Wizara ya Ardhi yazidi kuiheshimisha Sekta Binafsi

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula amesema, kwa sasa mwelekeo wa wizara hiyo ni kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza kazi na majukumu mbalimbali.

Mheshimiwa Dkt.Mabula amesema,hivi karibuni,wizara imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa Uimarishaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (Land Tenure Improvement Program (LTIP) ambao utaihusisha sekta binafsi wakati wa utekelezaji wake.

Ameyasema hayo Februari 14, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Wadau wa Sekta ya Ardhi nchini katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa pili, umeongozwa na kauli mbiu ya "Usimamizi bora wa ardhi kwa maendeleo endelevu ya biashara na Uwekezaji nchini".

Waziri Dkt.Mabula amesema, mradi huu utaimarisha miundombinu muhimu ya wizara,mifumo kazi, utoaji wa hati milki, hati za hakimiliki za kimila na uandaaji wa mipango ya matumizi.

Pia amesema, baadhi ya kazi zitakazotekelezwa na mradi huu ni kujenga ofisi za ardhi za mikoa 25,kusambaza mfumo wa ILMIS kwenye mikoa 25 na halmashauri 41.

Sambamba na kuandaa mfumo wa taarifa za uthamini ikiwemo kutoa Hati Milki 1,000,000 pamoja na leseni za makazi 1,000,000 nchini.

"Jambo lingine ni kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 250 pamoja na mipangokina ya vijiji hivyo, kwa hiyo, mradi huu mkubwa kama nilivyoeleza tutashirikiana kikamilifu na sekta binafsi katika utekelezaji wake,"amefafanua Waziri Dkt.Mabula.

Wakati huo huo,Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema kuwa,suala linalohusu sekta ya uendelezaji milki nalo katika mkutano wa awali uliofanyika Mei 23, 2022 lilijadiliwa kwa kina na kutolewa mapendekezo.

"Napenda kuwafahamisha kuwa wizara ilifanya mkutano Septemba 2, 2022 katika Ukumbi wa Kisenga Millennium Tower jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya majadiliano na wadau wa Sekta ya Milki.

"Katika mkutano huo, wizara ilipokea maoni na mapendekezo ya kuboresha mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Milki nchini kama vile Serikali kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na mifumo ya kutoa maamuzi kwani imekuwa ni kikwazo,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Aidha, amesema suala lingine ni benki kurejea suala la riba na taratibu za kutoa mikopo, sekta binafsi kuwa wabunifu na kuzingatia sera, sheria na taratibu.

Sambamba na kuzuia vitendo vya ukiukwaji wa maadili (rushwa) vinavyochangia kwa kiasi kikubwa kudumaza Sekta ya Milki kuweka mfumo mahsusi wa kuwezesha mawasiliano kwa wakati ili changamoto zinazojitokeza zitatuliwe kwa wakati.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, mkutano huo wa Ministerial Public Private Dialogue (MPPD) ni wa pili toka ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukutana na wadau wa Sekta ya Ardhi ndani ya mfumo wa majadiliano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).

Amesema, mkutano huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,ambayo aliyatoa kwenye Mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Juni 7,2022.

Zanzibar

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Mheshimiwa Juma Makungu Juma, ameishukuru wizara kwa kuwapa mwaliko kuja kujifunza na kutoa mchango wao katika mkutano huo muhimu nchini.
"Ushirikiano huu unapaswa kuendelezwa kwa sababu tunajenga nchi moja na maendeleo ni ya Watanzania wote unapozungumza Jamhuri ya Muungano unazungumzia Tanzania Bara na Zanzibar, kwa hiyo mwaliko huu ni jambo muhimu. Tutajifunza kutoka kwa wadau hapa na kwenda kuyafanyia kazi, kwani changamoto tulizonazo zinafanana sana,"amefafanua Mheshimiwa Juma.

Amefafanua kuwa, Sekta ya Ardhi ni muhimu kwa kuwa, hauna uwekezaji,kama hauna ardhi. "Kwa hiyo tutumie fursa hii vyema kwa ajili ya kuijenga Tanzania yetu,"amebainisha Mheshimiwa Juma.

Sekta Binafsi

Naye Dkt.Samuel Nyantahe akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa na ushirikiano mzuri katika masuala mbalimbali nchini.

"Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa na ushirikiano mzuri sana kwa masuala mbalimbali. Ninashukuru katika mkutano wa kwanza uliofanyika nilihudhuria, mambo mengi yaliulizwa na kwa kweli Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inafanya kazi kubwa sana na nzuri kwa ajili ya Watanzania.

"Tunamshukuru Waziri (Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula) kwa kazi nzuri,jambo la muhimu sana ni ule ushirikiano ambao umeoneshwa kwa maneno na vitendo unatuwezesha sana kuwa pamoja katika kuijenga nchi yetu.

"Naomba ushirikiano huu uwepo kama ambavyo unafanyika hivi sasa na sio wakati wa vikao tu, hapo kati kati tuwe na mawasiliano na kupeana mrejesho kwa kila hatua muhimu kutoka wizarani uwe na tija,"amefafanua Dkt.Nyantahe.

Mrejesho

Akiwasilisha wasilisho kuhusu utekelezaji wa hoja za wadau ambazo zilitolewa katika mkutano wa Mei 23, 2022 Mkurugenzi wa Milki Kuu,Lucy Kabyemela amesema, jumla ya wadau 53 walitoa maoni na ushauri na kuuliza maswali ambayo kimsingi yalijikita kwenye hoja 15.

Mkurugenzi huyo alisema hoja zote walizipokea na kuzifanyia kazi na hoja zingine zilihitaji ufafanuzi na taarifa ya utekelezaji ambapo wameambatanisha katika Bangokitita.

