Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ustawi wa jamii-Rais Dkt.Samia

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ustawi wa jamii kama elimu, maji na afya ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia Maabara ya Kisasa mara baada ya kufungua Skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe iliyojengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Fedha za Uviko-19 kupitia Shirika la Fedha Duniani (IMF). (Picha na Ikulu).

Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Januari 10, 2023 wakati akifungua Skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe katika kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Samia amesema, Serikali itahakikisha wananchi wote wanapata haki yao ya elimu kwa kuimarisha miundombinu ya Skuli ili kuendana na ongezeko la idadi ya watoto wanaohitaji kupatiwa elimu bora.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan akiangalia umahiri wa wanafunzi wa somo la kompyuta katika Skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe mara baada ya kuifungua kwenye Sherehe zilizofanyika Mwanakwerekwe, Zanzibar tarehe 10 Januari, 2023.

Rais Dkt.Samia pia amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na ya Muungano zitahakikisha kunakuwepo mazingira bora ya kujifunza na kufundishia kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani ili kufikia lengo la wanafunzi 45 kwa darasa.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Samia ameipongeza Wizara ya Elimu Zanzibar kwa kuunda Kikosi Kazi cha kuishauri Serikali mageuzi muhimu ya elimu ambayo yatakidhi mahitaji ya ulimwengu wa sayansi na teknolojia katika karne ya 21.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kuashiria ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe iliyojengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Vile vile, Rais Dkt.Samia amesema utekelezaji wa Dira ya Zanzibar ya 2050 pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Taifa (Zanzibar Development Plan) unategemea upatikanaji wa wataalamu kupitia sekta ya elimu.
Hivyo, Rais Dkt.Samia amesema Serikali haina budi kuimarisha wataalamu kwa kuwapatia fani zinazoendana na mahitaji ili kuiwezesha Zanzibar kufaidika na matumizi ya rasilimali ya bahari kupitia mkakati wa kuimarisha Uchumi wa Buluu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news