Rais Dkt.Mwinyi ataja siri za mafanikio ndani ya miaka miwili

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema amani, umoja na mshikamano ndio siri ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akifungua pazia kuashiria ufunguzi wa Hospitali kubwa ya kisasa ya Ghorofa ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Januari 3, 2023 katika shamra shamra za miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, kushoto ni Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi. (Picha na Ikulu).

Pia ameeleza kufunguliwa kwa miradi ya maendeleo ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar kunatokana na kuwepo kwa mapenzi makubwa ya wananchi kwa viongozi wao, jambo alilolisisitiza kuendelezwa ili maendeleo zaidi yaongezeke kama ilivyo azma ya Serikali anayoiongoza.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo kwenye ufunguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza ufunguzi wa miradi kama hiyo ni kuyaenzi na kuyathamini Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga Hospitali katika ngazi mbalimbali ikiwemo za Wilaya kama hiyo, Mikoa hadi Taifa.
Amesema, ndani ya miaka mitano ya uongozi wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kukamilisha haspitali zenye ubora katika mikoa yote ambazo zitatoa huduma bora za afya na hazitomfanya mwananchi kusafiri nje ya nchi kufuata matibabu.

Dkt.Mwinyi amewataka watoa huduma za afya wakiwemo Madaktari, Wauguzi na wahudumu wa afya kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa wanaowahudumia kwani lugha nzuri nazo ni tiba.
Naye Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui aliahidi kuwa Wizara hiyo itaendelea kusimamia na kutekeleza maagizo yote ya Rais kuhakikisha inakuwa na mageuzi kwenye utoaji wa huduma bora za matibabu ili wananchi wanapate huduma nzuri zaidi.

Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Pemba, ilikadiriwa kutumia zaidi ya shilingi billion sita hadi kufunguliwa kwake na tayari imeshatumia zaidi ya shilingi Billion 5.
Aidha, hospitali hiyo itatoa huduma mbalimbali muhimu za matibabu zikiwemo chumba cha ICU, dharura, vitanda vya kujifungulia na huduma za ICT.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news