"Hoja ya kwanza ilihusu urasimishaji na waliotoa maoni yaliyohusu wananchi kutolipia gharama za urasimishaji kwa kampuni zinazotekeleza kazi hiyo, wengine walishauri uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe kwa kampuni ambazo hazikukamilisha kazi ya urasimishaji na kwamba wizara imetoa ahadi ya kuwawezesha wananchi kuhusu gharama za urasimishaji kwa kushirikiana na Benki ya NMB, lakini ahadi hiyo wanaona ni kama haikutekelezwa.

"Kuhusu suala la urasimishaji kumekuwa na mwitikio hafifu wa wananchi kulipia gharama za urasimishaji na baadhi zikisababishwa na baadhi ya kampuni kutokamilisha zoezi hilo kwa wakati na hivyo kuvunja imani kwa wananchi wanaofanyiwa hizo kazi.

"Wizara imechukua hatua ambapo Januari 6,2023 wizara ilifanya kikao pamoja na kampuni za urasimishaji na kuhusisha mamlaka za upangaji za Mkoa wa Dar es Salaam, kikao hicho kilipelekea kuandaa mwongozo wa kukwamua hizi kazi ambazo zimekwama na ambazo zimeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Mwongozo huo na mkakati huo utatumika katika mikoa mingine. Vilevike wizara imefanya uhakiki wa kampuni za urasimishaji na kuchukua hatua kama ambavyo baadhi wameshauri hasa zile kampuni ambazo hazijafanya kazi vizuri kwa kuzisimamisha kufanya kazi mpya mpaka pale zitakapokamilisha kazi za awali,"amefafanua.

Mkurugenzi wa Milki Kuu amefafanua kuwa,jumla ya kampuni 15 kati yake saba zikiwa za upanga na nane za upimaji zimekabidhiwa kwenye vyombo vya uchunguzi kwa kosa la kuchukua fedha za wananchi bila kukamilisha kazi.

Pia amesema,kuna kampuni 10 zilichukuliwa hatua na mamlaka za upangaji kwa kukiuka taratibu za kimkataba.
 
"Kuhusu utaratibu uliowekwa na wizara kuwezesha wananchi kumudu gharama za urasimishaji kupitia NMB tukiri kwamba hili lilitekelezwa na mradi wa mfano ulishirikisha NMB ulifanyika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya wananchi walikosa vigezo vinavyotakiwa na benki,"amebainisha.

Hoja ya pili amesema, inahusu gharama za huduma za ardhi. "Na hapa wengi walidai gharama kuwa ni kubwa zipunguzwe, lakini pia uwepo utaratibu wa kulipia gaharama hizi mara moja mtu anapofanya upimaji zitolewe mara moja badala leo unalipia hiki na kesho unalipia hiki, pia kulikuwa na hoja inashauri kwamba huduma hizi za upimaji na upangaji zitolewe bure, lakini wananchi wapewe fursa ya kulipia kodi ya pango ya ardhi ambayo inalipiwa kila mwaka.

"Kuna ushauri ulitolewa kuhusu gharama kubwa za usajili wa rehani hususani vijijini ambako tunatoa hati milki za kimila kwamba ni kubwa kulingana na kipato cha wananchi wa vijijini, hili nalo limefanyiwa kazi, kwani wizara imekuwa ikifanya mapitio mara kwa mara ya tozo ambazo zinatozwa na Serikali kwa ajili ya umilikishaji mathalani malipo ya mbele.

"Ambayo ilikuwa ikitozwa kabla ya mwaka 2021/2022 ilikuwa ikitozwa kwa asilimia 2.5, lakini imeshuka hadi 0.5 lakini vile vile bado Wizara inaendelea kufanya marejeo ya taratibu ya tozo hizi ili kutoa unafuuu kwa wananchi,"amefafanua.

Ameongeza kuwa,wizara pia imekuwa ikirejea viwango kila baada ya miaka mitatu na sasa hivi wanapokea maoni ya wadau.

"Kuhusu gharama za miamala hususani hati za kimila kabla ya mwaka 2021 ni kweli gharama hizi zilikuwa zinatozwa zikizingatia gharama zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 kwa maana ya hati milki za mjini, lakini mwaka 2021 ziliandaliwa kanuni za gharama za miamala yote za kimila na rehani sasa hivi gharama hizo zimepungua tofauti na gharama za awali.

"Hoja nyingine ilihusu mabaraza ya ardhi ya nyumba na hapa ilionekana yamekuwa sehemu ya vyanzo vya migogoro ya ardhi kwa kutoa maamuzi kwa wasio husika hususani kwenye maeneo ambayo yanamilikiwa na watu wana hati miliki, lakini pia kulikuwa na mapendekezo ya kuimarisha mabaraza haya hasa wilaya ya pembezoni kwa kupatiwa wenyeviti.

"Kimsingi mabaraza ya ardhi na nyumba yanaongozwa na Sheria ya Mahakama za Ardhi sura namba 216 na haya yamepewa uhuru wa kufanya kazi kama mahakama katika kutekeleza majukumu yake, lakini kwa mwananchi yeyote ambaye haridhiki na maamuzi ya mahakama ya nyumba na ardhi sheria hii imetoa haki ya kuomba ama marejeo ama kukata rufaa kwenye mahakama ya juu. Na kama kuna jambo lolote linatekelezwa kinyume sheria imetoa nafasi ya kuomba marejeo ama rufaa.

"Serikali pia imefanyia kazi hoja ya kuimarisha mabaraza kwa kuongeza wenyeviti na wenyeviti waliopo wameongezewa maeneo ili wananchi wote wapate huduma,"alifafanua Mkurugenzi huyo ikiwa ni sehemu ya hoja na maoni yaliyoibuliwa na wadau awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news