Hakuna haki bila uwajibikaji katika utumishi wa umma-OWMS

NA MWANDISHI WETU

WATUMISHI wapya kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi kwa kuwa hakuna haki bila uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi.Sarah Mwaipopo (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya kufungua mafuzo elekezi kwa watumishi hao yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani. Wa pili kulia Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, James Kibamba wa Ofisi hiyo.(Picha na OWMS).

Hayo yamesemwa Mei 4, 2023 na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi.Sarah Mwaipopo wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo akifungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuhusu sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma. Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Cha Uongozi wa Mwalimu Nyerere Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumzia aina ya mafunzo yatakayotolewa, Bi.Mwaipopo amesema kuwa, ofisi hiyo imekusudia kuwajengea uewezo watumishi hao katika masuala mbalimbali yanayohusu majukumu yao, haki na wajibu wao kama watumishi wa umma.

Pia, muundo wa Serikali,taratibu za utendaji kazi,maadili, nidhamu,uadilifu na ustahimilivu ambavyo vyote kwa pamoja vinapaswa kuzingatiwa ili kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi wa umma hususani kwa ajira mpya.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha kwa ajil ya kufungua mafunzo elekezi ya siku mbili kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Ameeleza kuwa, mafunzo hayo ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ambapo ofisi imeona umuhimu wa kutenga bajeti ili kufanikisha mafunzo haya muhimu yatakayowajenga na kuwapa uelewa katika masuala mbalimbali ya kiutumishi.
Wakati huo huo, akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Bi.Mwaipopo amewaeleza kuwa, mafunzo hayo yatawasaidia katika kuimarisha utendaji kazi, nidhamu na maadili ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kuepuka makosa mbalimbali ya kinidhamu na yale ya kiutumishi ambayo yangeweza kufanyika kwa kukosa uelewa ili kuweza kuyaepuka wakiwa mahali pa kazi.

Aidha, amewataka watumishi wapya kujifunza na kuelewa vyema dira, dhima na misingi muhimu ambayo taasisi imejiwekea katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya usimamizi wa mashauri ya madai na usuluhishi yanayofunguliwa na au dhidi ya Serikali,ndani na nje ya nchi. 
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza kwa makini Bi. Sarah Mwaipopo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya (hawapo pichani) wa Ofisi hiyo yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Misingi hiyo amesema, inahusu uwajibikaji,uadilifu, uaminifu na weledi ambayo ikitekelezwa vyema ni nguzo ya maendeleo endelevu ya nchi yetu.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Francis Oswald ameishukuru ofisi kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu ambayo yatawawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
James Kibamba, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali akimkaribisha Bi. Saraha Mwaipopo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) kufungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo kuhusu sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamewahusisha watumishi 64 waajiriwa wapya wa ofisi hiyo wa kada mbalimbali ikiwemo mawakili wa Serikali 41, maafisa TEHAMA wawili,makatibu sheria wanne, makatibu muhtasi wanne, madereva tisa,watunza kumbukumbu wanne na afisa usafirishaji mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news