Maagizo ya Waziri Kairuki kuhusu elimu yawagusa wakuu wa wilaya,mikoa nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Angellah Kairuki amewataka wakuu wote wa mikoa na wilaya nchini kuendelea kuwa karibu na sekta ya elimu na kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu unaotolewa.
Mheshimiwa Kairuki ametoa maagizo hayo Januari 25, 2023 katika kikao kazi cha uboreshaji wa usimamizi wa elimu msingi, na sekondari na maafisa elimu kata, wakuu wa shule za sekondari, walimu wakuu wa shule za msingi na viongozi wa elimu ngazi ya halmashauri mkoani Dar es Salaam.

Amesema, maagizo hayo yakitekelezwa kikamilifu yatawezesha kupandisha viwango vya ufaulishaji ambapo lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2024 asilimia 100 ya wanafunzi wanafaulu na kujiunga na kidato cha kwanza.

Pia amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imewekwa vizuri miundombinu na mazingira ya shule, hivyo jukumu limebaki moja la kuhakikisha kila mmoja anatekelea wajibu wake ili kuyafikia matokeo chanya katika Sekta ya Elimu.

"Baada ya kuweka uwekezaji mkubwa katika shule hizo, basi elimu inayotoka katika shule zetu inapaswa kuwa na ubora wa hali ya juu.

"Viongozi wetu waendelee kusimamia na kufanya ufuatiliaji na kusimamia suala zima la madili, nidhamu lakini pia utekelezaji wa mpango kazi wa ubora wa elimu katika mikoa, wilaya pamoja na halmashauri zetu na kata na katika shule zetu husika,"amefafanua Waziri Kairuki.

Pongezi

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Kairuki amempongeza Mkurugenzi wa Elimu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Vicent Kayombo kwa kuandaa mkakati wa utendaji kazi ambao unalenga kuongeza ufanisi.

"Katika hili, Mkurugenzi wa Elimu nikupongeze kwa uandaaji wa mkakati wa utendaji kazi au mkataba. Pia ninapongeza mikoa yote kwa namna ambavyo nimeona mnaendelea kusaidiana kuanzia chini, ni imani yangu mtaweza kutekeleza kwa mujibu wa vigezo wa viashiria vyote.
"Wakurugenzi wetu na wakuu wa wilaya ni vyema wakapata mkakati huo. Kwa upande wa maafisa elimu wilaya na mikoa nao ni vyema mkaendelea kutekeleza wajibu wenu na viongozi wengine katika ngazi za msingi na sekondari katika wilaya na kata nao pia wakajua wajibu walio nao.

"Lakini pia waweze kuona wajibu walionao katika kusimamia viongozi wote walioko chini yao na mchango walionao katika kuinua kiwango cha elimu na ubora wake. Vile vile nitoe rai kwa walimu wote pamoja na viongozi wengine kuhakikisha tunajiwekea mpango kazi wa siku, wa wiki, wa mwezi wa nusu mwaka na pia mwaka.

"Lakini pia ninyi walimu ni wafuatiliaji wazuri sana, kwenye hili mmekuwa mkilifanya vizuri sana, lakini kwa wale ambao mmekuwa hamtekelezi basi ni imani yangu mtaweza kutekeleza, lakini mpango huo uwe unaoeleweka, unaotekelezeka kwa upande wa vikao, walio wakuu mtaendelea kufanya vikao na walimu walio chini yenu, waratibu elimu kata mtaweza kutembelea shule zenu na maafisa elimu wilaya mshuke chini,"amefafanua na kuagiza Waziri Mheshimiwa Kairuki.

Ushirikishwaji

Pia, Mheshimiwa Kairuki amesema, wanapaswa kuendelea kuwashirikisha wazazi pamoja walezi kwa ujumla wake wajue wajibu walio nao kwenye makuzi na malezi ya watoto wao wawapo nyumbani.

Sambamba na ulinzi wa watoto wao wanapokuwa nyumbani ili kuweza kuwasoma na kuwafahamu vizuri watoto wao wanapokuwa na changamoto iwe rahisi kutoa taarifa na kuzitatua.

"Na sisi kama viongozi wa elimu tunao wajibu wa ulinzi, malezi na makuzi kwa watoto hao tuendelee kuwalinda dhidi ya ukatili wa vitendo mbalimbali dhidi yao, lakini kubwa zaidi kuwajengea kujiamini wapo wengine wana mengi yanayowasibu, lakini wanashindwa kuyatolea taarifa kwa sababu wamejengewa roho ya hofu, wametishwa wamewekewa hofu, inakuwa ni vigumu kwao kusema, lakini watoto wetu tuwaelimishe wanatakiwa kutoa taarifa.

Nidhamu

"Taarifa hizi wanatakiwa kuzitoa,maafisa wote wa elimu muwe na maadili, suala la ulevi nafikiri ilikuwa Tanga kaja mmoja kwenye kikao kalewa, nimemtuma mkuu wa wilaya akathibitishe pale, nimemtuma mkurugenzi akathibitishe kalewa.

