MIWILI YAKE SAMIA-3: Kila sekta Kazi Inaendelea

NA LWAGA MWAMBANDE

NDANI ya miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, licha ya kufanya mambo mengi kwa ustawi bora wa Taifa, pia amefanikiwa kuipaisha Sekta ya Utalii.

Aprili 28,2022 jijini Arusha wakati akizindua rasmi filamu ya Tanzania Royal Tour katika ukumbi wa mikutano wa AICC, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia aliwataka Watanzania kuiunga mkono filamu hiyo, kwani ni kwa faida yao na maslahi mapana ya Taifa.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alisema kuwa,filamu hiyo itasaidia kuchochea utalii kwa nchi yetu, kwani baada ya kukamilika na kuanza kuoneshwa katika nchi mbalimbali imeweza kuchochea utalii huku wengi wao wakitaka kuja kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali.

Pia aliwataka watanzania wote watakaopata fursa ya kujionea filamu hiyo kuwa mstari wa mbele kuisambaza ili iweze kuinufaisha nchi na kuwavutia watalii wengi zaidi.

“Katika uandaaji wa filamu hii nimekutana na matatizo mengi sana ikiwemo kutungiwa jina la Rambo (John James Rambo) na jina la Shoznigger (Arnold Alois Schwarzenegger) kutokana na kuigiza filamu hiyo kwa kuwa nje ya ofisi siku nane kwa kuitengeneza hiyo filamu huku nikiambiwa suala la urais niweke pembeni.

“Sijawahi kuandaa filamu, ndio ugumu ulikuja hapo kutokana na kuwa nje siku nane na kuacha shughuli za utendaji wa urais, halikuwa suala jepesi kabisa ila namshukuru Mungu kwa kuwa tumefanikisha hilo,”alisema.

Rais Samia alisema kuwa, filamu hiyo italipa mara dufu kwa jinsi ilivyotengenezwa kwa umakini mkubwa na hiyo ni kwa maslahi ya nchi kwa sababu ni mara ya kwanza kutengenezwa na gwiji maarufu duniani.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, filamu ya Royal Tour ndani ya kipindi kifupi imeleta matokeo makubwa katika Sekta ya Utalii nchini, licha ya sekta hiyo kuathiriwa na vikwazo vya UVIKO-19 duniani na Taifa linaendelea kujivunia uongozi wake ambao umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Endelea;


51.Uchumi wa Tanzania,
Nao wauangalia,
Hutaki ukasinzia,
Heko Rais Samia.

52.Tangu ulipoingia,
Urais Tanzania,
Makubwa twayapitia,
Heko Rais Samia.

53.UVIKO liikutia,
Dunia kishambulia,
Uchumi ulititia,
Heko Rais Samia.

54.Bado haijaishia,
Japo tunafurahia,
Dunia inatulia,
Heko Rais Samia.

55.UVIKO kuangalia,
Vita mpya kaingia,
Ukraine nakwambia,
Heko Rais Samia.

56.Imezidi kuchangia,
Hali ngumu ya dunia,
Bado twajipigania,
Heko Rais Samia.

57.Chakula bei sikia,
Kali tunalialia,
Hali unafwatilia,
Heko Rais Samia.

58.Nchi kuitumikia,
Mitaji unavutia,
Twaona inaingia,
Heko Rais Samia.

59.Kwingi unakufikia,
Vema tuwakilishia,
Inatajwa Tanzania,
Heko Rais Samia.

60.Kwa ramani ya dunia,
Yasikika Tanzania,
Yavutia Tanzania,
Heko Rais Samia.

61.Kikubwa litufanyia,
Matunda yanaingia,
Royal Tour nakwambia,
Heko Rais Samia.

62.Ulivyotutangazia,
Utalii Tanzania,
Ikasikia dunia,
Heko Rais Samia.

63.Watalii waingia,
Kotekote Tanzania,
Vile uliwavutia,
Heko Rais Samia.

64.Zanzibar wanaingia,
Na mbuga za bara pia,
Pesa safi zaingia,
Heko Rais Samia.

65.Pesa zilizoingia,
Za kigeni nakwambia,
Nyingi tunafurahia,
Heko Rais Samia.

66.Kwa wageni kuingia,
Ni neema Tanzania,
Sisi tunafurahia,
Heko Rais Samia.

67.Kwa wengi Watanzania,
Kazi ndiyo zaingia,
Mnyororo nakwambia,
Heko Rais Samia.

68.Hoteli zafurahia,
Hata wapagazi pia,
Mifuko yajitunia,
Heko Rais Samia.

69. Mboga kuwahudumia,
Na magari yetu pia,
Ni pesa zinaingia,
Heko Rais Samia.

70.Vinyago kuwauzia,
Na kuwatafsiria,
Kazi tunafurahia,
Heko Rais Samia.

71.Nje ametangulia,
Milango tufungulia,
Kote tunamsikia,
Heko Rais Samia.

72.Wakati akiingia,
Wengine lifikiria,
Hapa kazi tafifia,
Heko Rais Samia.

73.Inaendelea pia,
Kazikazi nakwambia,
Mengi yanayovutia,
Heko Rais Samia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news