YULE ANAYEUMIZA, NAYE NI WA KUUMIZA

NA LWAGA MWAMBANDE

MOSES Phiri ambaye anatajwa kuwa mshambuliaji hatari wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam amewapa tafakari nzito mashabiki wa klabu hiyo na hata wafuasi wake baada ya kuonekana kuwa ni majeruhi.

Ni majeraha ambayo huenda yanatokana na kile ambacho kinatajwa ni kuchezewa michezo ya rafu, baada ya klabu hiyo kuumana na Kagera Sugar hivi karibuni ambapo walitoka suluhu ya bao moja kwa moja uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera.

Phiri anaonekana kuwa hatari zaidi katika safu ya ushambuliaji ya Simba, kwani hadi sasa amefunga mabao 10 kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, rafu za namna hiyo hazikubaliki. Endelea;

1.Yale makosa ya kadi,
Yaani nyekundu kadi,
Bora yawe na miadi,
Ili yasijirudie.

2.Ukimuumiza mtu,
Kwa hicho chako kiatu,
Umeshajiumiza tu,
Upigwe usirudie.

3.Kama ametoka nje,
Muda wake umpunje,
Na wewe ukae nje,
Kufanya usirudie.

4.Pale tunatangaziwa,
Ya kwamba amezidiwa,
Nawe kooni kalowa,
Ili yasijirudie.

5.Kwa muda mwezi mmoja,
Hatutakuwa pamoja,
Hapa ninaleta hoja,
Mabaya yasirudie.

6.Huyo alomuumiza,
Naye aende gereza
Kwenye mpira fukiza,
Makosa yasirudie.

7.Muda anajiuguza,
Huyu asiweze cheza,
Hiyo itatokomeza,
Makosa yasirudie.

8.Kwani kuna wachezaji,
Rafu zao hawachuji,
Kama kuua vipaji,
Hawa tusiwaachie.

9.Nje miezi mitatu,
Buti kwa makusudi tu,
Na yeye asicheze tu,
Haya yasijirudie.

10.Nje miezi mitatu,
Huyu eti mechi tatu,
Ni utaniutani tu,
Maadhabu tukazie.

11.Mchezaji akijua,
Akiua ajiua,
Kufanya atateua,
Yasije yamrudie.

12.Lakini kama ajua,
Anapona akiua,
Vipaji ataviua,
Na cha kwake kisalie.

13.Ni vema tuangalie,
Haya yasijirudie,
Wachezaji watulie,
Kufanya wasirudie.

14.Yule anayeumiza,
Naye ni wa kuumiza,
Hilo abaki awaza,
Ili yasijirudie.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news