Musoma Vijijini wampa tano Prof.Muhongo kwa kufuatilia miradi

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wamepongeza ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo unaofanywa na Mbunge wao, Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo.
Wamesema mbali na kufanya ufuatiliaji, Prof.Muhongo amekuwa akitoa taarifa za fedha ambazo Serikali imekuwa ikitoa za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya elimu, afya na maji pamoja na matumizi ya fedha za mfuko wa Jimbo.

Wameyasema hayo wakati wakizungumza na DIRAMAKINI kwa nyakati tofauti mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji kutembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu ya bomba la maji la Mugango-Kiabakari-Butiama Januari 14, 2023 ambapo Prof.Muhongo pia alishiriki na kutoa pongezi zake kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza mradi huo mkubwa unaogharimu fedha nyingi.

Ambapo, mradi huo unagharimu shilingi bilioni 70.5 na kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 73, ukitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2023 kusudi uweze kuwahudumia wananchi takribani vijiji 39. Ukifadhili na Serikali ya Tanzania asilimia (19.48,) BADEA asilimia (31.4) na Saudi Arabia (49.12) unajengwa na mkandarasi UNIK Construction Engineering Lesotho (PTY) LTD.

Veronica Mafuru ni Mkazi wa Kata ya Mugango Wilaya ya Musoma akizungumza na DIRAMAKINI amesema ni faraja kubwa kuona mbunge wao Prof.Muhongo akifanya ufuatikiaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi wa jimbo hilo.

"Mbunge wetu amekuwa mstari wa mbele kufuatilia miradi inayotekelezwa na Serikali na kutueleza hatua mbalimbali zinazofanywa na Serikali kutuletea maendeleo. Pia amekuwa wazi kuweka hadharani fedha za miradi zinazotolewa kupitia Tovuti ya Jimbo la Musoma Vijijini. 

"Hatua hiyo inatusaidia wananchi kujua Serikali inafanya nini katika jimbo letu na kutupa hamasa wananchi kujenga imani zaidi kwa Mbunge wetu pamoja na Serikali ambayo inaongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha za utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji ambao utatusaidia kututua ndoo kichwani wanawake,"amesema Veronica Mafuru.

Fabian Paul Mkazi Etaro amesema kuwa,hatua ya Prof.Muhongo kufuatilia miradi mbalimbali na kuwashirikisha wananchi, inaongeza imani kwa wananchi kwamba anatekeleza majukumu yake kikamilifu na kuonesha uwajibika thabiti kwa ajili ya wananchi ambao walimchagua awatumikie.

"Tumeona kwenye vyombo vya habari baada ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Kilimo Mifugo na Maji kutembelea ule mradi wa Mugango-Kibakari-Butiama Mbunge ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais na jinsi ambavyo wananchi tunausubilia mradi huo kwa shauku kubwa kutuondolea changamoto ya maji. 

"Na pia kunapokuwa na jambo lolote linalogusa maisha ya wananchi Mbunge hutuambia, mfano hivi karibuni Serikali imeonesha nia ya kufufua kilimo cha Umwagiliaji katika bonde la Bugwema alitueleza,"amesema na kuongeza kuwa.

"Mbunge katika ziara zake mbalimbali ambazo hufanya, haachi kutueleza hatua mbalimbali za miradi ya maendeleo zilipofikia nasi kama wananchi tunapoelezwa tunatambua hatua hizo na kupata fursa ya kueleza changamoto zetu kwa uhuru na uwazi na yeye anazishughulikia ambazo ziko chini yake ambazo zinahitaji ngazi za juu yeye ni mkweli lazima aseme atazipeleka juu na akipeleka tu huleta mrejesho. huu ni uwajibikaji ambao mimi ninauita unalenga kutusaidia sisi wananchi,"amesema Fabiani Paul.

Magesa Yusuph Mkazi wa Kata ya Nyakatende Wilaya ya Musoma amesema Prof. Muhongo katika ziara zake amekuwa akiyasema yale ambayo Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia inayafanya. Ambapo amesema pia amekuwa bega kwa bega na wananchi kushiriki ujenzi wa miundombinu ya elimu afya kwa kuwashirikisha kila hatua wananchi na kuwaomba kuzidi kuipa ushirikiano serikali.

"Mbunge Prof.Muhongo amekuwa akitoa hamasa na msisitizo kwetu wananchi jinsi gani tuondokane na umaskini amekuwa akisisitiza tuchape kazi kwa bidii iwe ni uvubi, kilimo au ufugaji pia huunga mkono vikundi mbalimbali vya maendeleo, na pia yeye mwenyewe kutembelea vikundi hivyo na kuvipa hamasa na fedha ili kuona vinajikwamua kiuchumi na pia kueleza hatua ambazo Serikali inakusudia kufanya,"amesema Alphonce Thomas.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news