Musoma Vijijini waiomba Serikali kuongeza kasi ujenzi wa barabara kiwango cha lami

NA FRESHA KINASA

KUFUATIA mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, zimeleta maafa kwa baadhi ya vijiji vilivyoko pembezoni mwa barabara ya Musoma-Makojo-Busekera ambapo wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wametoa ombi kwa Serikali kuipa kipaumbele ikiwemo kuwezesha ukamilishaji wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 92 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa kutoa fedha ambazo zitawezesha kukamilika ujenzi wake. 

Hayo yamebainishwa na wananchi hao kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Aprili 3, 2023 ambapo wananchi hao wametoa ombi hilo wakiwa eneo la maafa Kijiji cha Kusenyi katika kitongoji cha Kwikuyu wakiiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo.
"Jana usiku na leo asubuhi, Kijiji cha Kusenyi, Kitongoji cha Kwikuyu kimekubwa na mafuriko makubwa. Wakazi wa hapo wamepoteza mali zao, kikiwemo chakula walichokuwa wamehifadhi majumbani mwao.

"Mkandarasi aliyejenga kilomita 5 kwenye hii barabara ya urefu wa kilomita 92 tunamlalamikia kwa kuziba vidaraja vidogo vidogo vilivyokuwa vinapitisha maji kwenda ziwani Ziwa Victoria. 

"Umuhimu wa barabara ya Musoma-Makojo-Busekera. Vijiji 68 vya Musoma Vijijini vinaunganishwa na barabara kuu moja tu, ambayo ni hii ya Musoma-Makojo-Busekera. Barabara hii inaunganisha Musoma Vijijini na Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara, na hatimae inaunganisha Musoma Vijijini na mikoa ya jirani ya Mwanza, Simiyu, Manyara na Arusha. 

"Barabara hii inaunganisha Musoma Vijijini na Kiwanja cha Ndege cha Musoma Mjini na Mwanza), na Bandari ya Meli iliyopo Musoma Mjini. Mazao ya uvuvi (dagaa, sangara na sato) yanasafirishwa kutumia barabara hii. Mazao ya Kilimo, yaani, mihogo, viazi vitamu, mpunga, mahindi, mtama, matunda, mbogamboga, pamba, alizeti, n.k. yanasafirishwa kutumia barabara hii. Dhahabu na madini mengine yanasafirishwa kutumia barabara hii," imeeleza taarifa hiyo. 

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo na viongozi wengine wa CCM na Serikali wanaendelea kuiomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ijengwe kwa kiwango cha lami tangu mwaka 1980 - 2023.

"Maombi ya wana Musoma Vijijini na viongozi wao juu ya barabara hii ni kujengwa kwa kiwango cha lami ni tokea mwaka 1980," imeeleza taarifa hiyo. 
Aidha, DIRAMAKINI imezungumza na Nehemia Bwire na Ester Pius wakazi wa Makojo ambapo wamesema, "ninaimani kubwa na Mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyochapa kazi za maendeleo kwa dhati na kutoa fedha nyingi katika miradi mingi mikubwa na ya kimkakati. 

"Tunatarajia atasaidia pia kutoa fedha kusudi barabara hii ijengwe ikamilike haraka maana ikijengwa itachangia sana maendeleo yetu wananchi, na pia hata maafa ya mafuriko tutaondokana nayo,"amesema Bwire. 

"Serikali yetu ni sikivu Sana nina uhakika Wizara yenye dhamana itaona umuhimu wa kuijenga barabara hii kutokana na umuhimu wake. 

"Mbunge anapambana na viongozi wa chama pia wako pamoja na Serikali. Na Serikali iliyopo madarakani ya CCM, kwa hiyo ninaimani kabisa fedha zitatolewa na hili ni ombi letu wana Musoma Vijijini kuona barabara hii kwa kiwango cha lami inakamalika mapema, naomba serikali isikie ombi letu," amesema Ester Pius.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news