Waziri Mkuu atoa wito mapambano dhidi ya dawa za kulevya Tanzania

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wote nchini kushirikiana na Serikali kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito huo leo Aprili 5, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.

"Nitoe wito kwa wadau wote mkiwemo waheshimiwa wabunge wenzangu, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyombo vya habari na jamii nzima kushirikiana na Serikali kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho,"amesisitiza Waziri Mkuu.

Pia amesema, Serikali kwa kutambua madhara ya dawa za kulevya kwa nguvu kazi hapa nchini, imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya dawa hizo.

Waziri Mkuu amefafanua kuwa, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendesha oparesheni za kuwakamata wanaojihusisha na biashara hiyo pamoja na kuzuia mianya ya kusafirisha na kusambaza dawa hizo.

Katika oparesheni hizo watuhumiwa 7,113 pamoja na kilogramu 20,450.30 za dawa za kulevya zilikamatwa. Dawa hizo ni heroin kilogramu 53.01, cocaine gramu 843.55, bangi kilogramu 12,869.39, mirungi kilogramu 7,525.53, na aina nyingine ya dawa za kulevya (Methamphetamine na Mescaline) gramu 1,024.7.

Aidha, iliteketeza ekari 69 za mashamba ya bangi katika maeneo mbalimbali nchini na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.

"Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuongeza idadi ya kliniki zinazotoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya kutoka 9 mwaka 2020/2021 hadi kliniki 15 zinazohudumia waathirika zaidi ya 14,500 mwaka 2022/2023.

"Licha ya hayo, Serikali kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi imewezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu wapatao 245 kupata mafunzo ya ujuzi kupitia vyuo vya VETA, Don Bosco na SIDO,"amebainisha Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kusimamia na kuratibu uendeshwaji wa nyumba za upataji nafuu 44 nchini, kuzijengea uwezo asasi za kiraia 65 ambazo zinatoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa jamii.

Sambamba na kuandaa Mwongozo wa Utoaji Elimu kuhusu Tatizo la Dawa za Kulevya nchini ambao umezinduliwa Julai 2, 2022 kwa lengo la kuwapatia elimu na mbinu sahihi kulingana na mahitaji ya makundi mbalimbali ya kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news