Dodoma waendelea kuimarisha miundombinu katika Sekta ya Elimu na Afya

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI mkoani Dodoma imeendelea kuimarisha miundombinu katika sekta ya Elimu na Afya kwa lengo la kuboresha na kusogeza huduma kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Chemba kukagua miradi ya maendeleo.
Bw. Gugu ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa madarasa, maabara na zahanati katika Vijiji vya Jangalo, Soya na Ombiri ambapo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho na umegharimu kiasi cha Shilingi millioni 90.6 kwa madarasa 12 na maabara 1, kwa upande wa ujenzi wa zahanati umegharimu kiasi cha Shilingi millioni 50.

"Ndugu zangu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha miradi hii ya maendeleo, nitoe rai kwenu kwanza kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati, pili miradi ikamilike kwa ubora wa hali ya juu,” Gugu amesisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Bi. Siwema Jumaa amesema mbali ya fedha kutoka Serikali kuu utekelezaji wa miradi hiyo ni pamoja na jitihada za nguvu za wananchi ambao kwa baadhi ya majengo ya zahanati na madarasa wananchi wamejenga maboma.

Pia, amewataka wakazi wa vijiji vya Jangalo ,Soya na Ombiri kuwa walinzi namba moja wa miradi hiyo kwa kuwa inaghariimu fedha nyingi za Serikali.
Ziara ya Bw. Gugu ilianzia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Chemba na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kuongea na watumishi na kufanikiwa kukagua umaliziaji wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya Msingi Ombiri, ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa, jengo la Utawala, matundu 30 ya vyoo katika shule ya Msingi Soya, umaliziaji wa chumba 01 cha maabara shule ya Sekondari Jangaro na ujenzi wa Zahanati ya Mlongia.

Katika hatua nyingine Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Senga Gugu amefanikiwa kuongea na watumishi na kuwaasa kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano, kupendana na kufanya kazi kwa ubora na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news