ZMBF yatekeleza kwa vitendo Sera ya Uchumi wa Buluu

NA DIRAMAKINI

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi amesema taasisi hiyo inatekeleza kwa vitendo Sera ya Uchumi wa Buluu ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi (katikati) alipokuwa akizungumza na viongozi wa ngazi ya Taifa UVCCM waliofika kujitambulisha katika ofisi ya Taasisi hiyo Migombani jijiji Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa,Rehema Omary Sombi.

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo hivi karibuni kwenye ofisi za taasisi hiyo, Migombani Wilaya ya Mjini alipozungumza na ugeni kutoka jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) waliofika kumtembelea.

Alisema, tangu kusajiliwa kwa ZMBF, Febuari 19, mwaka jana ambayo kwa sasa imetimiza mwaka mmoja, wanajivunia mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Sera za Serikali kwa vitendo hasa Sera ya Uchumi wa Buluu.

Mama Mariam Mwinyi alisema, dhana ya Uchumi wa Buluu kwa taasisi ya ZMBF imejikita kwenye harakati za kuwasaidia na kuunga mkono juhudi za kinamama wanaojitoa kupigania maendeleo ya kiuchumi kupitia matunda ya baharini.

Alisema, ZMBF imefanikiwa kuwafikia kinamama wengi Unguja na Pemba wanaujishughulisha na kilimo cha mwani na kueleza asilimia 90 ya ukulima huo hushirikisha kinamama.

Alisema katika jitihada za kuwaunga mkono, ZMBF imewasaidia vifaa mbalimbali vya uvuvi kinamama hao ikiwemo boti zenye mashine, viatu vya kuvalia baharini, mashine za kusagia mwani zenye uwezo wa kusaga mwani mwingi kwa wakati, hali iliyowasaidia kinamama hao kuongeza ufanisi wa kazi zao na kuwaongezea kipato kwa kukabiliana vyema na soko la bidhaa hiyo.

“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, siku hizi kinamama hufanya shughuli za kilimo cha mwani nje kidogo na usawa wa bahari kutokana na kina cha maji ya bahari wanayolimia tofauti na zamani walilima maeneo karibu hivyo, ZMBF imeona haja ya kuwasaidia vifaa kimama hao, hususani boti zenye mashine kwa ajili ya kuvulia na shughuli zao za baharini pamoja na viatu kwa usalama wanapokua baharini,”alifafanua Mama Mariam.

Mama Mariam ambaye pia ni Mlezi wa Matembezi ya UVCCM ya Mapinduzi ya Zanzibar aliwaeleza vijana hao kwamba pia ZMBF imejita kwenye harakati za utunzaji mazingira kwa kuishajihisha jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha usafi.

Alisema katika harakati hizo, ZMBF inajishughulisha na utengenezaji wa taulo za kike za kufua na kuhifadhi baada ya matumizi, ambazo huwasaidia wasichana shuleni hasa wale wanaotoka kwenye mazingira magumu ambao hawana uwezo wa kuhimili taulo za kawaida.

Aidha, alieleza taulo za kawaida ambazo hutupwa baada ya matumizi huchangia wimbi la uchafuzi wa mazingira na kueleza kwama nyingi husalia kutupwa baharini na kuathiri viumbe vya bahari.

Akizungumzia tatizo la magojwa yasiyoambukiza yanayoendelea kuiathiri jamii, Mama Mariam Mwinyi alieleza ZMBF imekua ikishajihisha jamii kufanya mazoezi na kuambatana nao kwenye makongamano mbalimbali yanayohusisha matembezi ya hiari ambayo husaidia jamii kufanya mazoezi ili kujiepusha na kujinginga na maradhi hayo yakiwemo, presha, kisukari matatizo ya moyo na saratani.

Kuhusu suala la udhalilishaji wa kijinsia, alieleza ZMBF inakerwa zaidi na vitendo hivyo ambavyo huwaathiri zaidi wanawake na watoto, alisema licha ya harakati nyingi zinazofanya na taasisi hiyo kwa kuwagusa moja kwa moja kinamama, vijana, wasichana na Watoto suala la udhalilishaji wamekua wakilikemea kwa nguvu zote na kulipiga vita.

Katika hatua nyingine Mlezi huyo wa UVCCM aligusia matayarisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwataka vijana hao kufanya maandalizi ya aina yake, kwani vijana ni sauti ya chama hasa kwenye kuimarisha mustakabali wa maendeleo na mabadiliko kwenye nyanja zote za siasa, uchumi na jamii.

“Kuna haja ya kukaa chini na kufikiria namna kutakavyoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yawe ya aina yake, muje na fikra tofauti, UVCCM ije na kitu tofauti sababu vijana ndio injini ya Chama” aliwashajihisha vijana hao.

Naye Makamu Mwenyekiti UVCCM Taifa,Rehema Sombi Omari (MNEC) kwa niaba ya ugeni alioambatana nao, waliipongeza ZMBF kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa kwa kipindi cha muda mfupi pia waliahidi kuwa balozi wazuri wa kukitangaza chama na kupaza sauti zao kwa umma kuyasemea mazuri yote yanayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt.Hussen Ali Mwinyi na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi imara wa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Akilizungumzia jengo la UVCCM, ofisi ya Jimkana, Zanzibar alisema wanatarajia kulifanyia maboresho makubwa ili kuweka alama kwa vizazi vijavyo kwamba UVCCM 2022-2077 ilifanya makubwa wakati wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news