SABABU KWA NINI MNAHIMIZWA KUVITAFUTIA VIWANJA NA NYUMBA ZENU HATI MILIKI HARAKA

NA BASHIR YAKUB

MAHAKAMA ya Rufaa katika Shauri la ardhi Na.35/2019 AMINA MAULID AMBALI na Wengine vs RAMADHANI JUMA inasema kuwa ;-

"ikiwa watu wawili au zaidi wanagombea ardhi moja, basi yule mwenye HATIMILIKI ndiye atayehesabika kuwa mmiliki halali".

Haya ni maneno ya majaji watatu wa Mahakama ya rufaa na yamenyooka sana.Jitahidi sana unaponunua kiwanja, nyumba, shamba kuhakikisha unakitafutia hatimiliki haraka.

Ile mikataba yenu mnayonunulia huko serikali za mitaa na kwingine sio hatimiliki, tumeshasema sana hili.

Pia kupimiwa ardhi pekee, ama kuwekewa vigingi pekee, ama kufanyiwa upimaji wa pamoja hasa wale wanaoletwa na serikali za mitaa na kukusanya hela za upimaji kutoka kwa wakazi wa eneo au mtaa husika sio hatimiliki.

Hayo juu yakifanywa wengi wenu hujua tayari mna hatimiliki tayari, hapana. Mtafute hatimiliki katika mamlaka za ardhi katika miji, manispaa, na halmashauri zenu.

Hatimiliki ni ulinzi tosha wa ardhi yako. Ukishaikamata hatimiliki mkononi hatokei wa kusema sijui uliuziwa eneo langu, sijui mpaka wako umeingia kwangu, sijui niliuziwa kabla yako nk.

Mnapotenga bajeti ya kununua kiwanja, nyumba, shamba tenga pia bajeti ya kutafuta hatimiliki ili viende kwa pamoja. Hili litakusaidia sana.

Ukiona kufanya hivyo ni ngumu ama kupoteza hela basi subiri mgogoro ambao ni mwepesi na haupotezi hela.

Nasisitiza tena, penye mgogoro mahakamani wa nani mmiliki halali mwenye hatimiliki anashinda mapema labda iwe vinginevyo.

Mwandishi wa makala haya, ndugu Bashir Yakub kitaaluma ni Wakili anapatikana kupitia simu +255714047241.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news