MAC yafanyika jijini Bujumbura, Magavana Benki Kuu wakubaliana

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Jamhuri ya Burundi, Dieudonné Murengerantwari ameongoza Mkutano wa 26 wa kawaida wa Kamati ya Masuala ya Fedha ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki-EAC (Monetary Affairs Committee (MAC).

Picha na BankiNkuru.

Murengerantwari ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa MAC aliongoza mkutano huo ambao umefanyika Machi 17, 2023 ana kwa ana kwa mara ya kwanza jijini Bujumbura, Burundi tangu mwaka 2019. Mikutano iliyofuata 2020, 2021 na 2022 ilifanyika kwa njia ya mtandao kutokana na vikwazo vya UVIKO-19.

Miongoni mwa walioshiriki katika mkutano huo ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya,Patrick Njoroge, Gavana wa Benki Kuu ya Rwanda, John Rwangombwa.

Wengine ni Gavana wa Benki Kuu ya Sudan Kusini,Johnny Ohisa Damian na Mkurugenzi Mtendaji, Utafiti na Uchambuzi wa Kiuchumi, Benki Kuu ya Uganda, Adam Mugume ambaye aliiwakilisha Benki ya Uganda.

Aidha,Marie Malangu Kabedi Mbuyi ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hakuweza kushiriki katika mkutano huo, badala yake aliomba hudhuru.

Mkutano huo ulifanyika huku kukiwa na hali ya shinikizo la kuendelea kwa mfumuko wa bei, kuimarisha hali ya kifedha,changamoto za kiuchumi ambazo zinachochewa na vita vya Ukraine, hali mbaya ya hewa na hatari nyingine zinazojitokeza.

Kamati ilibaini kuwa, ufanisi wa kiuchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki mwaka 2022 uliendelea kuwa imara, na kurekodi ukuaji wa Pato la Taifa kwa asilimia 4.5.

Pia,utendaji huo uliungwa mkono na ukuaji mkubwa katika sekta ya viwanda na huduma kufuatia kupunguzwa kwa vikwazo vinavyohusiana na UVIKO-19, kupunguza vikwazo vya ugavi duniani na kuendelea kwa shughuli mbalimbali za uwekezaji.

Kamati pia ilibainisha kuwa, ukuaji katika kanda unatarajiwa kuimarika kutokana na kuimarika kwa shughuli za kilimo, kuendelea kwa ufanisi katika sekta ya huduma, na sera makini za fedha.

Wakati huo huo, ukuaji dhaifu wa kiuchumi kimataifa, mzunguko duni wa kifedha duniani, mivutano ya muda mrefu ya kijiografia, hatari ya mabadiliko ya hali ya hewa na bei tete za bidhaa zimeonekana kuwa na matokeo hasi.

Kamati pia ilibaini kuwa, Benki Kuu nyingi za nchi wanachama hivi karibuni zimekaza sera zao ili kukabiliana na shinikizo la mfumuko wa bei.

Mbali na hayo, kikao hicho kilipitia hali ya utekelezaji wa hatua zilizokubaliwa hapo awali kuhusu uanzishwaji wa Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki (EAMU), kwa kuzingatia maamuzi ya Mkutano wa 25 wa Kawaida wa MAC uliofanyika Machi 2022. Kamati pia ilitafakari hatua iliyofikiwa kuelekea kuanzishwa kwa Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki.

Kamati ilibaini kuwa, Benki Kuu za nchi wanachama zimepiga hatua kubwa katika uanzishaji wa taasisi muhimu za Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki (EAMU), hususani Taasisi ya Fedha ya Afrika Mashariki (EAMI), kuoanisha sera za fedha na viwango vya ubadilishaji, kuoanisha mifumo ya udhibiti, utekelezaji wa hatua za kuimarisha mifumo ya malipo ya kikanda, uboreshaji wa mifumo ya usalama wa mtandao, kujenga uwezo katika Kupambana na Utakatishaji wa Pesa/Kupambana na Ufadhili wa Ugaidi (AML/CFT) na Usimamizi wa Hatari kwa Benki Kuu za nchi wanachama na kukuza malipo ya mipakani.

Aidha, kamati ilisisitiza dhamira yao ya kufanya kazi pamoja na Sekretarieti ya EAC kuharakisha utekelezaji wa shughuli za Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki (EAMU).

Kamati ilibaini kuwa, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika eneo la mifumo ya malipo ya mipakani na kukubaliana kuendelea kutekeleza mipango ya muingiliano katika ngazi ya kitaifa, kuimarisha Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS), huku ikishirikisha wadau wengine katika Bara la Afrika katika ujumuishaji zaidi wa mifumo ya malipo ya mipakani.

Magavana walitia saini Nyongeza ya Mkataba wa MOU kuhusu ubadilishaji wa sarafu ili kuzingatia masuala ya AML/CFT katika eneo hilo.

Kutiwa saini kwa nyongeza hii ya Mkataba wa Maelewano ni mafanikio muhimu katika mchakato wa kuimarisha miamala katika eneo zima kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha.

Magavana hao walitumia fursa hiyo kuwakaribisha Gavana wa Benki ya Banque de la République du Burundi, Gavana wa Benki ya Sudan Kusini na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania waliokuwa wakihudhuria mkutano wa MAC kwa mara ya kwanza tangu wateuliwe katika majukumu yao na kuwatakia kila la heri katika majukumu yao.

Katika hatua nyingine,Magavana walimshukuru Gavana wa Benki ya Jamhuri ya Burundi kwa kuandaa na kuongoza mkutano wa 26 wa MAC na kwa ukarimu waliopewa Magavana na wajumbe wa nchi wanachama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news