Ajali ya basi la Sheraton yaua saba, yajeruhi 10 mkoani Geita

NA MWANDISHI WETU

WATU saba wamefariki dunia na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa katika ajali ya basi la abiria la Kampuni ya Sheraton lenye namba za usajili T922 ADC iliyotokea katika Kijiji cha Mwilima kata ya Kasamwa wilayani Geita mkoani.

Kwa mujibu wa Mwangaza TV, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Kamishina Msaidizi wa Polisi, ACP Berthaneema Mlay akiwa katika eneo la ajali amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Amesema, ajali imetokea leo Machi 7, 2023 majira ya saa 10:30 jioni na chanzo cha ajali ni kupasuka kwa tairi la mbele la basi hilo.

Kamanda ACP Berthaneema Mlay amesema, basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kuelekea Ushirombo mkoani Geita ambapo dereva alipoteza ustahimilivu baada ya tairi la mbele kupasuka na basi kutumbukia darajani.

Ameeleza kuwa, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Hayo yanajiri ikiwa ni siku moja baada ya ajali nyingine kutokea na kuua watu tisa na wengine 30 kujeruhiwa mkoani Katavi.

Ni kutokana na ajali iliyotokea katika Mlima mkali wa Nkondwe, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi baada ya basi (Tata) lenye namba za usajili T506 DHH kampuni ya Komba's kupinduka na kudondokea bondeni.

Taarifa ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Dkt.Alex Mrema imesema vifo hivyo tisa vimetokea papo hapo ambapo kati ya waliofariki wanaume ni watano kati yao watu watu ni wawili na watoto watatu na wanawake ni wanne akiwemo mjamzito.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame amesema ajali hiyo imetokea Machi 6, 2023 jioni. “Baada ya kufika katika Mlima huo gari liliserereka na kudondokea kwenye bonde kubwa lenye kina cha mita zisizopungua 75.”

Amesema, hadi sasa chanzo cha ajali hakijajulikana na Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na uchunguzi huku zoezi la kuitambua miili likiendela kwa ajili ya taratibu nyingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news