TANZIA:JAJI MFAWIDHI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA IRINGA, MHE. DKT.JOHN HAROLD KULIMBA UTAMWA AFARIKI

NA DIRAMAKINI

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mheshimiwa Dkt.John Harold Kulimba Utamwa amefariki dunia.
Mheshimiwa Dkt. John Harold Kulimba Utamwa enzi ya uhai wake.

Hayo leo yamebainishwa leo Januari 2, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano- Mahakama ya Tanzania, Artemony Vincent Tiganya.

"Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, anasikitika kutangaza kifo cha Mhe. Dkt.John Harold Kulimba Utamwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa kilichotokea leo Januari 2, 2023 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alipokuwa anapatiwa matibabu.

"Marehemu Mhe.Jaji Dkt.Utamwa amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu ambapo tarehe 17 Desemba, 2022 alilazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Mnamo tarehe 18 Desemba, 2022 alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kuendelea kupatiwa matibabu hadi mauti yalipomfika.

"Marehemu Jaji Dkt.Utamwa alijiunga na Mahakama ya Tanzania tarehe 17/02/1992 akianzia ngazi Hakimu Mkazi. Alipanda ngazi mbali mbali ndani ya Mahakama na hatimaye aliteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 24/6/2010.

"Akiwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alifanya kazi katika kanda za Dar es Salaam, Tabora, Mbeya na Iringa.

"Kufuatia msiba huo, taratibu za maziko zinafanyika nyumbani kwa marehemu Madale jijini Dar es Salaam. Taarifa zaidi kuhusu msiba huu zitaendelea kutolewa,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA LA BWANA LIHIMIDIWE.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news