Rais Dkt.Samia:Hakuna mwanafunzi atayekosa nafasi ya shule kwa uhaba wa madarasa nchini

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, hakuna mwanafunzi atakayekosa nafasi ya kusoma kutokana na changamoto ya ukosefu wa madarasa nchini.

Ameyabainisha hayo kupitia taarifa fupi aliyoitoa kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii Januari 2, 2023 ikiwa zimebaki siku chache kabla ya shule kufunguliwa nchini kote.

"Katika siku 100 zilizopita nchi yetu imefanikiwa kujenga madarasa ya sekondari 8,000 na samani zake nchi nzima. Tunaanza kuyatumia juma lijalo.

"Hatua hii ya kihistoria ni ukombozi kwa wanafunzi zaidi ya 400,000. Hakuna mwanafunzi atayekosa nafasi ya shule kwa uhaba wa madarasa,"ameeleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Awali, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde alisema wanafunzi 1,073,941 waliochaguliwa kidato cha kwanza 2023 wataanza shule kwa wakati mmoja.

Hatua hiyo inafanya kusiwepo na utaratibu wa chaguo la pili kama ilivyozoelekea kutokana na kukamilika kwa madarasa 8,000.

Dkt.Msonde aliyasema hayo hivi karibuni wilayani Kongwa mkoani Dodoma wakati wa zaiara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa.

Alisema, hakutakuwa na changuo la pili kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza Januari, 2023 na kuwasihi wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni kwa wakati.

"Kwa mwaka huu hakutakuwa na second selection (chaguo la pili la wanafunzi) kwa sababu fedha zilizotolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Elimu zimetosha kuboresha miundombinu ya kuwachukua watoto wetu wote kwa intake(mkupuo) mmoja ."

Dkt.Msonde alisema tangu Rais Dkt.Samia aingie madarakani ameshatoa fedha zilizowezesha kujenga zaidi ya vyumba vya madarasa 20,000 ndani ya miaka miwili, hatua ambayo imewaondolea adha watoto kwa kuanza masono kwa pamoja huku wazazi wakiwa hawajachangishwa kitu.

"Katika kukabiliana na ongezeko la wanafunzi kwa mwaka huu Rais Dkt.Samia ametoa shilingi bilioni 160 zilizotumika kujenga madarasa 8,000.Ujenzi wa madarasa hayo nchi nzima umekamilika,"alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news