Makamu wa Rais Dkt.Mpango akemea mapenzi ya jinsia moja

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwalea watoto na vijana kwa kuzingatia maadili ya kitanzania pamoja na kuongeza umakini katika maudhui yanayooneshwa katika Televisheni.

Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati akiongea na waumini wa Kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma baada ya kushiriki Ibada ya kawaida ya katikati ya wiki katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani kijijini hapo ambapo.
 
Amesema, kumekuwepo na mmomonyoko wa maadili ikiwemo ndoa za jinsia moja ambazo hazipo hata kwa Wanyama hivyo Wazazi waangalie watoto na vijana wanaangalia nini ili kuondokana na kuwa na Taifa la ajabu.

“Hili ni gumu kweli, maadili ya Nchi yetu yameporomoka sana, yaani na mengine hata kuyasema ni ngumu, ndoa za Wanaume wawili? Ndoa za wanawake wawili? mliziona wapi? Hata wanyama hawafanyi hivi,”amebainisha.

Kwa upande mwingine, Dkt. Mpango amewaasa wananchi wa Kasumo na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla kutoa ushirikiano wakati huu ambapo Serikali inafanya ujenzi wa miundombinu ya Barabara katika Mkoa huo ambao ni nyenzo muhimu kwa biashara na urahisi wa kufikia huduma za jamii kama vile Hospitali na Shule na kuzingatia pia kuwapa Wawekezaji ushirikiano ikiwemo kuzingatia bei halisi za ardhi katika maeneo yao ili kutowapoteza.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Buhigwe wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Wilaya za Chama hicho leo tarehe 23 Machi 2023.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 23 Machi 2023 ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inaotekelezwa katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa barabara ya Buhigwe - Muyama – Kasumo. Amesema barabara hiyo ni jitihada za serikali katika kuufungua mkoa wa Kigoma na kuunganisha na mikoa mingine pamoja na nchi jirani hivyo kuchochea biashara na ukuaji wa uchumi kwa wananchi.

Amewataka viongozi wa chama na serikali katika mkoa huo kuwa na ushirikiano ili kufanikisha miradi kwa haraka zaidi na kwa ufanisi.

Makamu wa Rais amewataka wananchi kutambua gharama za maendeleo ni pamoja na kujitoa hivyo wanapaswa kuunga mkono tathimini na fidia zitakazotolewa na serikali kupisha ujenzi wa mradi huo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kasumo na nyumba za wahudumu wa afya wa zahanati hiyo,mradi unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na serikali.

Amewapongeza wananchi wa Kijiji hicho kwa kujitolea kuongeza eneo la zahanati hiyo pamoja na kutoa mchango wa hali na mali katika utekelezaji wa mradi huo na kuwaasa kuendelea kutoa mchango wao katika miradi mingine.

Makamu wa Rais amesema serikali itafanya ukarabati wa nyumba za walimu katika shule ya msingi Lemba iliopo jirani na zahanati hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto ya uchakavu kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana kidato cha tano na sita yenye jumla ya majengo 18 inayojengwa katika kata ya kajana Kijiji cha kasumo.

Pia amekagua ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilaya ya Buhigwe, Mradi wa Ujenzi wa Ofisi za Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Buhigwe pamoja na Ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Wilaya hiyo.

Makamu wa Rais amewasihi wakandarasi kuendelea kutoa fursa kwa wazawa wa maeneo husika ya ujenzi ili waweze kujiinua kiuchumi.

Pia amewataka wananchi wa wilaya ya Buhigwe kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutumia vema fursa za miradi iliopo wilayani humo kujipatia maendeleo.

Pia Makamu wa Rais amewataka wananchi hao kutoa kipaumbele katika elimu kwa kutumia vema fursa iliotolewa na serikali ya awamu ya sita kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news