Wizara yatoa ufafanuzi kuhusu Uwanja wa Benjamin Mkapa

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa ufafanuzi kuhusu picha na taarifa zinazosambaa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari 'Uwanja wa Mkapa Unaanza kutia Aibu'.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 5, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, John Mapepele imebainisha kuwa, picha zinazotumika pamoja na ujumbe huo ni zile ambazo zilichukuliwa siku ya nyuma mara baada ya tukio la Mkesha lililofanyika 16/12/20 katika uwanja huo.

"Kufuatia hali hiyo iliyojitkeza wakati huo, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ilichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kuwa, hali hiyo haijitokezi tena kama ifuatavyo,

"Mosi, wizara ilifanya mabadiliko ya Menejimenti ya Uendeshaji wa uwanja huo, pili wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi ambayo ndiyo mdau mkubwa imeandaa muongozo wa matumizi wenye lengo la kudhibiti masuala ya usafi.

"Tatu, wizara imeunda kikosi kazi kidogo cha usafi na mazingira ambacho kinafanya ukaguzi wake kabla na baada ya uwanja kutumika ili kuimarisha usafi na nne wizara ilimuelekeza mzabuni wa uwanja huo kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vibarua wa usafi wakati wa matukio,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara imetoa rai kwa wadu wa michezo na umma wote wa Watanzania kushirikiana kwatika kuvitunza viwanja vyote kwa kuzingatia usafi wakati wa matumizi yake na kujiepusha na aina yoyote ya uharibifu.

Historia ndogo

Julai 29, 2020 Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Hayati Dkt.John Pombe Magufuli aliutangaza rasmi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwa ni Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa (Benjamin Mkapa Stadium) ili kuendelea kumuenzi Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa.

Hayati Dkt.Magufuli alitoa tamko hilo katika hafla ya kuaga mwili wa Hayati Benjamin William Mkapa iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo alisisitiza Mzee Mkapa alikuwa na mchango mkubwa katika sekta ya michezo nchini hivyo taifa linapaswa kumuenzi.

“Mzee Mkapa aliujenga uwanja mkubwa wa michezo na alikua hapendi vitu viitwe kwa jina lake, lakini kwa kuwa kwa sasa amelala na hawezi kuniadhibu na kwa kuwa nimepokea meseji nyingi nimekubali na sasa natamka rasmi uwanja ule uitwe Mkapa Stadium,”alibainisha Rais Dkt.Magufuli wakati wa uhai wake.

Pia Dkt.Magufuli aliongeza kuwa, katika michezo Mzee Mkapa alikuwa anapenda sana michezo ndio maana alifanya mambo mengi sana katika sekta hiyo,vile vile alikuwa ni shabiki wa timu ya Yanga japo hakuwahi kuonesha hadharani hivyo tunapaswa kumkumbuka na kutunza kumbukumbu hizo.

Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (Mkapa Stadium) ni miongoni mwa viwanja vikubwa barani Afrika ambavyo vimekidhi vigezo vyote vilivyoanishwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na una uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 kwa wakati mmoja.

Aidha, uwanja huo wa kisasa upo Kata ya Miburani ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na ulifunguliwa mwaka 2007 na ulijengwa karibu na Uwanja wa Uhuru, uwanja wa zamani wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news