Hotuba ya Rais wa UMMT Dkt. Nabiijoshua yagusa wengi nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT), Dkt.Nabiijoshua Aram Mwanyala ameupongeza umoja huo mkoani Kilimanjaro kwa kuendesha kongamano kubwa la kuombea Taifa na umoja wao.

Dkt.Nabiijoshua ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania iliyopo mjini Morogoro amesema, kongamano la hivi karibuni limekuwa la baraka kubwa.

"Amani iwe nanyi Mitume na Manabii wote nchini Tanzania na asante sana Baba yetu mpendwa Dkt.Dustan Haule Maboya,umetuonyesha upendo halisi wa Mungu usiotikisika kama mlima Sayuni.Umekataa kata kata kufa na upako wako kama Nabii Elisha wa wakati wa ule Namani

"Badala yake umetangaza rehema juu ya uzao wa Ghazi yaani sisi tusiangamizwe kabisa kusudi ni kuzuia zile nyakati za giza kuu ulizopitia wewe na wazee wenzako wa injili zisijirudie tena juu ya uso wa nchi yetu njema ya Tanzania

"Umekuwa kama chemichemi ya maji ya uzima kwa mti ambao mbegu yake iliangukia jangwani au kama Ishimaili wa Hajili mtoto wa mjakazi kule jangwani alipotupwa na kuwa hana urithi katika nyumba ya Baba yake aliyemzaa

"Umetuchimbia kisima kipya kama Isaka baada ya vile vya urithi kugombaniwa hakika sasa tutastawi katika nchi na Wafalme wamefanya agano la amani pamoja nasi.

"Umejinyenyekeza sana mbele za Mungu wako hadi umefika mavumbini walipotupwa watoto wakataliwao wa kizazi ulichokiita wewe mwenyewe ni kizazi cha nne hiki. Kizazi kilichopata kuishi wakati wa Farao asiye mjua Yusufu na kuteswa mengi na wasimamizi wao.

"Lakini wewe umefanyika Musa mbele ya wazee wenzako wenye hekima, hatimaye mmetukusanya turudi katika nchi yetu ya asili ya umoja wa kanisa bila ubaguzi wala matengano.Mungu awabariki sana wazee wetu wote kwa upendo wenu na uvumilivi mwingi kwetu,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.

Wakati huo huo,Dkt.Nabiijoshua amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uongozi thabiti ambao umeendelea kuwaunganisha kwa pamoja Watanzania.

"Ndugu Mitume na Manabii, naomba kwa umuhimu kabisa, kwa niaba yenu nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwani chini ya uongozi wa Serikali yake kila tabaka la jamii yetu kubwa ya Watanzania zaidi ya milioni sitini kote nchini wana mashangilio ya namna yao.

"Vyama vya siasa vinashangilia,wafanyakazi wanashangilia,wafanyabiashara wanashangilia,watu wa makundi maalumu wakiwemo walemavu wanashangilia,wavuvi,wakulima,wachimba madini,wanafunzi wa shule za msingi hadi kidato cha sita, wanafunzi wa vyuo vikuu,madhehebu ya dini hadi machifu na wengineo wote wanashangilia, yaani Mama ameligeuza Taifa lote kuwa la mashangilio, watu wanaifurahia nchi yao wenyewe, asante sana Mama.

"Mama unafanana na mvua ikiinyeshea nchi kila mmea hustawi na kutoa maua ya mashangilio tayari kwa kuzaa matumda.

"Japo najua mvua huotesha hata miba ikakuchoma,na wakati mwingine husababisha utelezi tunakuombea usianguke Taifa lote lipo upande wako kukutegemeza Mama yetu mwema, usirudi nyuma tunakuomba sana.Mama umefanana na jua wakati wa mavuno humpa kila mtu matumaini ya kuvuna alichopanda.

"Unafananishwa na kila kitu chema vitaijaza Dunia nikiviandika vyote itoshe kusema umekuja na kutokea kama mwanga gizani, umeangaza umeijua siri ya furaha ya Taifa lako.

"Umekuwa kama merikebu ya Nuhu inayompa salama kila mwenye hekima ya kuijua kesho yake, Mungu akubariki sana Mama yetu mwema.

"Kwa kuwa hii ni wiki ya Wanawake Duniani tunakuombea kwamba kupitia wiki hii MWENYEZI MUNGU aifanye nyota yako izuke tokea Chamwino Dodoma imulike kuwakilisha wanawake wote ulimwengu mzima na taa yako isizimike usiku wakuu wote wa Dunia na waseme Amina,"amefafanua Dkt.Nabiijoshua.

Mbali na hayo, Dkt.Nabiijoshua amewaomba mitume na manabii kwa umoja wao wasikubali kurundi nyuma juu ya safari yao ya mashangilio ifikapo Aprili Mosi, mwaka hii katika Ukumbu wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

"Wenyeviti wetu wa mikoa na wilaya zote nchini nawaomba fanyeni yote hata yasiyowezekana kwa wanadamu ili mfike kwenye kongamano hilo la mashangilio, kwa njia hiyo pekee tutakuwa tumevuka kikwazo cha mwisho kilichowakwamisha waliotutangulia kabla yetu.Nawatakia Upendo, Amani, Furaha na Umoja asanteni sana,"amefafanua Dkt.Nabiijoshua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news