Mzani wa Rubana kukamilika Mei, Serikali yatoa maagizo

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya CHICO anayejenga mzani wa Rubana utakaokuwa unapima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion), uliopo katika barabara kuu ya Mpakani mwa Simiyu na Mara hadi Sirari kuongeza kasi ya ujenzi wake ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2023.
Agizo hilo limetolewa wilayani Bunda na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, mara baada ya kukagua ujenzi wa mzani huo unaogharimu kiasi cha Bilioni 22.2 na kusisitiza kuwa hakuna changamoto yoyote ya malipo kwa mkandarasi na mhandisi mshauri ya kusababisha ucheleweshwaji wa mradi huo.

"Niwahakikishie kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kujenga na kusimamia uboreshaji wa miundombinu hapa nchini kwa jicho la pekee na ndio maana fedha zinapelekwa kila kona ya nchi na miradi inaendelea,"amefafanua Mhandisi Kasekenya.

Mhandisi Kasekenya ametaja umuhimu wa ujenzi wa mizani hapa nchini ikiwemo kuilinda miundombinu ya barabara na madaraja ambayo inajengwa kwa fedha nyingi.

Ameeleza pia uwepo wa mizani inaondoa usumbufu kwa watumiaji wa barabara kwani wasafirishaji watapimwa huku wakiwa kwenye mwendo na watasimama endapo watakuwa wamezidisha uzito kwa ajili ya kupima zaidi.

Vilevile uwepo wa mizani za kisasa nchini utaepusha kupitisha magendo kwa njia ya barabara hasa ukizingatia barabara hii ni kuu inaunganisha nchi na nchi.

Kasekenya amefafanua kuwa mizani hiyo pindi itakapokamilika ndiyo itakuwa kubwa, bora na ya kisasa katika Ukanda wa Ziwa maana itafungwa scanner yenye kuonesha kila kitu kilichobebwa ndani ya malori na vyombo vingine vya moto.

"Mizani hizi ni kwa ajili ya kusaidia barabara zetu zidumu zaidi hii ndio kitu ambacho kinafanya wasafirishaji wasizidishe mizigo na kuipunguzia Serikali gharama kubwa za ukarabati wa barabara," amesema Naibu Waziri huyo.

Akitoa taarifa ya mradi Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS),Mhandisi Vedastus Maribe, ameeleza kuwa maendeleo ya ujenzi wa mzani huo umefikia asilimia 50.6 na wanaendelea kuusimamia mradi ukamilike kwa muda uliopangwa.

Mhandisi Maribe ameongeza kuwa tayari kiasi cha Milioni 430 zimetumika kulipa wananchi kwa ajili ya fidia na eneo lipo wazi kwa ajili ya ukamilishaji wa mzani huo.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Mara katika ziara ya ukaguzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Sekta ya Ujenzi

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news