Waziri Mkuu azitaka halmashauri zitekeleze miradi ya fedha za ndani

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi mingi ya huduma za jamii kila eneo hivyo watendaji wa halmashauri zote nchini wanatakiwa waendelee kubuni miradi mikubwa na kuitekeleza kwa kutumia fedha za makusanyo ya ndani badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa wilaya ya Songwe kwenye ukumbi wa Chuo cha Uuguzi Mwambani uliopo Mkwajuni mkoani Songwe, Februari 13, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejifunza mambo mengi ikiwemo miradi mingi ya halmashauri kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu. Watendaji wote wa halmashauri lazima wapanue wigo wa ukusanyaji mapato.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi wa umma waondoe urasimu katika kuwahudumia wananchi na badala yake wafanye kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu ili waweze kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao. “Hakikisheni mnawafuata katika maeneo yao na kutatua kero zao.”

Aliyasema hayo Februari 13, 2023 wakati akizungumza na watumishi, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Songwe akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Songwe. Amesema watendaji wahakikishe miradi inasimamiwa kikamilifu na kukamilika kwa wakati.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Songwe amchunguze mtumishi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Silas Meshilieki pamoja na fundi seremala Michael Bangu kwa tuhuma za kuchukua mbao zilizokamatwa na samani na kuzipeleka kwa fundi Bangu kinyume na taratibu za uhifadhi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini ambapo amewataka Wakaguzi wa Elimu kwenda kufanya ukaguzi katika shule na kujionea wanachofundishwa na kujifunza ikiwa ni pamoja na kukagua vitabu vinavyotumika. “Baadhi ya vitabu vina mafundisho ya ajabu hayaendani na mila na desturi za Kitanzania.”

Hivi karibu akizungumza na Shirikisho na Elimu ya Juu (TAHILISO) na Zanzibar (ZAHLIFE) Mheshimiwa Rais Dkt. Samia aliwataka vijana hao kuwalinda watoto wa Kitanzania dhidi ya mila, tamaduni na desturi zisizo Kitanzania.

“Walindeni wadogo zenu vinginevyo mtakuja kuwa na Taifa la ajabu, huko tunakotembea nje mambo sio shwari, tuishini kwa mila na desturi zetu, mambo ya kuletewa yapo ya kuiga, suti zimetoka nje tunavaa tunapendeza, unataka kusema kizungu cha kubana pua sema, lakini yale mengine acha."

Naye, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde alisema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anataka matokeo chanya katika utendaji na ana imani kubwa na watumishi wa umma, hivyo wafanye kazi kwa bidii ili wasimuangushe. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alisema tayari Serikali imeshakamilisha usanifu wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Mbalizi-Changombe-Mkwajuni-Saza-Patamela-Makongorosi yenye urefu wa kilomita 118 na kuwataka waendelee kuwa na subira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news