UZINGATIE KIAPO:Naye alitoka hapo

NA LWAGA MWAMBANDE

MARA nyingi hizi kazi za viapo ni ngumu sana kumeza. Kuna mambo anasaidia Mungu, kwani umeapishwa kuwa waziri wa fulani ukitoka ulinzi pembeni, ukiingia ulinzi pembeni.

Kila unakopita heshima tele tele, halafu unaondolewa hapo kupelekwa wizara nyingine ambayo haina itifaki hiyo, ngumu sana kumeza hiyo.

Unafanya kazi kwa mtu au kwa taasisi. Umekaa mahali kwa miaka kadhaa, watoto umezaa pale, wanasoma pale, mara paa! unaambiwa unahamishiwa kituo kingine, tena pengine mazingira yake si mepesi kama hapo ulipokuwa.

Pengine hata unapandishwa cheo, inakuwa shida sana kukubaliana na hali hiyo, na sana sana unaweza kuanza kutafuta wachawi.

Vivyo hivyo kwa watumishi wa Mungu, unaapa kwamba utakwenda kutumika kokote. Unafika mahali, hali unaizoea na mahali hapo panakuzoea kama nyumbani.

Halafu mara inakuja barua ‘YAH: Uhamisho...Moyo kama wachanika, kiapo unakisahau, unatamani uendelee kukaa pale pale.

Inaweza kuwa mtumishi mwenyewe kushawishi abakie, au waumini kushinikiza asiondoke kwa sababu wanazozijua wao.

Lakini ndiyo kiapo. Kukiuka kiapo sawa na kuikana kazi yako. Wako wengine hukana kazi zao na hivyo kuondoka katika mifumo ya ajira zao. Kwa msingi huo, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anaeleza umuhimu wa wote ambao kazi zao zina viapo kuzingatia viapo vyao badala ya kuvivunja. Endelea;

1.Ndizo kazi za viapo,
Huutawali uwepo,
Leo upo kesho hupo,
Utazidisha kuwepo,
Kama watii kiapo,
Vinginevyo wewe hupo,
Hata utake uwepo,
Uzingatie kiapo.

2.Huduma za watu zipo,
Makanisa yao yapo,
Hao hawatoki hapo,
Wala hawana kiapo,
Lakini mwenye kiapo,
Hapo siyo kwako hapo,
Hapo pa wenyewe hapo,
Uzingatie kiapo.

3.Mwokozi alikuwepo,
Na historia ipo,
Naye alitoka hapo,
Kabaki kwenye uwepo,
Kina Petro ndio wapo,
Tena na huduma ipo,
Nao wakitoka hapo,
Wengine watakuwepo.

4.Wewe ni polisi hapo,
Usalama sasa upo,
Sasa watolewa hapo,
Uende kule haupo,
Using’ang’anie hapo,
Kinyume chako kiapo,
Aste ondoka hapo,
Na kwingine kazi ipo.

5.Shambani mavuno yapo,
Watendakazi hawapo,
Umeonekana upo,
Fukuto la Neno lipo,
Watumwa ondoka hapo,
Fuata watu walipo,
Wasiabudu makopo,
Wakati Muumba yupo.

6.Mwalimu na shule zipo,
Wasojua soma wapo,
Usibakie ulipo,
Kule walimu hawapo,
Ila wanafunzo wapo,
Singoje likae jopo,
Likutoe kama popo,
Uzingatie kiapo.

7.Sifa za kibali zipo,
Popote pale ulipo,
Tena Mungu wako yupo,
Wala si wa hapohapo,
Aliyoyafanya hapo,
Pale ulipokuwepo,
Hata hapo uendapo,
Utambue Mungu yupo.

8.Musa alipokuwepo,
Hata kazi yake ipo,
Alidhania hayupo,
Kuamua watu hapo,
Hekima ya mkwe hapo,
Kapata wazee hapo,
Mzigo kuwa haupo,
Kumbe na wengine wapo.

9.Nguvu zake Mungu zipo,
Kwa Musa zilikuwepo,
Alipokosea hapo,
Kaambiwa hapohapo,
Mwisho wa safari hapo,
Na nchi mpya haipo,
Nasi tusifike hapo,
Kikatupata kichapo.

10.Kama kazi ikiwepo,
Na matunda yakiwepo,
Hata kama wewe upo,
Mkono wa Mungu upo,
Sifa siyo zako hapo,
Ni Mungu kafanya hapo,
Utukufu ukiwepo,
Wa kuupokea yupo.

11.Wachungaji wengi wapo,
Na Maaskofu wapo,
Inuka hapo mlipo,
Tafrani isiwepo,
Toeni elimu hapo,
Ukengeufu haupo,
Mazoea kweli yapo,
Kwenye mwanzo mwisho upo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news