GEDAGEDA:Jino lisilotibika, linafaa kung'olewa

NA LWAGA MWAMBANDE

KILA mmoja wetu anatambua wazi kuwa, meno ni muunganiko wa mfupa wa jino,fizi na mishipa. Katika siku za karibuni, wengi wetu tumekuwa tukikabiliwa na matatizo ya meno.

Haya ni yale matatizo ambayo yanatokea baada ya bakteria na wadudu wengine kuwepo mdomoni, hali hii hufanya mtu kuwa na maumivu makali kwenye meno na mpaka kupelekea kutoa damu au harufu mbaya na kuathiri meno.

Wengi wetu tuna matatizo ya meno ila tunatofautiana, wengine wana matatizo madogo, wengine pia matatizo makubwa huku chanzo cha magonjwa ya meno kwa asilimia kubwa kikitajwa kuwa ni kutokana na mitindo ya maisha ya kila siku.

Hii inagusia upande wa kutozingatia usafi kikamilifu, ulaji, mazingira na tabia mbalimbali ambazo zinachangia kuathiri mfumo wa kinywa. 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, jino likigedageda ni vema ukamuona daktari. Endelea;

1.Jino likigedageda, kamuone daktari,
Wala usipate shida, takushauri vizuri,
Bila ya kupita muda, taepukana na shari,
Jino lisilotibika, linafaa kung'olewa.

2.Jino kiungo muhimu, jinsi linavyotumika,
La mbele hilo ladumu, twaliona ukicheka,
Likigedageda sumu, Amani inaondoka,
Jino lisilotibika, linafaa kung’olewa.

3.Kwa watoto kawaida, kwa meno yao kuchoka,
Huwa yanagedageda, muda wake ukifika,
Usije chukua muda, ng’oa liweze kutoka,
Jino lisilotibika, linafaa kung’olewa.

4.Tofauti na watoto, wakubwa yafahamika,
Kugedageda ni wito, kwamba jino limechoka,
Maumivu ya moto, siyo ya kuvumilika,
Jino lisilotibika, linafaa kung'olewa.

5.Kama linagedageda, hospitalini fika,
Eleza ya kwako shida, kwa wale wanahusika,
Uchunguzi kawaida, ili uweze fanyika,
Jino lisilotibika, linafaa kung'olewa.

6.Kama ni maambukizi, ya kwamba litatibika,
Waweza elezwa wazi, na dawa zikatumika,
Kama imezidi ganzi, kuvumilia wachoka,
Jino lisilotibika, linafaa kung'olewa.

7.Likigedageda jino, haliwezi kutumika,
Vya moto huuma mno, jino linapogusika,
Vya baridi hata neon, utashindwa kutamka,
Jino lisilotibika, linafaa kung'olewa.

8.Tiba za jino ni nyingi, ambazo zinatumika,
Likigedageda wengi, mara moja huchoka,
Vile maumivu mengi, siyo ya kuvumilika,
Jino lisilotibika, linafaa kung'olewa.

9.Jino likigedageda, ni muda wa kuamka,
Usikae kunywa soda, utazidi jeruhika,
Ondoka kwenye kigoda, hospitalini fika,
Jino lisilotibika, linafaa kumg’olewa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news