"Nikamwambia RAS angalia taratibu za kinidhamu nini kinachotakiwa kufanywa, lakini nikasema tushirikishe vyombo. Niseme tu kwamba suala la ulevi kwa ujumla wake halifai kabisa kwenye maeneo ya kazi,"amebainisha Waziri Kairuki

Mkurugenzi Elimu

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Vicent Kayombo amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kipindi kifupi imefanya mambo makubwa katika Sekta ya Elimu ikiwemo miundombinu, vitendea kazi na kuwajengea uwezo watumishi wa sekta hiyo.

Kayombo ameyasema hayo katika kikao kazi hicho cha uboreshaji wa usimamizi wa elimu msingi, na sekondari kati ya Waziri wa OR-TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki na maafisa elimu kata, wakuu wa shule za sekondari, walimu wakuu wa shule za msingi na viongozi wa elimu ngazi ya halmashauri mkoani Dar es Salaam.

"Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha elimu nchini yako mambo mengi imefanya,jambo la kwanza ni kutekelezwa kwa Sera ya Elimu bila ada, ambayo iliongeza idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na elimu ya awali, msingi na sekomdari nchini.

"Jambo la pili, viongozi wa elimu wa kata, halmashauri, mikoa pamoja na wathibiti ubora wa shule wanapatiwa vyombo vya usafiri,kwa lengo la kuwezesha kufuatia ufundishaji,na ujifunzaji wa walimu na wanafunzi shuleni, maafisa elimu sekondari magari yameshanunuliwa, na wengine wanategemea kupewa kadri yanavyonunuliwa,"amefanua Kayombo.

Pia amesema,Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jambo kubwa zaidi la kutoa posho kwa viongozi wa shule na kata katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi.

Amefafanua, mbali na hayo pia Serikali imekuwa ikijenga madarasa ya shule za msingi na sekodari ukiwemo ujenzi wa shule za msingi na sekondari mpya ambao umewezesha wanafunzi kuingia kwa awamu moja shuleni mwaka huu.

Changamoto

"Zipo changamoto kadhaa zinazohitaji kutatuliwa ili kuinua ubora wa elimu kwa kasi zaidi. Changamoto hizo tulizozishuhudia, bado kuna wanafunzi waliomaliza darasa la kwanza na la pili bila kuwa na umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

"Pili bado kuna wanafunzi takribani asilimia 20 wanaoshindwa kufaulu na kumaliza elimu ya msingi na kushindwa kujiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza kama inavyoelekezwa na sera ya elimu ya mafunzo,"amefafanua Kayombo.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa,uwepo wa idadi ndogo ya wanafunzi wanaofaulu mtihani wa kidato cha nne kwa daraja la kwanza hadi la tatu ni changamoto, kwani wanayo asilimia 35 tu wanaoweza kujiunga na elimu ya kidato cha tano.

Amesema, wanafunzi wengi wamekuwa wakikosa walimu wa somo la Kiingereza ambalo hufundishwa shule za msingi na pia ni lugha ya kujifunzia katika shule za sekondari. "Changamoto nyingine ni baadhi ya shule kutokuwa na utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi mchana wawapo shuleni.

"Na viongozi wa elimu ngazi za kata,halmashauri, na mikoa kutofuata hatua za ujifunzaji na ufundishaji kwa walimu pamoja na kutotatua kero za walimu,"amebainisha Kayombo.

Tunavuka vipi

Mkurugenzi wa Elimu, Bw.Kayombo anasema, ili kuhakikisha changamoto zote zinapatiwa ufumbuzi wanaendelea kuyafanyia kazi maagizo ya Waziri wa OR-TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki ya kushirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kuboresha elimu msingi na sekondari nchini.
"Kwa madhumuni ya kutatua changamoto hizi, Mheshimiwa Waziri, ulituelekeza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tuandae mikakati itakayotumika kuboresha elimu msingi na sekondari. Mikakati hiyo iliandaliwa na kupata heshima ya kuzinduliwa na Mheshimiwa Kassim Majamiwa, Waziri Mkuu wa Tanzania tarehe 4 Agosti, 2022 mkoani Tabora.

"Kwa madhumuni ya kuleta ufanisi na matokeo tarajiwa katika elimu ya msingi na sekondari ambapo ulituelekeza tufanye kikao kazi hiki ngazi ya mkoa, halmashauri, kata.

"Madhumuni ya kikao kazi hiki ni kuwezesha kuwa na uelewa wa pamoja ili kujipanga upya na kuhakikisha ufundishaji na uwajibikaji ili uwe wenye kuleta matokeo tarajiwa kwa sekondari na msingi nchini kuanzia Januari 2023,"amesema Kayombo.

Pia amesema, kwa Mkoa wa Dar es Salaam wamejipanga vizuri kufanya kazi kwa lengo la kuleta matokeo tarajiwa. "Na kila kiongozi anajua wajibu wake na dhamana aliyopewa kuhakikisha wanafunzi wote wanapata ujuzi, stadi na maarifa yanayotarajiwa katika kila ngazi,"amebainisha Kayombo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news