TULEE WATOTO VIZURI

NA ADELADIUS MAKWEGA

WAKRISTO wametakiwa kuzitunza familia zao vizuri kama ilivyokuwa kwa familia aliyozaliwa Yesu Kristo na siyo kuwaacha watoto wao wanazagaa hovyo katika dunia hiii.
Hayo yamesemwa na Padri Paul Mapalala katika misa ya pili ya Jumapili ya Mwaka Mpya- Mwaka A wa Kanisa, Januari Mosi, 2023 ambayo pia ni dominika ya sherehe ya Maria Mtakatifu mama wa Mungu iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

Akihubiri katika misa hiyo Padri Mapalala alisema kuwa, “Maandiko yanatuambia tufuate utaratibu wa familia hiii na maisha ya wale wazee waliotutangulia, Mama Bikira Maria na Yosefu walimlea vizuri mtoto wao, kwa hiyo na sisi kama wanajumuiya na wana familia tuige mfano huu, tulee familia zetu vizuri, tusiziache zinazagaa hovyo mitaani, tuwafundishe dini, tuwafundishe elimu ya dunia na utamaduni wa Kiristo.”

Padri huyo aliongeza kuwa, familia za sasa zina mkanganyiko mkubwa, wapo wanaolea familia zao vizuri, wanazitunza vizuri sana lakini familia zingine hapana, watoto wako huru mno. Wazazi sasa wanatakiwa wasali na familia zao siyo wakati wa chakula tu na hata nyakati zinginezo.

“Pahala pengine kuwaona wazazi/walezi ni shida labda wakati wa kununua nguo za sikukuu. Kwa maisha ya Kikristo haitoshi mtoto kulelewa na viongozi wa dini tu muendelezo wa malezi uwepo nyumbani maana huko upo muda mwingi."

Misa hiyo ambayo wanakwaya wake waliimba nyimbo zinazofahamika na waamini wengi na kwa ustadi mkubwa iliambatana na maombi kadhaa na mojawapo lilikuwa hili,

“Kwa maombezi ya Bikira Maria mama wa Kristo, uwasaidie wote wanaochochea magomvi, fitina na vita kuacha ubaya huo, pokea ombi letu Baba Mungu.”

Wakati misa hiyo ya pili inafanyika hadi inamalizika, hali ya hewa ya eneo la Chamwino Ikulu kwa juma zima ilikuwa ya jua kali, mvua imepotea kwa siku kadhaa sasa. Nayo mazao kama mahindi yaliyopandwa yanayoota kwa kasi kubwa, lakini yakiwa yamejawa na kiu ya kunyeshewa na mvua ili kuleta matumaini zaidi kwa wakulima wa eneo hili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news