Waziri Bashe awataka wakulima kuvumilia changamoto za mfumo, asema msimu ujao mambo safi

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe amesema Changamoto zilizopo kwenye mfumo wa utoji wa ruzuku ya mbolea ni za muda mfupi kwani mfumo huo umeanzishwa mwaka huu na mwanzo ni mgumu.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akizungumza na wananchi waliokuwa kwenye foleni ya kununua mbolea kwenye ghala la kampuni la mbolea la ETG, Vwawa Mkoani Songwe tarehe 5 Januari, 2023 akiambatana na viongozi wa serikali na chama.

Amesema mfumo ni mzuri kwani unamtambua mkulima anayelengwa kunufaika na mbolea za ruzuku tofauti na mfumo wa vocha uliotumika miaka ya nyuma na kunufaisha wafanyabiashara wa mbolea pekee.
“Mfumo wa mbolea ya ruzuku una changamoto zake lakini hatuwezi kurudi nyuma sasabu unamtambua mkulima,”Waziri Bashe alikazia.

Waziri Bashe alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Songwe akitembelea maghala ya mbolea na kukagua namna utoaji wa huduma ya mbolea ya ruzuku kwa wakulima unavyoendelea pamoja na kuwasikiliza, kuzungumza na kutatua kero za wananchi.
Waziri wa kilimo, Hussein Bashe ( mwenye t-shirt nyeupe) akizungumza jambo wakati wa kikao kifupi ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Waziri Kindamba (wa kwanza kulia). Mwenye t-shirt nyekundu ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo.

Waziri Bashe amefafanua kuwa lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kumlipia ruzuku mkulima na kwa kutumia mfumo huo Serikali italipia mbolea iliyomfikia mkulima na si vinginevyo.

Katika kutatua changamoto ya misongamano Bashe amewaelekeza wauzaji wa mbolea kuongeza idadi ya watoa huduma za kuuza ili kuweza kuwahudumia wakulima wengi kwa muda mfupi.
Waziri Bashe amewataka wakulima kuwa na subira na kubainisha kufikia msimu ujao wa kilimo changamoto hizo hazitakuwepo.

“Mateso mnayoyapata ya foleni yatakwisha kuweni wavumilivu wakati serikali inajenga mfumo,” Waziri Bashe alimaliza.
Aidha, Waziri Bashe ameuomba uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe kuwa waelimishaji wakubwa wa wananchi juu ya kutunza namba zao za utambulisho wa mkulima ili wasirubuniwe na kuziuza kwa mawakala wasiowaaminifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news