NA MWANDISHI WETU
WIKI ya Sheria mkoani Geita imezinduliwa kama ilivyo kwa nchi nzima kwa kuanza na maandamano yaliyojumuisha watumishi, wadau mbalimbali pamoja na wananchi ambao wote walishiriki kikamilifu.

Wakati anamkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mhe. Waane aliwakaribisha wananchi wote kufika katika vituo vilivyoandaliwa ili waweze kunufaika na elimu itakayotolewa katika Wiki ya Sheria nchini.
Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “Umuhimu wa utatuzi wa Migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: Wajibu wa Mahakama na wadau.”
Mhe. Waane alibainisha kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi unatambulika kisheria, huchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha amani na mahusiano.

Alisema kuwa uwepo wa Wiki ya Sheria hukumbusha kila mwananchi kwamba hakuna aliye juu ya sheria na Mahakama ndiyo chombo pekee kilichoidhinishwa kikatiba kutoa haki.
Mhe. Mkuu wa Wilaya amesisistiza na kuwaomba wananchi wote kuitumia fursa hiyo kupata elimu ya kisheria. “Tunapaswa kuitumia vyema fursa hii ili tuweze kujifunza kupitia vituo hivi na jambo zuri ni kwamba wanaotoa elimu katika wiki hii ndiyo wale wanaotoa tafsiri ya sheria, hivyo tuitumie fursa hii,” alisisitiza.
Akielezea kauli mbiu ya mwaka huu, Mkuu wa Wilaya huyo alisema kuwa imebeba ujumba muhimu kwa kuwa inakumbusha kusuluhisha migogoro kwa kukaa pamoja bila kufika mahakamani, hivyo kuipunguzia Mahakama mlundikano wa mashauri.

Ameomba kama ikiwezekana huduma ya Mahakama Kuu ianze hata kabla ya jengo linalotarajiwa kujengwa kwa kupitia majengo mengine na yeye mwenyewe yupo tayari kutoa ushirikiano kufanikisha mpango huo.