Kocha Robertinho:Muda wa mashangilio Simba SC unakuja

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam, licha ya kutoka sare ya bao moja dhidi ya Azam FC, Kocha mkuu, Roberto Oliviera (Robertinho) amewapongeza wachezaji kwa kupambana kutafuta alama tatu ingawa hawakufanikiwa.

Mtanange huo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara umepigwa jioni ya Februari 21, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Robertinho amesema, wamecheza vizuri, lakini bao la mapema kipindi cha kwanza liliwafanya kutoka kwenye mfumo uliowafanya kupoteza nafasi.

Pia Robertinho amesema, kipindi cha pili alibadili mfumo wa kuwaingiza washambuliaji watatu wenye kasi ili kuwafungua Azam ambao mara nyingi walikuwa nyuma mpaka wakafanikiwa kusawazisha.

“Kwanza nawapongeza wachezaji wangu, wamejitahidi kupambana kutafuta ushindi. Tulitamani kupata pointi zote tatu lakini lazima tukubali tulichojaaliwa na huu ndio mpira.

“Baada ya kuruhusu bao la mapema kipindi cha pili tulibadili mfumo na kutumia washambuliaji watatu ili kuongeza presha na kuwafanya Azam kufanya makosa.

“Tulimuingiza Jean Baleke, Habib Kyombo na Kibu Denis na kuwatoa Pape Sakho, Saido Ntibazonkiza na John Bocco ambao waliongeza kasi na tulibadili hali ya upepo na kupata bao la kusawazisha,” amesema Robertinho.

Robertinho amewapongeza mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu ingawa hawajapata matokeo ya kufurahisha huku akisisitiza muda wa furaha unakuja.

Post a Comment

0 Comments