujasiri wake wa kujenga hoja, kutenda haki na kuharakisha maendeleo leo tuna barabara ya Kilwa Road, barabara hii ilijengwa kwa kumuenzi Bibi Titi Mohamed.

"Leo ina lami, Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Mwinyi alijenga hii kumuenzi, leo pia Kuna mitaa mingi Dar es salaam na sisi tumekubaliana kwamba pamoja na kuwa na siku maalum tunakwenda kuandika haya yote ambayo tumeyazungumza kwa maneno, lakini hayajaandikwa yako mengi sana,"amebainish Waziri Mchengerwa.

UWT

Naye Makamu Mwenyekiti Umoja wa Wanawake (UWT) Taifa, Zainab Shomari amesema kuwa, ushirikiano walio nayo wana Pwani ni moja ya nguzo kuu ya kuimarisha upendo, amani na mshikamano.
Pia amewapongeza wana Rufiji kwa namna ambavyo wamekuwa wakiunganisha nguvu makundi ya vijana, wanawake na wanaume kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

"Kubwa niendelee kuwashukuru na kuwapongeza kwa namna ambavyo mmenionesha mapokezi makubwa, hakika Pwani hakuna shughuli ndogo,kijani imetawala mwanzo mwisho, kijani hii inadhirisha kuwa, Pwani ni CCM na CCM ni kwa Mama Samia na Mheshimiwa Mchengerwa,"amefafanua Bi.Shomari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Pwani, Zainabu Vullu amesema kuwa, ni jambo la heri kwa makundi mbalimbali ya vijana, wanawake na wazee kujitokeza kwa wingi katika siku ya kwanza ya Maadhimisho ya Tamasha la Bbi Titi Mohamed

Amesema, kuasisiwa kwa Tamasha la Bibi Titi linadhirisha kuwa, viongozi wote kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo wanathamini mchango mkubwa wa waasisi wa Taifa letu akiwemo Bibi Titi Mohamed.

"Mwitikio huu unadhirisha namna ambavyo mchango wa Bibi Titi wakati wa uhai wake ulivyokuwa na manufaa makubwa kwa taifa letu, na Wanarufiji ambapo alizaliwa ingawa asilimia kubwa ya maisha yake aliyatumkia nje ya Rufiji.Lakini alitupatia mengi na mazuri, aliwakomboa wanawake na pia aliwakomboa wanaume. Ni imani yangu kuwa, tutaendelea kuwaenzi waasisi wetu akiwemo Bibi Titi Mohamed kwa namna ambavyo walijitoka kwa manufaa ya jamii zetu na Taifa kwa ujumla,"amefafanua Vullu.

Bibi Titi

Historia naonesha, Bibi Titi Mohammed alizaliwa Juni mwaka 1926 huko Rufiji ingawa muda mwingi aliutumia nje ya wilaya hiyo kwa maslahi mapana ya Taifa hususani katika harakati zake za kuwakomboa wanawake.

Bibi Titi alikaririwa siku moja akisema, " Dhumuni langu kubwa ni kuhakikisha naamsha akili za wanawake waliolala na kubadilisha fikra na mitazamo yao na kuwaaminisha kwamba Uhuru wa Tanganyika utapatikana kama wanawake watajitambua".

Pia alikuwa muasisi wa Umoja wa Wanawake Tanganyika (UWT) uliokuja kuundwa rasmi mwaka 1963, wakati wa harakati za kupigania Uhuru.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news