Wananchi zitumieni vema fursa za kiuchumi zinazowazunguka-Rais Dkt.Mwinyi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wa Zanzibar kuzitumia vyema fursa za uwekezaji zilizopo kwenye maeneo yao ili kujikwamua na changamoto za maisha.
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi aliyasema hayo katika Kijiji cha Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofungua hoteli ya nyota tano ya, Emarald Resort and SPA.

Amesema, fursa za uwekezaji haziwanufaishi wageni pekee, bali wazawa wana nafasi kubwa ya kuzitumia na kujikwamua na ugumu wa maisha ili kuondokana na mkwamo wa maendeleo kwa kujiongezea kipato na kubadili mfumo wa maisha walionao kupitia fursa hizo.

Amesema wazawa hunufaika kupitia uzalishaji ikiwemo, uvuvi, kilimo na biashara watakazozizalisha ambazo zitawalenga wageni waliopo kwenye maeneo yao.

“Kuna faida nyingi tunazozipata kupitia uwekezaji, zikiwemo ajira, masoko ya bidhaa zetu, na mambo yanayofanywa na wawekezaji kupitia huduma za jamii jumuishi kama kujenga visima, vituo vya afya, umeme, barabara ambapo moja kwa moja zinawanufaisha wananchi,”amesema Dkt. Mwinyi.

Amesema, wawekezaji wameweka imani kubwa serikalini kwa kuwekeza miradi ya mitaji mikubwa, hivyo aliwasihi wananchi kuendelea kuwaunga mkono kwa kushirikiana nao katika kuinua uchumi wa nchi.

Akizungumzia masuala ya ajira, Dkt.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa wote waliopitiwa na miradi ya uwekezaji na kueleza kuwa asilimia 95 ya ajira zinazotokana na wawekezaji zimelengwa kwa wananchi wazawa kuongeza kuwa asilimia tano pekee ndio inayobakia kwa mwekezaji hivyo, aliwataka wananchi kizikimbilia fursa hizo kwa kuonesha uzalendo wakuwapokea wawekezaji kwa vitendo.

“Niseme kwa wananchi mara zote tuwe tayari kuwapokea wawekezaji na kuwasaidia ili wao wanufaike na sisi tunufaike,”aliwasihi Rais Dkt.Mwinyi.

Rais Dkt.Mwinyi aligusia suala la kuimarisha miundombinu kijijini hapo ikiwemo maji na barabara, aliwaeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeweka pesa za kutosha kuondosha kero za maji na barabara kwa visiwa vya Unguja na Pemba na kueleza kuwa katika kipindi kitakachojenga barabara nyingi zaidi ni awamu ya nane ambapo inatarajia kujenga barabara za kilomita 100 hadi 277.

Hata hivyo, aliwaahidi wanakijiji cha Matemwe kwamba Serikali itawajengea barabara zao za kutoka kibuyuni hadi kijini na barabara ya round about hadi Nungwi.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alieleza kasi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imeipa kipaumbele na umuhimu wa pekee sekta ya Uwekezaji kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na kuendelea kuweka mkazo kwenye maeneo yote ya uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji, Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji Vitega Uchumi, Zanzibar (ZIPA), Sharif Ali Sharif, alisema kwa kipindi cha miaka miwili kutoka 2021 hadi 2022, Zanzibar imewekeza miradi 223 ikilinganishwa na kipindi cha miaka sita iliyopita, kutoka 2015 hadi 2020 ambapo miradi 203 iliwekezwa.

Alisema, matarajio ya ZIPA ni kuhakikisha maeneo huru yote ya uchumi, Unguja na Pemba yanakamilika kwa miundombinu sahihi ili kuendelea kuwakaribisha wawekezaji pamoja na kutoa huduma mtandao ili kurahisisha ufanisi wa utendaji wao.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli ya Emarald Resort and SPA, Bw. Aldo Scarapicchia alisifu juhudi za Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa ubunifu wake wakutoa maelfu ya ajira kwa vijana wa Kizanzibari kupita sekta ya utalii na uwekezaji.

Aidha, aliwaahidi Wazanzibari kufanyakazi nao kwa heshima ya kipekee katika kuendeleza ushirikano uliopo baina yao. Alisema, ukarimu wa Wazanzibari kwa wageni ni heshima kubwa wanayojivunia kwa kipindi chote walichoingia Zanzibar tokea mwaka 1992 na kuongeza kuwa Zanzibar ni visiwa vinavyoongoza kwa uzuri kati ya visiwa vya Bahari ya Hindi.

Post a Comment

0 Comments