TUJITIBU KIVINGINE:Mazoezi dawa,Vyakula asilia, Kulia ni dawa, Kushirikishana dawa

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, magonjwa yanayoambukiza kama vile ya wanyama kwenda kwa wanadamu, yanayohusiana na zinaa, kifua kikuu,malaria,kipindupindu,homa ya manjano na kichocho bado ni tatizo kubwa kwa nchi nyingi zinazoendelea.

Pia nchi hizo kwa sasa zinakabiliwa na tatizo linaloongezeka kwa haraka la magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kisukari, saratani,magonjwa ya akili, dawa za kulevya zikiwemo ajali.

Wataalam wa afya wanasema kuwa, kati ya vyanzo vya magonjwa haya ni ulaji usiofaa, kutoshughulisha mwili, matumizi ya tumbaku na kunya pombe kupita kiasi, vyote ambavyo vinahusiana na mtindo wa maisha.

Changamoto iliyopo ni ya kwamba, wakati bado kuna wanajamii wengi wenye lishe hafifu, wako wengi wenye lishe ya kutosha, lakini isiyo bora.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ili kukabiliana na magonjwa hayo unaweza kufanya uamuzi sahihi ikiwemo kutumia vyakula vya asili kwa wingi na mazoezi au kushirikishana mawazo na watu sahihi. Endelea:

1.Hospito kuna dawa, na nyumbani kuna dawa,
Nzuri sana zile dawa, za nyumbani twaambiwa,
Bila ugonjwa ni dawa, hata kwa ugonjwa dawa,
Tukwepe hospitali, tujitibu kivingine.

2.Fanya zoezi ni dawa, huwezi ukauguwa,
Hata kufunga ni dawa, ndivyo tunavyoambiwa,
Chakula asili dawa, kicheko nacho ni dawa,
Tukwepe hospitali, tujitibu kivingine.

3.Mboga na matunda dawa, usingizi pia dawa,
Mwanga wa jua ni dawa, kuwapenda watu dawa,
Kushukuru hiyo dawa, hata yule anapewa,
Tukwepe hospitali, tujitibu kivingine.

4.Kujipenda hiyo dawa, kujiona sawasawa,
Sahau kosa ni dawa, kutafakari ni dawa,
Kusoma Neno ni dawa, Mungu unamuelewa,
Tukwepe hospitali, tujitibu kivingine.

5.Fikra chanya ni dawa, kumwishia Mungu dawa,
Marafiki bora dawa, kunywa maji mengi dawa,
Kujisamehe ni dawa, samehe wengine dawa,
Tukwepe hospitali, tujitibu kivingine.

6.Moyo wa amani dawa, kutosheka pia dawa,
Kutabasamu ni dawa, kucheka sana ni dawa,
Hata kulia ni dawa, kushirikishana dawa,
Tukwepe hospitali, tujitibu kivingine.

7.Kunywa sana hizo dawa, epuka duka la dawa,
Mwili hutasumbuliwa, na wala kuchafuliwa,
Afya imarishiwa, na malengo kufikiwa,
Tukwepe hospitali, tujitibu kivingine.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news