Kamishna Jenerali wa DCEA ashiriki uzinduzi wa muongozo maalumu nchini

NA DIRAMAKINI

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas James Lyimo ameshiriki hafla ya uzinduzi wa muongozo wa ushirikiano katika upelelezi na uendeshaji mashtaka ya utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi na ufadhili wa ugaidi.
Hafla hiyo ilifanyika Mei 24,2023 katika hoteli ya Best Western Dodoma City iliyopo 
Dodoma ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Damas Ndumbaro huku washiriki wakiwa ni wakuu wote wa Taasisi za Haki Jinai na wale wanaoguswa na mfumo mzima wa haki jinai kwa namna moja ama nyingine.
Taasisi hizo ni Ofisi ya Rais-Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Ofisi ya Taifa ya 
Mashtaka, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Taasisi ya Kuzuia na 
Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Kituo cha Taifa cha Kuratibu Mapambano Dhidi ya Ugaidi, Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Fedha Haramu, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Benki Kuu ya Tanzania na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,Lyimo amesema muongozo huo utasaidia katika kupambana na uhalifu wa kupangwa.
"Taasisi ninayoiongoza inahusika na kudhibiti dawa za kulevya, dawa za kulevya ni eneo mojawapo linalotumika sana katika utakatishaji wa fedha,kufadhili ugaidi pamoja na eneo la kutoa rushwa.
"Muongozo huu utatusaidia kwa kuwa tutashirikiana na taasisi zote katika kupambana na uhalifu wote wa kupanga ikiwemo utakatishaji wa fedha, utatusaidia kuunganisha nguvu sisi kama taasisi zinazohusika na kupambana na makosa 
hayo," amesema Aretas Lyimo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na 
Kupambana na Dawa za Kulevya. 
Maandalizi ya muongozo huo yamefanywa na wataalamu kutoka katika taasisi hizo na 
kukutana mara nne katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha kuanzia mwezi Januari 
hadi Mei, 2023 chini ya Uratibu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Aidha, mchakato mzima wa kuandaa hadi kuuzindua muongo husika umefadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa Ulaya kupitia Programu yake ya Mapambano dhidi Utakatishaji Fedha Haramu,Ugaidi na Ufadhili wa Ugaidi kwenye ukanda wa Kusini,Mashariki na Kati wa Afrika na Yemeni (European Union Anti Money Laundering and Counter Financing Terrorism Eastern Southern, Central Africa and Yemen (AML-CFT ESCAY).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news