The Citizen waamuriwa kumlipa Mchechu fidia bilioni 2.5/-

NA DIRAMAKINI

GAZETI la The Citizen limeamuriwa na Mahakama Kuu ya Tanzania kumlipa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambaye kwa sasa ni Msajili wa Hazina, Nehemia Kyando Mchechu fidia ya shilingi bilioni 2.5 baada ya kuthibitika kuwa, taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo Machi 23, 2018 haikuwa na ukweli wowote.

Kupitia ukurasa wa mbele gazeti hilo liliandika habari iliyobeba kichwa cha habari, 'Kwa nini JPM alivunja Bodi ya NHC na kumng’oa Mchechu?' (Why JPM dissolved NHC Board, Sacked Mchechu).

Hukumu hiyo ya Kesi Na.48 ya 2021 imetolewa leo Machi 3, 2023 na Jaji Leila Mgonya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Wakili wa Mchechu, Aliko Mwamanenge na Wakili wa Gazeti la The Citizen, Ambrose Nkwera.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mgonya amesema, katika adhabu hiyo,The Citizen wanapaswa kumlipa Mchechu shilingi bilioni mbili kama fidia kwa kumchafulia jina alilolijenga kwa muda mrefu huku shilingi milioni 500 zikiwa ni kwa ajili ya kumsababishia hasara ya jumla.

Jaji Mgonya amefafanua kuwa, pia gazeti hilo linapaswa kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi ikiwemo kuandika habari ya kumuomba radhi Mchechu katika ukurasa wa mbele.

Amesema, radhi hiyo inapaswa kuombwa kwa ukumbwa ule ule wa Machi 23, 2018 na watalipa riba ya asilimia 12 kila mwaka endapo watashindwa kulipa fedha hizo kwa wakati kuanzia leo Machi 3, 2023.

Pia,Mahakama hiyo imelionya The Citizen na kulitaka kutomwandika tena Mchechu kwa habari za uongo na zenye kumchafulia jina kwa namna hiyo, isipokuwa tu pale ambapo wanakuwa na ushaidi na vielelezo vya kutosha kwa ajili ya habari. Pia Mahakama imetoa nafasi ya upande wa mlalamikiwa kukata rufaa iwapo hajaridhika na maamuzi hayo.

Hivi karibuni Mchechu aliiomba Mahakama iamuru Gazeti la The Citizen kumlipa fidia ya shilingi bilioni tatu na kumwomba radhi, kwa madai ya kumchafulia jina na kushusha hadhi na heshima yake katika jamii.

Aidha,habari hiyo iliainisha sababu kadhaa kutoka vyanzo vyake mbalimbali, zinazodaiwa kuwa sababu za Rais wa Awamu ya Tano,Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, kuchukua uamuzi wa kuivunja Bodi ya NHC na kumuondoa Mchechu.

Jaji Mgonya amesema, baada ya wahariri wa gazeti la The Citizen kuwasilisha ushaidi na vielelezo vyao mahakamani hapo, havikuthibitisha tuhuma zilizoelekezwa kwa Mchechu kupitia habari hiyo, hivyo Mahakama haikubaini ukweli wowote.

Baadhi ya tuhuma zalizoibuliwa kwenye habari hiyo, ni pamoja na madai kwamba Mchechu alikuwa akichunguzwa na Bodi ya Wakurugenzi ya NHC na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu mgongano wa madaraka juu ya ununuzi wa ekari 500 za mradi wa NHC Safari City, Arusha.

Pia gazeti hilo lilidai kuwa Mchechu anachunguzwa na TAKUKURU kwa madai ya kumtumia mkandarasi aliyekodishwa na NHC, kujenga barabara yake binafsi karibu na mradi huo wa NHC Safari City.

Kuhusu mradi wa Kawe, gazeti hilo lilidai kuwa Mchechu aliingia makubaliano na kampuni ya ukandarasi ya PHILS International yenye makao yake Dubai, bila kushirikisha kitengo cha ununuzi wa NHC.

