Waziri Mkuu:Tutaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa OACPS kudumisha amani

NA MWANDISHI WETU

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) katika kudumisha usalama na amani miongoni mwa nchi washirika.

Amesema, pia Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Jumuiya hiyo katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wao.

Amesema hayo Desemba 10, 2022 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Munngano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 10 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Interconental jijini Luanda, Angola.

Amesema licha ya changamoto ambazo nchi hizo zimeendelea kupitia, ikiwemo janga la Uviko-19 na athari za migogoro inayotokea duniani, Jumuiya hiyo imeendelea kushirikiana kikamilifu katika kutimiza malengo husika na kuratibu shughuli zake kwa maslahi ya nchi wananchama.

“Tanzania itaendelea kuwa mshirika thabiti katika jumuiya hii na ili kuhakikisha malengo ya nchi washirika yanatimia ni vyema kila mmoja wetu akajenga nia hiyo ili kupata mafanikio ya pamoja.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo malengo mengi ya pamoja yamefikiwa na manufaa yamepatikana kupitia programu mbalimbali na utekelezaji wa miradi ya ubia miongoni mwa nchi washirika “licha ya mafanikio hayo bado jitihada thabiti zinahitajika ili kupata mafanikio zaidi”

“Hatujafanya vya kutosha kutimiza kikamilifu malengo ya kuanzishwa kwa OACPS, hivyo, ni vema tuendelee kutekeleza sera, shabaha, programu na miradi tuliyoweka ili kufikia malengo tarajiwa.”

Waziri Mkuu amesema mshikamano miongoni mwa nchi wanachama ndio nguzo pekee inayoweza kuziweka nchi zote salama ikiwa ni pamoja na kuleta maendeleo ya kweli yanayowagusa wananchi moja kwa moja.

Jumuiya ya OACPS ina jumla ya Nchi Wanachama 79 kutoka Afrika, Karibiani na Pasifiki yenye madhumuni ya kuimarisha mshikamano, umoja na maendeleo kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo ikiwemo Umoja wa Ulaya na wadau wengineo ili kufikia maendeleo endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news