Serikali yafunguka kuhusu ugonjwa usiojulikana Kagera

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imesema kuwa, imepokea taarifa za uwepo wa ugonjwa ambao bado haujajulikana huko katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega vilivyopo Kata ya Maruku na Kanyangereko, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Hayo yamebainishwa leo Machi 16, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini J.Nagu.

Mganga Mkuu wa Serikali amefafanua kuwa,kwa mujibu wa taarifa hizo jumla ya watu saba wanasadikika kupata dalili za homa, kutapika, kutokwa na damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi.

Pia, Prof.Nagu amefafanua kuwa, watu watano kati yao wamefariki na wengine wawili wako hospitali wakiendelea na matibabu.

"Mwendo wa ugonjwa huu unaashiria uwezekano kuwa ni ugonjwa wa kuambukiza. Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu na kuchukua hatua za kudhibiti ili usisambae,"amefafanua Mganga Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miongoni mwa hatua ambazo Serikali inachukua ni kuchukua sampuni kutoka kwa wagonjwa na waliofariki ili kubaini chanzo na kuthibitisha aina ya ugonjwa huo.

Aidha, hatua nyingine ni ufuatiliaji wa watu wenye viashiria vya ugonjwa kwenye jamii na vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na waliotangamana na wagonjwa hao ili kuwapa huduma stahiki za kimatibabu.

"Timu za kitaalamu za kukabiliana na mlipuko ngazi ya mkoa na halmashauri zimetumwa katika maeneo yaliyoathirika na zinaendelea na uchunguzi na hatua za udhibiti,"amefafanua Prof.Nagu kupitia taarifa hiyo.

Wakati huo huo, Prof.Nagu amefafanua kuwa, hatua nyingine ni dawa, vifaa na vifaa tiba muhimu tayari vipo katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Kagera na wagonjwa wanaendelea na matibabu. Amefafanua kuwa, elimu ya afya inaendelea kutolewa kwa jamii katika Mkoa wa Kagera ili kuchukua tahadhari.

"Wakati Serikali inafuatilia mwenendo wa ugonjwa na kuchukua hatua za udhibiti, wananchi naomba muendelee kuwa watulivu na kuchukua hatua zifuatazo, mosi mtu yeyote mwenye dalili za homa, kutapika, kuharisha, kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu anashauriwa kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya mapema kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

"Pili, kutoa taarifa mapema kwenye kituo cha kutolea huduma kilicho karibu au kupiga simu namba 199 bila malipo endapo utamuona au kukutana na mtu mwenye dalili kama hizo.

"Tatu, kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili mfano mate, machozi, damu, mkojo na kinyesi yatokayo kwa mgonjwa au mtu yeyote mwenye dalili hizo.

"Nne, iwapo itakulazimu kumhudumia mgonjwa kwa dharura chukua tahadhari ya kujikinga na majimaji yoyote kabla ya kumhudumia.

"Tano, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na magonjwa yote ya kuambukiza. Sita, kuepuka kusalimiana kwa kushikana mkono na mwisho kushirikisha wataalamu wa afya katika shughuli za misiba na mazishi katika kipindi hiki,"amefafanua kwa kina Prof.Nagu kupitia taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Serikali amewakumbusha watumishi wa afya kuzingtaia kanuni za kujikina na magonjwa ya kuambukiza (IPC) wakati wa kutoa huduma.

"Serikali inatoa pole kwa familia zilizoondokewa na wapendwa wao, Aidha, wananchi hawapaswi kuwa na hofu, kila mmoja anapaswa kuwa na utulivu wakati wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu na kuchukua hatua za udhibiti na tutaendelea kuwapa taarifa za mwenendo wa ugonjwa,"amefafanua Mganga Mkuu wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news