Kamati ya Bunge yaguswa na ufanisi wa TCAA, TAA, ATCL na KADCO

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na utekelezaji na usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na mamlaka za usafiri wa anga nchini ikiwemo zile za udhibiti,uangalizi,watumiaji na waandaaji wa miundombinu ya usafiri wa anga nchini licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe, Seleman Kakoso ameyasema hayo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Serikali iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo taasisi za TCAA, TAA, ATCL na KADCO ziliielezea kamati utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kisekta na maendeleo ya sekta ya usafirishaji kwa njia ya anga nchini.

“Kamati imesikia mipango ya sasa,baadae na kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa faida ya sekta ya usafirishaji kwa njia ya anga nchini kama vile ufungaji wa rada mpya nne, maeneo ya Dar es Salaam, Kilimanjaro ,Mwanza na Songwe, ufungaji wa mtambo mkubwa wa kuwezesha ndege kutua kwa usalama, Maboresho ya uendeshaji kibiashara kwenye viwanja vya ndege na ongezeko la safari za ndege nchini," amesisitiza Mhe.Kakoso.

Akijibu hoja za wajumbe wa kamati, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya maboresho ya sekta ya anga nchini kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege nchini, ununuzi wa rada na ndege mpya.

Aidha, Waziri Mbarawa ameongeza kwa kusema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia, Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa zile taasisi ambazo zina uwezo wa kuzalisha na kuajiri ziajiri moja kwa moja hivyo utaratibu mzuri utakuja na changamoto hii itapungua kwenye taasisi zote.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini, Daniel Malanga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi na maboresho ya miundombinu mbalimbali kwa mustakabali wa maendeleo ya usafiri na usafirishaji kwa njia ya anga nchini,

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inaendelea na ziara zake za kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa 11 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Aprili 4,2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news