NA JAMES MWANAMYOTO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Angellah Kairuki amewataka Wakurugenzi, Wakuu wa Idara, Mameneja na Maafisa wanaosimamia utawala na rasilimali watu katika taasisi za umma kuhakikisha wanawasimamia vema wataalam na watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya kimkakati ya Serilikali.
Lengo likiwa ni wananchi wanufaike na miradi hiyo kama ilivyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.
Mhe. Kairuki ametoa wito huo kwa wasimamizi wa utawala na rasilimaliwatu jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene.
Mhe. Kairuki amesema wataalamu hao wa utawala na rasilimaliwatu ndio wenye jukumu la kuhakikisha waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ya kimkakati, wanatekeleza miradi hiyo kwa wakati, uadilifu na kwa kuzingatia ubora ili iwe na manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Kairuki amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika kuishauri Serikali kuhusiana na masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu ili kuwa na rasilimaliwatu itakayotoa mchango katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na maendeleo ya taifa.
Sanjari na hilo, Mhe. Kairuki amewataka wataalam hao wa utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu kutoka katika taasisi za umma nchini kutumia ujuzi na weledi wao kuishauri Serikali namna bora ya usimamizi wa rasilimaliwatu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi amesema, ofisi yake inatarajia mkutano huo wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania utaongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa wasimamizi hao wa masuala ya utawala na rasilimaliwatu nchini. “Mkutano huu utakuwa na msaada mkubwa kwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika kuyatafutia ufumbuzi masuala mbalimbali ya kiutumishi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi na wadau wa taasisi zetu za umma,” Bw. Mkomi amefafanua.
Bw. Mkomi hakusita kuwataka Wakurugenzi, Wakuu wa Idara, Mameneja na Maafisa wanaosimamia utawala na rasilimaliwatu katika taasisi za umma kuhakikisha Makatibu Muhtasi wao kutojikweza na kuwa kikwazo kwa wananchi na wadau wanaofuata huduma katika ofisi zao.
Bi. Mavika amesema jumla ya washiriki 281 kutoka katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Taasisi za Umma.