Hoja zingine zilizotajwa kwenye habari hiyo, ni kuhusu madai kwamba Mchechu anachunguzwa kwa tuhuma kuwa kampuni ya mkewe, ilipewa zabuni ya kutoa huduma za bima kwenye nyumba za NHC Mtwara, hali ambayo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Madai ya mwisho yaliyotajwa na gazeti hilo ni tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi yaliyotajwa kwa kiwango kikubwa.

Wakili wa Mchechu

Nje ya Mahakama, Wakili wa Mchechu, Aliko Mwamanenge amesema, kwa upande wao wameridhika na uamuzi wa mahakama.

"Hii ilikuwa ni kesi ya malalamiko dhidi ya Gazeti la The Citizen na kikubwa ilikuwa inahusu kushushiwa hadhi au heshima kwa mteja wetu Nehemia Kyando Mchechu, nafikiri wote mlipata kujua hili halikuwa geni machoni pa watu lilianzia Dodoma kwenye uongozi uliopita wa Rais John Pombe Joseph Magufuli.

"Alitoa maelezo mafupi akiwa anazindua mradi kule Dodoma, lakini kwenye ule mradi kuna maneno aliyaongea ambayo kimsingi hayakuenda mbali zaidi kama yale ambayo yalitolewa kwenye magazeti na ndio sababu Nehemia Kyando Mchechu akaamua kulalamika kwamba yale maneno mengi yalikuwa sio ya ukweli na baada ya kuja mahakamani tunashukuru Mungu.

"Mahakama imeona kweli yale maneno mengi hayakuwa na ukweli, hivyo kutoa maamuzi dhidi ya Gazeti la The Citizen kwamba watatakiwa kumlipa Nehemia Kyando Mchechu shilingi bilioni mbili kama sehemu ya kosa walilolifanya, lakini pia kulipa general damage kiasi cha shilingi milioni 500.

"General damage ni gharama ambazo huwezi kuzitamka, huwezi kusema ni kiasi gani unadai hizo ni mahakama ndio inatoa sio mtu anaweza kusema anatoa kiasi gani.

"Lakini pia wanatakiwa wa-apologies kutoa ile statement kwenye gazeti lile lile la The Citizen front page. Moja ya lalamiko kubwa lilikuwa ni kwenye ile front page ya gazeti la The Citzen waliandika huyu mtu amekuwa sacked maana yake mtu yuko fired na mtu akiwa fired maana yake kama kuna alegations zilitokea maana yake ni kweli, lakini at that point wakati wanaandika hilo gazeti huyu mtu hakuwa fired alikuwa suspended kwa hiyo suspended na kuwa sacked ni vitu viwili tofauti na mahakama imeona kweli hilo ni sahihi."

Na tuhuma nyingine ambazo zilitolewa kwenye gazeti hazikutolewa kwenye TV ya AZAM ambao walileta ushahidi. Hawajapewa muda lini walipe, lakini wanatakiwa walipe kuanzia sasa hivi.

"Pia kuna wamepewa conditions tano ya kwanza wanatakiwa waombe radhi kwenye gazeti lile lile, ya pili wanatakiwa wasirudie tena kumpublish huyu mtu kwa kumtukana au kumshushia hadhi, lakini tatu wanatakiwa walipe shilingi bilioni mbili kama sehemu ya defamation, halafu wanatakiwa walipe compasation ya shilingi milioni 500 ya general damages kama nilivyosema na mwisho ya tano wanatakiwa walipe gharama za kesi.

"Malalamiko yaliletwa kama nakumbuka vizuri yaliletwa mwaka jana mwanzoni 2022 kama nakumbuka vizuri na of-course tumeshachukua almost mwaka mzima au zaidi tukiwa mahakamani mpaka leo umetoka uamuzi,"amefafanua Wakili Mwamanenge.

Wakili wa The Citizen

Katika hatua nyingine, nje ya Mahakama Wakili wa Gazeti la The Citizen, Ambrose Nkwera hakuweza kuzungumza chochote kuhusu uamuzi huo wa Mahakama leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news