Kasulu kuendelea kunufaika na mashirika yanayowahudumia wakimbizi

NA RESPICE SWETU

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma itaendelea kunufaika na ufadhili kutoka katika mashirika mbalimbali ya Kimataifa yanayotoa huduma kwenye makambi ya wakimbizi yaliyopo katika halmashauri hiyo.
Akitoa taarifa ya shughuli zinazofanywa na World Vision kwenye sekta ya elimu siku ya wadau wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, afisa ufadhili wa shirika hilo kwa Kanda ya Kigoma, Simon Reuben amesema, World Vision itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii katika halmashauri hiyo.

Amesema kuwa, kwa muda huu, World Vision ina miradi ya aina mbili inayotekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu na kuitaja kuwa ni miradi ya muda mrefu na ya muda mfupi.
"Katika kipindi hiki tunayo miradi ya muda mrefu na ya muda mfupi, miradi ya muda mrefu inayotekelezwa kwa kipindi cha miaka 8 hadi 10 ilianza mwaka 2010 na mingine mwaka 2012, miradi hiyo itaendelea hadi mwaka 2025,"amesema.

Simon aliyekuwa amemwakilisha meneja wa World Vision Kanda ya Kigoma kwenye hafla hiyo, amesema pia kuwa kupitia ufadhili huo, wamekwishajenga vyumba 20 vya madarasa, matundu 135 ya vyoo, ofisi 5 za walimu na kutengenezewa madawati 2120 kwa shule 20 za msingi za halmashauri hiyo.
Aliendelea kueleza pia kuwa, kupitia mradi wa Buhoma unaotelelezwa katika tarafa za Buhoro na Makere, wameweka miundo mbinu ya maji kwenye shule 7 za msingi, na kuwasaidia watoto 7400 wanaotoka katika familia duni kwa kuwapatia sare za shule, madaftari pamoja na kalamu.

Misaada mingine kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na afisa huyo, ni kuwalipia bima ya afya wanafunzi 101, kuwanunulia viti mwendo wanafunzi 12 wenye mahitaji maalumu, kutoa taulo za kike kwa wasichana na kuwapa vyerehani vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi.
Taarifa ya World Vision ilizitaja shule za msingi zinazonufaika na misaada hiyo kuwa ni Muungano, Nyamuganza, Mvugwe, Nyamidaho, Nyarugusu na Kumtundu.

Nyingine ni Kumkambati, Kasasa, Muhanga, Buchuma, Kitagata, Makere, Nyamnyusi, Kisuma, Kitema, Murubanga na Nyakitonto.
Akisoma taarifa ya elimu kwenye kikao hicho, Afisa elimu awali na msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi, amelishukuru shirika hilo na wadau wengine wanaosaidia maendeleo ya elimu katika halmashauri hiyo.

Pamoja na shukrani hizo, halmashauri ya wilaya ya Kasulu imetoa tuzo ya cheti kwa World Vision na kwa wadau wengine kutambua na kuthamini mchango wao katika mustakabari wa maendeleo ya kielimu kwenye halmashauri hiyo.

Sanjari na World Vision, wadau wengine waliotunukiwa vyeti wakati wa hafla hiyo ni shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR, IRC na Save the Children.
Wengine ni benki ya CRDB, benki ya NMB na wafanya biashara maarufu wa mjini Kasulu Andrew Mpanduji, Moshi Kimila, Dekas Mfunya na Peter Ntayandi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news