Polisi yafutilia mbali maandamano ya Raila Odinga kesho

NA DIRAMAKINI

KAMANDA wa Jeshi la Polisi Nairobi nchini Kenya, Adamson Bungei amesema, maombi mawili ya maandamano ya Azimio la Umoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Nairobi yamekataliwa kwa kutokidhi matakwa ya kisheria.

Azimio la Umoja, muungano wa kisiasa unaoongozwa na Raila Odinga, umepanga kufanya maandamano Jumatatu kudai mageuzi ya uchaguzi na kushinikiza Serikali kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha. Hata hivyo, Bungei amesema hawakutoa taarifa polisi siku tatu kabla kama inavyotakiwa na Sheria ya Usalama wa Umma.

"Tumepokea maombi. Moja lilikuja jana jioni na moja leo asubuhi. Moja kutoka Azimio la Umoja na moja kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Nairobi. Hata hivyo, wote wawili hawajakidhi vigezo vya sheria na maombi yao yamekataliwa,” Bungei alisema.

"Sheria ya Utaratibu wa Umma Kifungu cha 5 kinasema mtu yeyote anayekusudia kufanya maandamano lazima aarifu polisi siku tatu kabla, lakini si zaidi ya siku 14," aliongeza.

Kulingana na Bungei, Azimio waliwasilisha ombi lao Jumamosi saa 10 jioni huku lile la Jumuiya ya Biashara ya Nairobi likiwasilisha leo Jumapili asubuhi.

Bungei pia amesema, Ikulu ambayo Azimio la Umoja ilikusudia kuandamana ni eneo lisiloruhusiwa na hakuna mtu anayeruhusiwa kwenda humo iwe kwa amani au la.

"Nyumba ile ya Serikali imetajwa kuwa ni eneo muhimu. Chini ya sheria za Kenya, ni eneo lisiloidhinishwa. Wakenya lazima waongozwe na sheria, sio watu wa maslahi. Huruhusiwi katika maeneo fulani, iwe kwa amani au la,” amesema.

Ameonya kuwa, mtu yeyote anayepanga uvunjifu wa amani atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria na kuongeza kuwa kesho kutakuwa na shughuli kama kawaida na hakuna barabara itakayofungwa.

Bungei amesema, mtu mwingine yeyote ambaye anakidhi vigezo vya Sheria ya Utaratibu wa Umma anaruhusiwa kuandamana kwa amani na bila silaha kama inavyothibitishwa na Ibara ya 37 ya Katiba. Amesema kuwa, polisi wanaongozwa na Katiba ili kulinda maisha na kulinda amani.

“Tungependa kuwahakikishia Wakenya wote na watu wenye nia njema ndani ya Jiji la Nairobi kwamba tumechukua hatua zinazofaa za usalama ili kuhakikisha usalama wa umma na uhuru wa kutembea katika ngazi zote. Hata hivyo, tunatoa angalizo kwamba mtu yeyote atakayevunja amani au kuvunja sheria wakati wa maandamano hayo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,”amesema.

Chini ya Raila Odinga, upinzani nchini Kenya umekuwa ukiandaa maandamano katika kaunti tofauti za taifa tangu kuanza kwa mwezi huu. Hata hivyo, maandamano ya Kisumu yalisababisha vurugu.

Upinzani ulikuwa umetoa muda wa siku 14 kwa serikali kuzingatia, siku hizo zitakamilika tarehe 20 mwezi huu. Moja ya masharti ni kwa serikali kupunguza gharama ya maisha, mageuzi kwenye taasisi inayosimamia uchaguzi ambapo tayari Rais William Ruto ameteua jopo la kuwachagua makamishna wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya IEBC.

Pia,upinzani unataka seva ya uchaguzi mkuu ifunguliwe, wakidai kuwa kura za Raila ziliibiwa. Rais Ruto amesema hilo halitafanyika akidai kuwa seva zilifunguliwa upinzani ulipowasilisha kesi katika Mahakama ya Juu. Raila ameapa kufanya maandamano ya amani.

Hayo yanajiri huku viongozi wa dini wakishauri viongozi hao kutafuta suluhu kupitia mazungumzo. Baraza la Makanisa nchini Kenya tayari limekutana na Rais William Ruto na Raila Odinga katika nyakati tofauti kujaribu kutafuta mwafaka.

Aidha, Raila ameapa kuwa wakati huu hataitikia salamu za heri kama ilivyofanyika katika utawala wa Rais Mwai Kibaki mwaka 2007 na Uhuru Kenyatta mwaka 2017.

Kwa upande wake, Rais ameshikilia kuwa wakati huu hapatakuwa na serikali ya nusu mkate. Raila amewataka wafuasi wake kuandamana jijini Nairobi siku ya Jumatatu, akisema Wakenya wana haki ya kufanya maandamano.(ntv,dw)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news