TUWAJIBIKE PAMOJA:Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema

NA LWAGA MWAMBANDE

FEBRUARI 10, 2023 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Emmanuel Tutuba alitajwa kuwa mtu sahihi wa kuongoza gurudumu la sekta ya benki nchini Tanzania.

Uongozi na wanachama wa umoja wa mabenki nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,Bw. Emmanuel Tutuba pamoja na Gavana mstaafu Prof.Florens Luoga hivi karibuni wakati wa usiku wa shukrani. (Picha na TBA).

Kauli hiyo ilitolewa katika hafla ya Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) wakati wa Usiku wa Kumshukuru Gavana aliyemaliza muda wake, Prof. Florens Luoga na Gavana Emmanuel Tutuba aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Prof. Luoga alisema, sekta ya benki iko chini ya usimamizi mzuri wa Gavana Tutuba. ''Ninaweza kuwahakikishia binafsi kwamba, Gavana Tutuba ndiye uteuzi ufaao zaidi, kwa bahati nzuri nimefanya naye kazi, najua uwezo wake, bidii, na ari yake ya kuona usimamizi mzuri wa uchumi na hasa sekta ya fedha''.

Aidha, licha ya kukiri mafanikio katika sekta ya benki, Gavana Tutuba alisisitiza kwamba mengi zaidi yanapaswa kufanywa ili kupunguza uwiano wa Mikopo Chechefu (Non-Performing Loans-NPL) na upatikanaji wa wateja kwa mikopo nafuu.

''Ni kweli kwamba tumefanikiwa kupunguza uwiano wa Mikopo Chchefu, lakini hatujapanda hadi kiwango kinachokubalika cha chini ya asilimia tano. Viwango vya mikopo bado viko juu, tushirikiane kuhakikisha wateja wetu wanapata mikopo nafuu,” alisema.

“Tumefanya vizuri kabisa katika ushirikishwaji wa fedha, lakini bado naona umuhimu wa kujikita katika kutengeneza bidhaa zinazomlenga mteja mbali na bidhaa za kibenki asilia tulizo nazo."

Ikumbukwe kuwa, mikopo chechefu (Non-Performing Loans-NPL) ni takwimu inayotumika kama kiashiria kinachoonesha uwiano kati ya mikopo isiyolipwa na jumla ya idadi ya mikopo ambayo imetolewa na benki au taasisi ya fedha.

Pia, Gavana Tutuba alikipongeza Chama cha Mabenki Tanzania kwa kuandaa mkakati wa miaka mitano (2023-2028) unaoweka Dira na Dhamira ya TBA katika kuongoza ajenda za kijamii,nchi ili kuimarisha uchumi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ushirikiano wa kutosha baina ya wadau wa sekta ya fedha nchini utaiwezesha Benki Kuu ya Tanzania,kutimiza jukumu la msingi la kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa. Endelea;


1.Wito sekta ya fedha, tuwajibike pamoja,
Sekta izidi ladha, iwavutie wateja,
Mambo hasi kwa orodha, hayo yazidi kuchuja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

2.Benki anaziambia, wakati ajenga hoja,
Hapo walipofikia, pazuri si pa kungoja,
Ni bora wakazidia, kuwajibika pamoja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

3.Hii mikopo chechefu, ni eneo linavuja,
Kiwango bado chakifu, na chaumiza wateja,
Ndivyo anawaarifu, kukipunguza ni haja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

4.Ni asilimia tano, hilo ni lengo taraja,
Iliko kukubwa mno, taratibu kunafuja,
Wala kusiwe miguno, kuishusha kazi moja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

5.Pia riba za mikopo, wanayopewa wateja,
Ziko juu kwa zilipo, kuzishusha ni faraja,
Na maendeleo yapo, kwa hatua moja moja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

6.Nondo zake anashusha, anao mwezi mmoja,
Anazidi kutukosha, jinsi anajenga hoja,
Alipo kweli atosha, tungoje mengi ya kuja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

7.Hii mikopo chechefu, ifike ifungwe hoja,
Vema kujua wasifu, kukopa wanaokuja,
Kupata ile harufu, wale watakaofuja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

8.Taarifa za mikopo, tayari zina wateja,
Benki popote mlipo, tumia bila kungoja,
Hizo taarifa zipo, ni wa kutumia kuja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

9.Vitambulisho vya NIDA, vitumike kwa pamoja,
Kutambulika si shida, mtu mmojammoja,
Ila kujificha shida, hata walio waseja,
Gavana wa Benki kuu, bwana Tutuba kasema.

10.Na benki wafanyakazi, kama wateja wakija,
Maombi fanyia kazi, bila ya kufujafuja,
Taarifa ziko wazi, kopesha palipo hoja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

11.Chechefu ikishashuka, toka benki moja moja,
Riba nazo zikashuka, kwa mikopo kwa wateja,
Uchumi utainuka, watu mmojammoja,
Gavana wa Benki Kuu, Bwana Tutuba kasema.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news