Wabunge wa Jubilee wasema wapo pamoja na Rais Ruto kuharakisha maendeleo ya wananchi

NA DIRAMAKINI

ZAIDI ya wabunge 30 wa Jubilee wameahidi kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kenya inayoongozwa na Rais wa Tano, Mheshimiwa William Samoei arap Ruto kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ili kuendeleza ajenda yake ya maendeleo.

Picha na Ikulu.

Wamesema ni wakati wa kuweka tofauti za kisiasa kando na kufanya kazi kwa ajili ya wananchi wa Jamhuri ya Kenya ambao wana shauku kubwa ya kuona Taifa lao linasonga mbele kiuchumi.

Hayo waliyabainisha Jumatano iliyopita walipokutana na Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua katika Ikulu ya Nairobi.

Rais alisema, ni jambo lisiloepukika kwa viongozi kufanya kazi pamoja, akibainisha kuwa "watu waliokuchagua ni watu wale wale waliotuchagua".

“Una haki ya kufanya uchaguzi, kwani Kenya ni nchi ya kidemokrasia. Ninyi sasa ni wanachama wetu na tutawatendea hivyo,” Rais alisema.

Alibainisha kuwa Bunge ni jukwaa muhimu la kutunga sheria kwenye ajenda za Serikali."Tutakuwa tukitafuta uungwaji mkono wenu kuhusu miswada na kanuni kuhusu Hazina ya Makazi, Mikataba ya Ununuzi wa Maji, miongoni mwa mengine," Rais Ruto alisema.

Kutokana na ukame unaoendelea, Rais alisema Serikali itaongeza upatikanaji wa chakula na maji kuanzia wiki hii nchini humo.

Wabunge hao waliongozwa na Mbunge wa Balambala, Omar Shurie, Mbunge wa Eldas, Adan Keynan na Seneta wa Isiolo, Fatuma Dullo. Walisema chama chao kina uhusiano wa karibu na Rais, na walichofanya ni "kurejea nyumbani".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news