WAZIRI MKUU AAGIZA HOSPITALI YA KATAVI IANZE KUTOA HUDUMA

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, Dkt. Patrice Serafin ahakikishe ifikapo Januari Mosi , 2023 hospitali hiyo iwe imeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Muonekano majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya Mkoa wa Katavi, Disemba 12, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim ametoa agizo hilo Disemba 12, 2022 baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ambayo inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 12.4 itakapokamilika na imefikia asilimia 92 ya ujenzi.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Meneja wa TANESCO mkoa wa Katavi kuhakikisha ifikapo Disemba 23, 2022 awe amefikisha huduma ya umeme katika hospitali hiyo.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutawezesha kulaza wagonjwa 170 na hivyo kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa jamii.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia imeanza kuweka huduma ya kipimo cha CT-SCAN katika hospitali zote za mikoa. “Kwa mara ya kwanza Katavi watapata huduma ya kipimo cha CT-SCAN katika hospitali hii.”

Naye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amedhamiria kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

“Dhamira hii njema ya Rais Dkt. Samia tunaiona na ndio maana hapa manispaa ya Mpanda kunajengwa vituo vya afya vitano na vipo katika hatua ya umaliziaji, pia ametoa shilingi milioni 150 kwa ajili ujenzi wa zahanati.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news